Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole
Sanare (kushoto) akipokea msaada wa shilingi milioni moja kutoka kwa
mwakilishi wa Viongozi wa Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania
Mkoani Morogoro Askofu Brayson Msuya ambaye pia ni Mwenyekiti wa CPCT
Morogoro (picha – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa)
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo (wa kwanza kulia)
akiwa amekabidhiwa fedha na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro zilizotolewa
msaada na viongozi wa CPCT kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa CORONA.
wa pili kulia ni Katibu wa CPCT Lameck Ngenzi ambaye pia ni Askofu wa
Kanisa la Free Pentekoste
*******************************
Na Farida Saidy,Morogoro
Baraza la Makanisa ya
Pentekoste Tanzania (CPCT) Mkoa wa Morogoro wameungana na jitihada za
Serikali ya Mkoa huo kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni moja za
kitanzania ikiwa ni mchango wao katika kupambana na ugonjwa wa CORONA
Mkoani humo.
Viongozi wa CPCT
wametoa msaada huo wa fedha mwishoni mwa wiki hii walipofika ofisini kwa
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kumkabidhi fedha hizo Mkuu wa Mkoa huo
Loata Ole Sanare kama ishara ya kumuunga Mkono na Serikali ngazi ya Mkoa
katika kupambana na ugonjwa wa CORONA Mkoani humo.
Wakizungumzia mara
baada ya kutoa msaada huo, Viongozi wa CPCT wakiongozwa na Askofu Bryson
Msuya Askofu wa TAG Morogoro Kaskazini ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa
CPCT Mkoa wa Morogoro walieleza kuwa wameguswa na jitihada za Mkuu wa
Mkoa za kupambana na ugonjwa wa CORONA.
Hamasa ya viongozi
hao inatokana na wito alioutoa Mkuu wa Mkoa huo Loata Sanare Aprili 21
mwaka huu katika kikao chake na wadau mbalimbali wa maendeleo Mkoani
humo kilichofanyika katika Chuo cha ualimu cha Morogoro ambapo kwa
pamoja walikubaliana kuunganisha nguvu zao ili kupambana na janga la
CORONA ambalo bado ni tishio kwa Taifa la Tanzania na Dunia kwa jumla.
Akipokea mchango huo
Loata Ole Sanare aliwashukuru viongozi hao kwa mchango walioutoa huku
akisisitiza kauli yake anayoitoa mara kwa mara kuwa pamoja na michango
ambayo ni muhimu, kubwa aliwataka viongozi hao kutoa elimu kwa watu
wanaowahudumia katika maeneo yao namna ya kujikinga na maambukizi ya
CORONA.
Aprili 24 mwaka huu
yaani siku tatu baada ya kikao cha Mkuu wa Mkoa na wadau kufanyika,
michango mbalimbali ilianza kumiminika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kutoka
kwa wadau ikiwa ni utekelezaji wa ahadi walizotoa siku ya kikao ambapo
siku hiyo pekee vifaa na fedha taslimu vilipatikana, vyote vikiwa na
jumla ya zaidi ya shilingi 141Mil.
No comments:
Post a Comment