Pages

Sunday, May 31, 2020

Serikali yatangaza neema kupitia matumizi gesi asilia,TPDC yaazimia kuifikia mikoa mingi

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (kulia katikati) pamoja na baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara ya Nishati na taasisi zake wakionyeshwa ramani ya mtandao wa usambazaji wa miundombinu ya gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani kutoka katika visima vya kuchimba gesi,baada ya kuzindua ujenzi wa miundombinu hiyo katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi. (Na Mpiga Picha Wetu). Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC) itasambaza na kuunganisha bila malipo miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani kwa wateja wa awali katika mikoa yote itayofikiwa na huduma hiyo nchini.
Hayo ameyabainisha wakati akizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika Kijiji cha Mnazi Mmoja mkoani Lindi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, Dkt.James Mataragio( aliyenyosha mikono) akicheza na wakazi wa eneo la Mnazi Mmoja, mkoani Lindi kufurahia uzinduzi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji  gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika eneo hilo. (Na Mpiga Picha Wetu). Pia Waziri amewataka wakazi wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo ili kujiletea maendeleo na kuondokana na uchafuzi wa mazingira,  gharama kubwa za kununua mkaa na kuni pamoja na adha kutafuta kuni porini kwa ajili ya kupikia, kwani matumizi ya gesi ni salama na nafuu.
Amesema kuwa, baada ya wateja hao kuunganishiwa miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika nyumba zao zikiwemo taasisi mbalimbali, mteja atawekewa mita ya kupimia kiasi cha gesi anayotumia itakayofanya kazi kama LUKU za umeme nchini.
Alisema baada ya kufungiwa miundombinu hiyo ya kusambaza gesi asilia, mteja atatakiwa kununua uniti za gesi kulingana na mahitaji yake kama ilivyo katika umeme, na kuzitumia endapo zitaisha kabla ya kuongeza nyingine, mita itafunga hadi pale atakaponunua uniti zingine kuongezea, mfumo huo unaitwa malipo kabla ya kutumia( Pre- Paid System).
Waziri amesema, kwa familia ya watu sita inakadiriwa kutumia kiasi cha gesi ya shilingi 30,000 tu, kwa mwezi kwa matumizi yote ya kupikia bila kubagua aina ya vyakula vinavyotumia muda mrefu jikoni.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati) akipata maelezo ya namna mita ya kupima gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani, inayofanya kazi kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC). (Na Mpiga Picha Wetu).
“Watanzania wenzangu mnataka serikali iwape nini tena jamani,imegundua gesi asilia nchini kwetu inayotuzalishia umeme, sasa tunasambaziwa gesi hii majumbani ili tuitumie kupikia vyakula vyetu na hatulipii chochote wakati wa kuunganishwa kwa hawa wateja wa awali, zaidi tutalipia kile tunachotumia na ni gharama ndogo mno ukilinganisha na matumizi ya kuni na mkaa, hebu jitokezeni kwa wingi mfungiwe gesi katika majumba yenu,”amesema Waziri huyo.
Waziri Dkt.Kalemani amesema, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli imeamua kufanya hivyo ili kuhamasisha matumizi ya gesi asilia iliyopatikana kwa wingi hapa nchini.
Sambamba na kupunguza ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa ili kusaidia juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira yetu, hatua ambayo itawezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia amesema,mradi wa usambazaji wa gesi asilia ni endelevu, ambapo kwa mwaka  wa fedha 2020/2021 wateja wapya 2,000 wataunganishia gesi majumbani, 300 kati yao wanatoka Mkoa wa Lindi na vitongoji vyake.
Alitaja mikoa inayofuata sasa katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kuwa ni pamoja na Morogoro, Dodoma na Singida.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC , Dkt. James Mtaragio amewatoa hofu watumiaji wa gesi asilia majumbani kwa kuwaeleza kuwa, usanifu na ujenzi wa miundombinu hiyo imezingatia hatua zote za usalama.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, Dkt.James Mataragio akizungumza na wakazi wa eneo la Mnazi Mmoja (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji  gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika eneo hilo. (Na Mpiga Picha Wetu). Amesema, lengo la kufanya hivyo ni ili kuhakikisha matumizi ya gesi hiyo yanakuwa salama zaidi kwa mtumiaji na jamii kwa ujumla.
Dkt.Mataragio pia amewaomba wananchi kuondoa hofu katika matumizi ya gesi asilia kwa shughuli za kupikia.
“Usalama wa gesi hii asilia unasababishwa na tabia yake, kwani ni nyepesi kuliko hewa tunayovut,a hivyo kama ikitokea imevuja basi hupotelea hewani mapema na haiwezi kulipuka wala kusababisha moto, vilevile usambazaji wa gesi hii ni salama zaidi kwa kuwa husambazwa katika mgandamizo mdogo kwa njia ya bomba tofauti na gesi nyinyine, ni imani yangu kuwa wananchi wengi mtatumia gesi hii kwakuwa ni salama zaidi na nigharama nafuu mno,”amesema Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC.
Dkt.Matargio akizungumzia gharama za matumizi ya gesi hiyo ikilinganishwa na mkaa pamoja na kuni amesema kuwa, kwa ulinganishi matumizi ya mkaa si chini ya shilingi 4,500 kwa,wakati matumizi hayo hayo kwa kutumia gesi ni shilingi 1000 tu kwa kupikia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema kuwa, Mkoa wa Lindi umeandika historia nyingine iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia itakayokuwa ikitumika kwa kupikia majumbani, mahotelini kwenye taasisi za afya, elimu na matumizi mengineyo kama viwandani na kuendeshea magari.
RC Zambi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TPDC kwa kutenga fedha zitakazowezesha utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Lindi na baadae kote nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi akizungumza na wakazi wa eneo la Mnazi Mmoja (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji  gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika eneo hilo. (Na Mpiga Picha Wetu). Pia Mkuu huyo amewashukuru wananchi mkoani hapa kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote cha kutekeleza mradi huo na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kizalendo kwani mradi huo ni kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment