Pages

Tuesday, December 1, 2020

WANANCHI WA MKURANGA KUPATA HUDUMA YA MAJISAFI IFIKAPO APRILI 2021

Mbunge wa Jimbo la Mkuranga,Abdallah Ulega (kulia) akipokea maelekezo ya ujenzi wa Mradi wa Maji katika Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga kutoka kwa,Erasto Mwakilulele ,Mhandisi wa Dawasa -Mkuranga , akimuwakilisha msimamizi wa mradi.
(Picha na Emmanuel Massaka michuzi Tv)
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega akizungumza na viongozi mabilimbali baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ujenzi ukiendelea katika chanzo cha maji cha wilaya ya Mkuranga.
Muonekano wa tanki la maji linalojengwa na Dawasa katika kata ya Mkuranga.
Muonekano wa jengo jipya  katika Hospital ya wilaya ya Mkuranga.WANANCHI wa Wilaya ya Mkuranga na maeneo jirani wapo mbioni kuondokana na adha ya ukosefu wa maji ya uhakika kutokana na ujenzi wa mradi wa maji ulioigharimu Serikali kiasi cha zaidi ya Sh Bilioni 2 wilayani humo, kufikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezwaji wake.

Hayo yamebainishwa na Meneja usimamizi wa mradi huo,Mhandisi Erasto Mwakilulele alipokuwa akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa wilayani humo.

Alisema matarajio ya wananchi wa wilaya hiyo kuanza kupata maji kutoka katika mradi huo, ni kuanzia Februari Mwakani mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa eneo litakalofungwa pampu za kusukuma maji ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 30 hadi sasa.

Alisema kwa upande wa tanki la kuhifadhia maji litakalokuwa na uwezo wa kubeba lita za maji milioni moja na nusu, ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 90 na kwamba kinachoendelea kwa sasa ni umaliziaji wa baadhi ya vitu wakisubiri kukamilika kwa ujenzi wa eneo zitakapofungwa pampu.

“Matarajio hadi kufikia Februari mwakani kazi hii itakuwa tayari imekamilika na wananchi waanze kupata maji kutoka katika mradi huu.” Alisema Mwakilulele

Kwa upande wake Mbunge Ulega, alimtaka Msimamizi wa mradi huo pamoja na mkandarasi kuhakikisha kazi ya ujenzi wa mradi huo inakamilika mapema iwezekanavyo ikibidi hata kabla ya kipindi hicho kufika ili kuondoa adha ya maji inayowapata wananchi. 

Alisema kwa giografia ya Mkuranga, Februari huwa ni kipindi chanye mvua nyingi hivyo endapo ujenzi huo utacheleweshwa hadi kufikia wakati huo ni wazi kuwa wananchi wa wilaya hiyo wataendelea kuusubiri kwa kipindi kisichojulikana, suala alilosema hapendi kuona likitokea.

Katika hatua nyingine Ulega amemuagiza Mkandarasi wa mradi huo kuwasilisha ofisini kwake utaratibu wa malipo anaoutumia kuwalipa wafanyakazi wanaojenga mradi huo baada ya uwepo wa malalamiko ya baadhi yao kuhusu malipo hayo.

Alisema hadi kufikia Saa 2 asubuhi ya kesho anahitaji taarifa hiyo iwe imefika katika Ofisi yake ili aweze kujua ni chanzo cha malalamiko hayo.

Mradi wa maji Mkuranga -Vikindu ni mradi inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Dar es salaam (DAWASA) na unatekelezwa kupitia fedha za ndani za Mamlaka kwa gharama ya Tsh 2.2 Bilioni.

 

No comments:

Post a Comment