Pages

Saturday, May 30, 2020

SIMBACHAWENE: SERIKALI IPO KATIKA MCHAKATO KUHAKIKISHA MAHABUSU NCHINI WANAFANYA KAZI MAGEREZANI KAMA WAFUNGWA



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na Maafisa na Askari wa Gereza la Mahabusu Segerea, wakati alipofanya ziara katika Gereza hilo, jijini Dar es Salaam, leo. Waziri huyo pia alifanya ziara katika Gereza Kuu la Ukonga na Keko na kulitaka Jeshi la Magereza kujitegemea, na Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha mahabusu nao wanafanya kazi kama ilivyokuwa kwa wafungwa. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (katikati), akitoka Gereza Kuu Ukonga, baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam, leo. Akizungumza na Maafisa na Askari wa Gereza la Segerea, Ukonga na Keko, Simbachawene alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha mahabusu nao wanafanya kazi kama ilivyokuwa kwa wafungwa ili kuwezesha Jeshi la Magereza kujitegemea kwa chakula. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es salaam, ACP. Solomon Urio, na kulia ni Mkuu wa Gereza Ukonga, ACP. Nsajigwa Mwankenja.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akimsikiliza Afisa Rasilimali Watu wa Gereza Kuu la Mahabusu Segerea, ASP. Hellen Jairo alipokuwa anauliza swali wakati Waziri huyo alipokuwa anazungumza na Maafisa na Askari wa Gereza hilo, jijini Dar es salaam, leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akimshika ng’ombe wa maziwa anayefugwa na Gereza Segerea jijini Dar es Salaam, leo, ikiwa ni hatua ya kujitegemea kwa chakula kwa Gereza hilo. Alifanya ziara gerezani hapo na kuwataka viongozi kuhakikisha wanajitegemea, na pia kulima matunda na mboga za majani kwa Magereza yote ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la Magereza, wakati alipokuwa anawasili katika Gereza Kuu la Mahabusu Segerea, jijini Dar es Salaam, leo, kwa ziara ya siku moja kusisitiza Magereza ya Mkoa huo kujitegemea kwa chakula.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (wapili kulia), akiangalia miche ya mikorosho inayozalishwa na Gereza Kuu la Mahabusu Segerea, Mkoani Dar es Salaam, wakati alipofanya ziara katika gereza hilo, leo, kusisitiza Magereza ya Mkoa huo kujitegemea kwa chakula. Kulia ni Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), George Wambura.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (aliyevaa Kaunda suti kulia), akipokea salamu kutoka kwa Maafisa wa Jeshi la Magereza, wakati alipokuwa anawasili
katika Gereza la Mahabusu Keko, jijini Dar es Salaam, leo, kwa ziara ya siku moja akisisitiza Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam kujitegemea kwa chakula. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio.  Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………………………………………………….
Na Felix Mwagara, MOHA, Dar.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha Mahabusu waliopo katika Magereza mbalimbali nchini wanaanza kufanya kazi kama ilivyokuwa kwa wafungwa. 
Amesema mchakato huo ambao tayari umeanza, utakapo kamilika utaleta mapendekezo madhubuti ya jinsi gani ya kuwatumia mahabusu hao pamoja na wafungwa katika kufanya kazi za uzalishaji mali na kuhakikisha Jeshi hilo linajitegemea kikamilifu. 
Akizungumza na Maafisa na Askari Magereza katika Magereza ya Segerea, Ukonga na Keko jijini Dar es Salaam, leo, kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya siku moja ya kusisitiza magereza yanajitegemea nchini, alisema ili binadamu ale lazima afanye kazi, na pia vitabu vitakatifu vinasisitiza hilo, hivyo mahabusu wanapaswa kufanya kazi kwa kuwa nao wanakula vyakula magerezani. 
“Kuna mjadala mkubwa tunaendelea kuchakata kuhusu mahabusu waweze kufanya kazi, lakini lengo letu sio kuwafanyisha kazi za sulubu, au kazi zinazotweza utu wao, hapana, wao pamoja na wafungwa wana adhabu wanayoitumikia, tunataka kuwatumia katika kuzalisha, kwahiyo watafanya kazi kama watu wengine wanavyofanya kazi, hili naomba lieleweke,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Mjadala unaendelea na tutakuja na majibu jinsi ya kuwatumia mahabusu na wafungwa, lakini tutakuja na majibu yenye mapendekezo tutashirikiana, lakini tunataka kuwatumia kwa nia njema ya kuzalisha, kama mnavyojua binadamu asipofanya kazi asile na imeandikwa katika vitabu vitakatifu, kama mtu umemfungia ndani alafu hafanyi kazi na anadai chakula na ajue kwamba asipofanya kazi hana haki ya kula, wewe umekuja ni mahabusu ili upeleke tonge hapa lazima uzalishe, huwezi kusema sifanyi kazi kwasababu ni mahabusu, hapana tutakulinda hata kwa bunduki utafanya kazi.”
Alisema lazima kuwepo na mtazamo mpana, mkubwa katika masuala ya kuzalisha na kujitegemea kwa Jeshi la Magereza, kwa ajili ya kuzalisha pamoja na kutatua matatizo mengine ndani ya Jeshi hilo ikiwemo kujenga nyumba, kulipa umeme pamoja na mahaitaji mbalimbali ya Jeshi hilo.
“Kama nilivyosema mjadala bado ni mkubwa kwa wafungwa na tunafahamu wapo chini ya Magereza, lakini hao wengine tumepewa tuwatunze wapo chini ya vyombo vingine, hivyo tunaendelea na mchakato wa kujadiliana kuhusu hilo, na ukikamilika tutawaletea majibu,” alisema Simbachawene. 
Aliongeza kuwa, dhana ya Jeshi hilo kuzalisha na kujitegemea ni agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt. John Magufuli kulitaka jeshi hilo kuzalisha kwa wingi ili kujitosheleza na kujitegemea. 
Aidha, alilitaka Jeshi hilo kuhakikisha Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam yaanze kufanya kilimo cha mboga za majani na matunda pamoja na ubunifu wa uzalishaji mwingine katika mkoa huo, na magereza yaliyopo mikoani yaendelee na kilimo cha mpunga, mahindi, ufugaji pamoja na uzalishaji wa aina nyingine wanaoendelea nao katika maeneo yao. 
Alisema kupitia uzalishaji mali huo utawezesha kupata fedha baada ya kuuza na kusaidia majukumu mengine ya Jeshi kuliko kutegemea fedha za matumizi mengine (OC) ambazo utolewa na Serikali kwa Jeshi hilo. 
Pia Waziri Simbachawene amelitaka Jeshi hilo kuhakikisha wanahakiki mali zote za Jeshi ikiwemo mashamba yajulikane, na pia ijulikane yana hati au hayana, na mifugo ya Jeshi hilo ipo wapi na idadi yake ikiwa ni lengo la kutambua mali hizo na kuwekwa wazi kwasababu ni mali za umma.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio, alimshukuru Waziri huyo kwa kufanya ziara katika Mkoa huo na kuwaomba viongozi mbalimbali nchini waweze kutembelea magereza ili waweze kujifunza na kujua kazi mbalimbali zinazofanywa na Jeshi mkoani humo.
“Tunakushukuru kwa kututembelea Mheshimiwa Waziri, na maelekezo uliyotaoa tutayafanyia kazi, na pia tunawaomba viongozi mbalimbali waweze kutembelea Magereza na kujua kazi mbalimbali tunazozifanya,” alisema ACP Urio. 
Simbachawene amemaliza ziara yake ya siku moja kwa kutembelea magereza hayo, ambayo ni Gereza Kuu la Mahabusu Segerea, Gereza Kuu la Ukonga na Gereza la Mahabusu la Keko, ambapo katika ziara yake alipokua taarifa ya utendaji kazi kutoka kwa Wakuu wa Magereza hayo pamoja na kuahidi changamoto zao kufanyiwa.   

No comments:

Post a Comment