Pages

Sunday, May 31, 2020

Bwawa la JNHPP litakavyogeuza historia ya nishati mijini na vijijini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua mradi wa bwawa la kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya bonde la Mto Rufiji wa Julius Nyerere (JNHPP) hivi karibuni.(Picha na OWM). Na Penina Malundo, TimesMajira Online
MRADI wa bwawa la kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Bonde la Mto Rufiji wa Julius Nyerere (JNHPP) ni miongoni mwa miradi mikubwa nchini unaotekelezwa na Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
Aidha, mradi huu ni miongoni mwa miradi itakayoleta tija kubwa kwa watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.
Kupitia mradi huu utaweza kuwasaidia watanzania kuachana na matumizi ya mkaa na ukataji wa kuni na badala yake kutumia umeme ambao utakuwa wa uhakika.
Kukamilika kwa mradi huo wa kihistoria, Taifa litakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya Megawati 2115, kiasi ambacho ni kikubwa cha umeme ambacho kinatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya nishati mijini, vijijini na nchi jirani.
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli imeamua kwa dhati kutekeleza mradi huu ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere takribani miaka 40 iliyopita.Mradi unaotekelezwa kwa kasi yake ili uweze kukamilika kwa wakati na hata kabla ya muda.
Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea eneo hilo kuona maendeleo ya mradi huo unavyoendelea akiambatana na viongozi mbalimbali.
Majaliwa anasema, mradi huo ni mradi wa kimkakati ambao unapelekea taifa kuhakikisha unakuwa na umeme wa kutosha.
Anasema, mradi huo utakapokamilika utafanya vijiji na vitongoji kufikiwa na umeme utakaozalishwa na bwawa hilo na kupata umeme utakaokuwa wa uhakika.
“Nia ya Serikali ni kuhakikisha mradi huu wa kufua umeme unakamilika kwa wakati ili watanzania waweze kupata matunda ya nchi yao na ndio matumaini ya watanzania wengi.Malengo ya Serikali ni kuwafanya watanzania kuachana na matumizi ya kuni na kuhifadhi misitu na kutumia umeme katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali,”anasema Waziri Majaliwa.
Anasema, kukamilika kwa mradi huo utafanya gharama ya umeme kushuka na kuwa nafuu kwa kila mtanzania ili kuwapa fursa watu kuutumia.
“Hadi sasa kazi inayofanywa na wakandarasi ni nzuri na ya uhakika,inaenda kwa wakati,wakandarasi wamemundu kufanya kazi hiyo na kuifikisha katika hatua nzuri hadi sasa.
“Kazi inayoendelea ni nzuri na mimi nimeridhika kwa kazi hii ,tumeshuhudia na kuona ni namna gani tuta linavyoandaliwa kwa ajili ya kuzuia maji ili yaweze kuondoka kwa utaratibu,pia tumeona njia za chini zinazopitisha maji kwa muda ili kuwezesha maji hayo kufika katika maeneo yanayotakiwa kuendesha mashine zitakazozalisha umeme,”anasema.
Aidha, anaongeza kuwa tayari mitambo ya kuzalisha umeme imeagizwa na kufanya kila idara kuhakikisha inafanya kazi yake vizuri.
Anasema, Watanzania wawe na matumaini na serikali katika mkakati wake wa kuhakikisha wanafikisha umeme katika vijiji na ni mkakati endelevu ambao utaweza kuwauzia hata nchi jirani.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati,Dkt.Medard Kalemani amewahakikishia watanzania kuwa wizara yake itasimamia mradi huo wa kihistoria kwa weledi ili uweze kukamilika kwa wakati.
“Sisi kama wasimamizi tunajipanga vizuri kusimamia mradi huu ili ukamilike mapema kabla ya mwezi mmoja kabla ya muda wake kwa kuwa tumemlipa vizuri mkandarasi na hana tatizo lolote tunasubiri kazi imalizike hata kabla ya muda.
“Watanzania wameendelea kuajiriwa hapa na matarajio yetu wote walioajiriwa hapa watatoka na ujuzi ili kusudi manufaa ya watanzania yapatikane,”anasema.
Anasema, mradi huo unatarajia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati nchini ,bwawa hilo litakapokamilika litakuwa ni bwawa la 70 kwa ukubwa duniani na bwawa la nne kwa ukubwa Afrika na Bwawa la kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki.
Anasema, mradi huo utakapokamilika Juni,2022 Tutakuwa na ziada ya megwati 3920 ukijumlisha na miradi mingine, hivyo tutajitosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote 12,268 na utafika katika maeneo yote.
“Naomba nihamasishe watanzania wawe watu wa kwanza kuja kufanya utalii bwawa hili litakapokamilika, kwani bwawa hili litakuwa la kimataifa,”anasema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),Dkt.Tito Mwinuka anasema, hadi sasa kazi zinaemdelea vizuri na wapo ndani ya muda na kuwa na uwezekano wa kumaliza kwa muda waliopangiwa.
Anasema, Serikali imetimiza wajibu wake wa kumlipa mkandarasi kwa kila hatua anayopaswa kulipwa hadi sasa mkandarasi tayari amelipwa kwa ‘certificate’ saba hakuna ‘certificate’ hata moja iliyowasilishwa serikalini akacheleweshwa kulipwa.
“Nashukuru sana Serikali,sisi Tanesco tukiwa wasimamizi wa mradi huu kupitia Tanroads Engineering Consulting Union (TECU) tutaendelea sisi kutekeleza wajibu wetu kusimamia na kutatua changamoto zozote mkandarasi atakazokuta nazo kushirikiana na taasisi nyingine za serikali ambazo zina mchango katika utekelezaji wa mradi huu,”anasema.
Anasema, miongoni mwa hatua mbalimbali zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na uchimbaji eneo la jengo la mitambo ya kufua umeme (power house),uchimbaji na uimarishaji wa mwamba eneo la jengo la mitambo ya kufua umeme na uchimbaji na uimarishaji wa mwamba wa kuta za bwawa kuu na uchimbaji wa njia ya maji yanayoelekea kwenye jengo la kufua umeme.

No comments:

Post a Comment