*Ni baada ya kushuhudia barabara ya Kusini kuanza kuharibika na hakuna matengenezo.
Na Said Mwishehe,Michuzi TV .
RAIS Dk.John Magufuli amesema ameshangazwa kwanini mawaziri wake, makatibu wakuu wake na watendaji wanaohusika na watendaji wake ambao wanahusika na barabara wameshindwa kuifanyia matengenezo barabara inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kusini ambayo imeanza kuharibika.
Amesema hayo wakati anazungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkuranga wakati anatokea mkoani Mtwara alikokwenda kushiriki mazishi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa ambapo amesema kuwa ameamua kutumia usafiri wa gari ili kuangalia maendeleo ya barabara hiyo.
"Sikutaka kutumia ndege, nilitaka kutumia hii barabara ili niione maendeleo yake,barabara imeanza kuharibika sana kule, nikaanza kushangaa kwanini mawaziri wangu, makatibu wakuu wangu.
"Na watendaji wanaohusika na hizo barabara hawajashughulikia hizo sehemu.Lakini dawa yao nakwenda kuitengeneza polepole, lakini nimepita hapa kuwasalimu ndugu zangu,"amesema Rais Magufuli mbele ya wananchi hao baada ya kushuhudia ubovu wa barabara hiyo ya Kusini katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kuwaambia wananchi hao anawapenda na anawapongeza kwa maendeleo wanayoyafanya wilayani Mkuranga pamoja na changamoto nyingi ambazo wanazipitia na yeye anazifahamu.
Wakati anasimama kwa wananchi hao Rais Magufuli alianza kwa kuwaeleza kwamba " Wana Mkuranga, kweli nimesimama hapa kuwasilimu, lakini napenda kuwapa pole sana kwa kuondokewa na Rais wa Awamu ya Tatu , mzee wetu Benjamin Mkapa.
"Msiba huu ni wetu wote, tumetoka kumpumzisha mahala pale pake na ndio maana nilikuwa nije na ndege nikasema hapana , nikaona ngoja niende na hili barabara ili kujua hata maendeleo yake,"amesema Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment