Pages

Thursday, July 2, 2020

SIRI 10 ZA TANZANIA KUWA NCHI YA UCHUMI WA KATI





Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitangaza siri 10 za Tanzania kung’ara na kuingia Uchumi wa kati miaka mitano kabla ya kabla ya lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

TANZANIA YAINGIA KUNDI LA NCHI ZA KIPATO CHA KATI


…………………………………………………………………………………
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Benki ya Dunia imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 50 duniani za uchumi wa kipato cha kati, ikiwa ni ya
pili baada ya Kenya katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, baada ya ukuaji wa uchumi unaosukuma pato la mwananchi kukua (Per capita GNI) mwaka 2020. 
Tanzania imeingia kwenye uchumi wa kati  miaka mitano kabla ya lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, jambo ambalo ni la kujivunia.
Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025 katika ukurasa wa pili, kipengele 1.2 “Uchumi wa kipato cha kati umehusishwa na kuwa na nchi ambayo umaskini unapungua, uchumi imara unaojengwa na kuimarika kwa uzalishaji viwandani unaimarika na wananchi wanapata maendeleo”.
Dkt. Abbasi alisisitiza kuwa uchumi wa kipato cha kati umegawanyika katika madaraja mawili daraja la chini ambapo ni kuanzia dola za Kimarekani 1036 hadi 4045 na daraja la juu ni  dola 4046 hadi 12,535 na mwaka huu Tanzania imepanda daraja kuwa uchumi wa kipato cha kati daraja la chini, pamoja na nchi za Algeria na Benin.
Aidha, Dkt. Abbasi alifafanua siri 10 zilizoisaidia Tanzania kutajwa kufikia daraja la uchumi wa kipato cha kati na  Benki ya Dunia hapo Julai 1, 2020 kuwa ni nchi yenye amani na utulivu, na hivyo ni msingi muhimu nyuma ya mafanikio  ya nchi ya Tanzania  kuingia katika uchumi wa kipato cha kati kwani  bila amani hakuna kufanyakazi, hakuna kuzalisha na hakuna kuongeza kipato. Na hivyo viongozi, wanahabari  na wananchi kwa ujumla  wamesisitizwa  kuwekeza akili zao katika kuimarisha amani iliyopo na kukataa chokochoko zozote zile zinazoweza kuharibu misingi ya maendeleo.
Siri ya  pili ni mipango thabiti ya maendeleo, ambapo Dkt. Abbasi alisema kuwa moja ya kanuni muhimu ya kuendelea ni kuwa na mipango inayokuwekea malengo makubwa  (Olympic targets). Serikali itaendelea kuweka mipango mbalimbali ya maendeleo ya muda mrefu na mfupi, akitolea mfano mwaka 2020 Serikali ilianza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo moja ya malengo ni kufikia uchumi wa kati.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi siri ya tatu ni utekelezaji usioyumba, katika miaka 59 ya Uhuru na mitano ya Awamu ya Tano Serikali imejitahidi kusimamia eneo hilo kwa  kuhakikisha mipango inayowekwa inatekelezwa kwa kina (3feet implementation).
Siri nyingine ni maamuzi magumu, “Moja ya mafanikio ya Serikali ya Tanzania kwa Awamu zote na sasa tumeimarisha katika Awamu ya Tano ni wakati fulani Serikali kufanya uamuzi mgumu ambao wakati fulani ulionekana kuwa ni ndoto lakini baadaye ukaleta mafanikio makubwa kwa jamii, tumepambana na wala rushwa na wahujumu uchumi, tumewekeza katika miundombinu mikubwa, tumekataa pia baadhi ya nadharia za kimagharibi kwenye utendaji wetu na utungaji wetu wa sera za maendeleo” alisema Dkt. Abbasi. 
Aidha, Dkt. Abbasi alitaja siri nyingine kuwa ni azma ya kujitegemea, nidhamu katika matumizi, kutekeleza miiko ya uongozi, kuwekeza kwenye miradi inayochechemsha uchumi, maendeleo ya vitu na sekta binafsi yenye tija.

No comments:

Post a Comment