Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro
Marine, Mhandisi Major Songoro, akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi
wa vivuko vipya viwili vya MV. Ukara na MV. Chato, Mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na Mkurugenzi wa
Kampuni ya Songoro Marine, Mhandisi Major Songoro, wakati akikagua hatua
za mwisho za ujenzi wa vivuko vipya vya MV. Ukara na MV. Chato, Mkoani
Mwanza.
Muonekano wa hatua za ujenzi wa
vivuko vipya viwili vya MV. Ukara na MV. Chato vinavyojengwa na kampuni
Songoro Marine ambavyo vipo katika hatua za mwisho za ukamilikaji.
Ujenzi wa vivuko hivyo unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 8.2.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akiwa na Katibu wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza, Bw. Salum Kali, wakielekea kukagua
ujenzi wa vivuko vipya vya MV. Ukara na MV. Chato, mkoani Mwanza. Vivuko
hivyo vinatarajia kuanza kutoa huduma mwezi Agosti, mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, akifafanua jambo kwa Katibu wa CCM mkoa wa Mwanza, Bw. Salum
Kali, walipokutana katika ziara ya kukagua ujenzi wa vivuko vipya vya
MV. Ukara na MV. Chato vinavyotarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi Agosti,
mwaka huu.
**************************************
Imeelezwa kuwa ukamilikaji wa
ujenzi wa Kivuko Kipya cha MV. Ukara kitakachotoa huduma kati ya
Bugolora (Ukerewe) hadi Ukara (Ukara) kitakuwa mwarobaini kwa wakazi wa
visiwa hivyo ambao mahitaji yao ya usafiri yamezidi kuongezeka.
Kivuko hicho ambacho kinajengwa na
Kampuni ya Songoro Marine kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 pamoja
na mzigo tani 100 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti
mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, ameyasema hayo akiwa mkoani Mwanza, wakati wa ziara yake
mkoani hapo ambapo alikagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa kivuko hicho
ambacho kinagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 4.7 na kuridhishwa na
maendeleo yake.
“Watanzania nyinyi wenyewe
mnajionea juzi tumepeleka Meli Bukoba lakini Serikali haiishi hapo tu
inaendelea na ujenzi wa kivuko hiki ambacho kitasaidia katika kutoa
huduma kwa wananchi wa visiwa vya ukara na ukerewe kwani mahitaji ya
usafiri kati ya visiwa hivyo ni makubwa zaidi”, amesema Naibu Waziri
Kwandikwa.
Aidha, amemtaka mkandarasi huyo
kuhakikisha anafunga haraka vifaa ambavyo waliviagiza ili mapema zaidi
ya mwezi wa nane kivuko hicho kiwe majini na kianze kutoa huduma.
Kwandikwa, amemuagiza Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kubuni vivuko vipya
vitakavyoweza kukidhi mahitaji ya ongezeko la watu kwa siku za usoni na
miaka ijayo ambayo itasaidia kutatua changamoto za usafiri wa visiwani.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri huyo amekagua pia ujenzi wa kivuko kingine cha MV. Chato ambacho
kinarajiwa kutoa huduma kati ya Chato hadi Nkome, mkoani Geita na
kumsisitiza mkandarasi kukamilisha haraka kazi zilizobakia katika kivuko
hicho ili nacho kianze kazi mapema mwezi Agosti mwaka huu.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa
vivuko vipya, Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi
Hassan Karonda, amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa kivuko cha MV. Ukara
umefikia asilimia 85 na MV. Chato asilimia 80 na miradi hii yote
ikikamilika wataweza kuwahudumia wananchi wengi na kwa karibu zaidi.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya
Songoro Marine, Mhandisi Major Songoro amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa
kazi ya kufunga vyuma imeshakamilika kwa vivuko vyote kwa asilimia 95,
tayari injini zimeshafungwa na kazi zilizobakia ni za kuweka milango,
madirisha, viti, mifumo ya umeme na kupaka rangi.
Kwa upande wake Katibu wa Chama
cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mwanza, Bw. Salum Kali, ameishukuru
Serikali kwa hatua ya ujenzi wa vivuko hivyo ikiwa ni moja ya
utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo imelenga kusaidia kuondoa adha ya
usafiri kwa wananchi wanaoishi katika visiwa hivyo.
No comments:
Post a Comment