Meneja miradi wa
shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini Emmanuel Mbise akizungumza
na wachekechaji wanaochekecha ndani ya ukuta unaozunguka madini ya
Tanzanite.
Wadau wanaochekecha migodi ya madini ya
Tanzanite wakiwa kwenye mafunzo ya usalama kazini yaliyotolewa na
shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini.
*********************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la
kiserikali la Haki Madini la jijini Arusha, limewajengea uwezo
wachekechaji wanaochekecha udongo ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya
madini ya Tanzanite, kwa kuwapatia elimu ya namna ya kujikinga na
madhara yatokanayo na shughuli wanazofanya.
Ofisa miradi wa
shirika la Haki Madini, Emmanuel Mbise akizungumza kwenye kijiji cha
Naisinyai Wilayani Simanjiro amesema lengo ni kuwajengea uwezo zaidi wa
kufanya kazi katika mazingira salama.
Mbise amesema katika
kufanya kazi za uchekechaji inatakiwa kuvaa vifaa vya kujikinga na vumbi
ili kuondokana na ugonjwa wa kifua kikuu na ulanga kuingia kwenye
kifua.
“Wakati wa kuchekecha
muwe mnamwagia maji katika udongo ili vumbi lisiingie vifuani na kwenye
mapafu kisha kupata TB na Silikosisi kupitia vumbi na ulanga unaokuwepo
wakati wa kazi,” amesema Mbise.
Amesema kufanya kazi
kwa muda mrefu hujenga majeraha kwenye baadhi ya viungo vya mwili na
mifupa hivyo tunapaswa kupumzika kila baada ya kzii na kufanya mazoezi.
“Pia kwenye shughuli
zetu hizi za uchekechaji wa madini tunapaswa kupumzika ili kuupa mwili
nafasi kwani madini yapo tuu yanatakiwa yatupe faida na yasituathiri,”
amesema Mbise.
Ofisa mtendaji wa
kata ya Naisinyai, Valentine Tesha amewataka wachekechaji hao 60
waliopatiwa mafunzo hayo wawe mabalozi wazuri kwa kutoa elimu
waliyoipata kwa wengine ambao hawakuipata.
Tesha amesema
washiriki hao wakisambaza elimu hiyo kwa baadhi ya wachekechaji ambao
hawajafika kwenye mafunzo hayo watakuwa nao wamejengewa uwezo.
Mmoja kati ya
wachekechaji hao, Isaya Maliyaki amesema wamekuwa wakitoa elimu
waliyoipata kwa baadhi ya vijana wachekechaji ila hawatekelezi.
Maliyaki amesema
baadhi ya vijana walevi wanawaeleza kuwa watumie vifaa vya kujikinga
vumbi kwa kuvaa barakoa lakini hawatekelezi hilo.
Mwenyekiti wa
wachekechaji ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite, Nai Leyani
amelishukuru shirika la Haki Madini kwa kuwapa elimu hiyo kwani kwa
namna moja au nyingine imewasaidia.
Leyani amesema
wamekuwa wakiwapa elimu baadhi ya wachekechaji wenzao ambao hawajapata
mafunzo hayo hasa wanawake ambao wamekuwa wanatekeleza hayo kwa kuvaa
vifaa vya kujikinga na vumbi na kumwagia maji mchanga.
No comments:
Post a Comment