Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehama Nchimbi (Mwenye miwani) na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi (kulia) wakimkabidhi zawadi ya Mbuzi Mwenyekiti wa Wazee Makazi ya Sukamahela, Mzee Yohana Andrea (kushoto) kwa ajili ya kuwasaidia kwa chakula katika Makao hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akimkabidhi Afisa Mfawidhi wa Makazi ya Wazee wasiojiweza Sukamahela, Twaha Kibalula (kushoto) chakula kwa ajili ya wazee wanaoishi katika Makazi hayo kulia ni Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Naftali Ng’ondi akifuatiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Viktorina Ludovick.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehama Nchimbi akiagana na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi baada ya kukabidhi zawadi kwa Wazee wa Makazi ya Wazee Wasiojiweza Sukamahela,Manyoni, Mkoani Singida.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi (Kulia) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wazee katika Makazi ya Wazee Wasiojiweza Sukamahela (hawapo pichani) Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehama Nchimbi na wa pili kushoto Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwigwisa.
Baadhi ya Wazee katika makazi ya Wazee wasiojiweza Sukamahela, Mkoani Singida wakifurahia jambo wakati Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi alipowatembelea na kuwapa zawadi kuelekea maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wazee Oktoba Mosi.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
……………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amesema jamii ina kila sababu ya
kuwatunza, kuwaenzi na kuwahudumia Wazee ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika Ustawi wa Jamii.DKt. Nchimbi ameyasema hayo katika Makao ya Wazee Wasiojiweza Sukamahela, Wilayani Manyoni Mkoani Singida alipokwenda kuwasalimia wazee hao ikiwa ni siku chache kabla ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe Mosi ya mwezi Oktoba.
Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka jamii kuhakikisha inawajali na kuwahudumia Wazee muda wote kwa kuzingatia mchango mkubwa walioutoa kwa nyakati tofauti wakati wakingali na uwezo wa kuzalisha mali.
“Hawa tunaowaona sasa hivi wazee, ndio waliotuzaa wakiwa vijana na wakingali katika umri wa kuzaa, Wazee ni neema na Baraka na siyo rahana” alisema
Ameongeza kuwa Serikali kwa upande wake imeweka utaratibu na Sera nzuri za kumlinda kila mtu katika hatua mbalimbali za maisha hata wakati wa uzee na ahsa kwa wazee wasio na ndugu na jamaa wa kuwatunza na kuwaangalia.
Amewataka Watanzania kuzingatia Kanuni za kupata watoto na kuwatunza vema ili baadaye wawe ni Wazee wenye busara na hekima, kwani jamii isiyowaandaa watoto wake ipasavyo, haiwezi kuwa na Wazee kama hao.
Ameongeza kuwa vizazi vya sasa wakiwemo wanafunzi wanatakiwa kuhimizwa kuwatembelea na kuwasilikiza Wazee wasiojiweza ili wapate uhalisia na uzoefu kutoka kwa wazee wenyewe.
“Tunaposema tumvushe salama tunalenga katika kuboresha afya ya mama na mtoto ili tuweze kupata kizazi salama na hatimaye kuwa na Wazee ambao tutawatunza na watafurahia uzee wao” alifafanua.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii. Dkt. John Jingu, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Naftali Ng’ondi alisema Serikali kupitia Wizara hiyo inawahudumia wazee 281 katika Makao mbalimbali nchini.
Dkt. Ng’ondi amefafanua kuwa pamoja na huduma mbalimbali kwa Wazee, Serikali imeboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kukarabati makazi ya Wazee na kujenga Ofisi ya Utawala.
Akiwa katika makazi ya Wazee Sukamahela, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Nchimbi amekabidhi zawadi ya vyakula mbalimbali zikiwemo kilo 100 za mchele, mafuta ya kula, vifaa kwa ajili ya usafi, mbuzi mmoja pamoja na sabuni ya unga.
Akitoa Shukrani kwa niaba ya Wazee wenzake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee Sukamahela, Adrea Yohana ameishukuru serikali kwa msaada wa chakula na matunzo yanayotolewa kwao.
“Tunamshukuru Rais Jonn Magufuli na nyie viongozi wetu kuja kututembelea na kutuletea msaada, Mwenyezi Mungu awabariki na kuwaongezea pale mlipotoa kiongezeke, mzidi kutupatia msaada Zaidi” Alisema Mzee Andrea.
Siku ya Wazee ya Kimataifa Mwaka 2020 inatarajiwa kufanyika katika ngazi ya mikoa na inaongozwa na Kaulimbiu isemayo“FAMILIA NA JAMII TUWAJIBIKE KUWATUNZA WAZEE”
No comments:
Post a Comment