![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2020/08/traboss.jpg)
***********************************
Na Mwandishi wetu,
Mtwara.
Mkoa wa Mtwara
unaendelea kuimarisha miundombinu inayochangia kukua kwa uwekezaji
ikiwepo upanuzi wa Bandari ya Mkoa huo uliogharimu shilingi Bilioni 157
na ujenzi wa
njia nyingine ya kurukia ndege unaogharimu sh. Bilioni 50.
Katibu Tawala wa
Mkoa huo Bw. Alphayo Kidata alisema lengo la ujenzi wa miundombinu hiyo
ni kuhakikisha Mkoa huo unafungua njia zake za kiuchumi hususan kwenye
Kilimo cha zao la Korosho na uwepo wa gesi asilia ambayo imekuwa chachu
ya uanzishwaji wa viwanda ambavyo vimekuwa na tija ya kiuchumi.
Kidata
aliyasema hayo Mkoani Mtwara wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji
wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi alipotembelea Mkoa
huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Kanda ya Kusini yenye lengo la
kuangalia fursa na changamoto za Uwekezaji.
“Mtwara
tumejipanga kupokea Uwekezaji, tunao Wawekezaji wanaofanya vizuri na
tunazidi kukaribisha wengine wengi, tunazo fursa na miundombinu yote,
pia kwa sasa tunaendelea kuimarisha ujenzi wa miundombinu mingine ya
kisasa ya usafirishaji ikiwepo Bandari na Uwanja wetu wa ndege, kwa hiyo
msiwe na wasiwasi” alisema Bw. Alphayo Kidata
Mkurugenzi
Mtendaji wa TIC Dkt. Maduhu Kazi pamoja na kuipongeza Serikali Mkoani
humo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ambayo inasaidia
kurahisisha uwekezaji alitoa wito kuendelea kuhamasisha uwekezaji pamoja
na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Naomba tu
niwapongeze Serikali Mkoani hapa, kazi ya kuvutia uwekezaji mnayoifanya
ni njema, sisi tunawaunga mkono na pia msisite kuwaleta TIC pale
wanapoonekana kuwa na changamoto” alisema Dkt Kazi.
Nae Mkuu wa
Wilaya Mtwara Bw. Dunstan Kyobya alisema milango ya uwekezaji katika
sekta zote ipo wazi katika Wilaya yake ambayo imekuwa ikipokea wageni
wengi kuliko maeneo mengine ya mikoa ya Kanda ya Kusini.
No comments:
Post a Comment