Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu akiwa
katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Kamishna
wa Uhifadhi TANAPA, Dkt. Allan Kijazi (Kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya
TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara (kulia) pamoja na viongozi
wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo baada ya kukabidhi magari
hayo jana Agosti 28, 2020 jijini Dodoma. Naibu
Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu akiwa
katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Kamishna
wa Uhifadhi TANAPA, Dkt. Allan Kijazi (Kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya
TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara (kulia) pamoja na baadhi ya
watumishi wanaosimamia mradi huo.
**************************************
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mamlaka ya
Hifadhi za Taifa (TANAPA) imekabidhiwa magari 14 yenye thamani ya
shilingi bilioni 1.6 yanayolenga kuboresha utalii katika Hifadhi za
Taifa zilizoko katika ukanda wa kusini za Ruaha, Udzungwa na Mikumi.
Fedha hizo ambazo
ni mkopo wa masharti nafuu ni sehemu ya dola za marekani milioni 60
zilizotolewa na Benki ya Dunia ambayo kwa pamoja na Serikali ya
Tanzania, zinatekeleza mradi wa kusimamia maliasili na kuendeleza Utalii
kanda ya kusini (REGROW).
Akizungumza
wakati wa kukabidhi magari hayo jana jijini Dodoma, Naibu Waziri wa
Wizara ya Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu alisema kuwa magari
hayo ni awamu ya kwanza, ambapo magari mengine 9 yanatarajiwa kufika
hivi karibuni kwa ajili ya hifadhi mpya ya Julius Nyerere.
Naibu Waziri
Kanyasu alisema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa pili wa
maendeleo ambapo moja kati ya vipaumbele vya kimkakati vinavyokuza
uchumi wa nchi ni sekta ya utalii, hivyo lazima kuendelea kutatua
changamoto katika sekta hiyo.
“Utalii
unachangia takriban asilimia 17 ya Pato la Taifa hivyo kuletwa kwa
magari haya katika Hifadhi za Taifa zilizoko kusini zikiwemo za Ruaha,
Udzungwa, Mikumi na Julius Nyerere kutaboresha hali ya utalii katika
hifadhi hizo na kutaongeza mapato nchini”, alisema Kanyasu.
Kwa upande wake
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii na Kamishna wa Uhifadhi
TANAPA, Dkt. Allan Kijazi alisema kuwa fedha za mradi huo zitatumika
katika jitihada za kukabiliana na tatizo la ujangili ikiwa ni moja wapo
ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza utalii na kuimarisha usimamizi katika
maeneo ya kusini ili yaweze kujulikana kitaifa na kimataifa.
“Tunaishukuru
Serikali kwa kuthamini mchango wa utalii katika nchi yetu na kusaini
mkopo huo ambao utakuwa chachu ya kuimarisha utalii nchini pia
tunaishukuru Benki ya Dunia kwa kukubali kufadhili mradi huu”, alisema
Dkt. Kijazi.
Nae, Mwenyekiti
wa Bodi ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara amefafanua kuwa
mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa na Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi ya Hifadhi za
Taifa, Bodi ya Utalii, Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori, Tume ya
Umwagiliaji na Bodi ya Bonde la Maji la Rufiji.
“Mradi huu
unatekeleza shughuli zake kwa kuzingatia malengo yake makuu yakiwemo ya
kuimarisha usimamizi wa maliasili kwa kuboresha miundombinu, kuimarisha
shughuli mbadala za kiuchumi kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi
hizo za kusini pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira na ujenzi wa
miundombinu ya umwagiliaji eneo la nje la Hifadhi ya Ruaha”, alisema
Waitara.
Kupitia
utekelezaji wa sehemu ya kwanza, TANAPA inaendelea na taratibu za
manunuzi ya ujenzi wa barabara, nyumba za kulala wageni na viwanja vya
ndege ndani ya hifadhi pia imepanga kununua magari madogo na mitambo
ili kuwezesha kusimamia vizuri maeneo yaliyohifadhiwa na kuimarisha
miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi.
No comments:
Post a Comment