Mwenyekiti wa Bodi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo akizungumza na Waandishi wa Habari katika Mkutano wa Bodi uliofanyika Jijini Dar es Salaam Aprili, 29, 2020.
Wajumbe wa Bodi wakifuatilia Mkutano wa Waandishi wa Habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas uliofanyika Jijini Dar es Salaam Aprili, 29, 2020.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii (TTB), Bi. Devotha Mdachi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa Waandishi wa Habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu
Thomas uliofanyika Jijini Dar es Salaam Aprili, 29, 2020, ukihusisha Bodi ya Taasisi hiyo.
Thomas uliofanyika Jijini Dar es Salaam Aprili, 29, 2020, ukihusisha Bodi ya Taasisi hiyo.
Picha na Idara ya Habari-MAELEZO.
*****************************
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
29.4.2020
BODI ya Utalii
Tanzania (TTB) imeainisha mikakati 10 ya muda mrefu inayolenga kuinua
soko la utalii nchini ambalo kwa sasa limeathirika na mlipuko wa ugonjwa
wa homa kali ya
mapafu (CORONA) unaosababishwa na kirusi cha (COVID-19)
na kuenea katika nchi mbalimbali duniani.
Hayo yamesemwa
leo Jumatano (Aprili 29, 2020) Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa
Bodi ya (TTB) Jaji Mstaafu Thomas Mihayo wakati wa mkutano na Waandishi
wa vyombo vya habari kuelezea athari za mlipuko ugonjwa wa CORONA na
tathimini ya sekta ya Utalii nchini.
Alisema kuwa kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO),
inaonesha kuwa mlipuko wa ugonjwa wa CORONA utasababisha kushuka kwa
kiwango cha kati ya asilimia 20-30 ya idadi ya watalii kwa mwaka 2020
pamoja na kusababisha ukosefu wa mapato kiasi cha Dola za Marekani
300-450 Bilioni duniani.
Akifafanua zaidi
Jaji Mihayo alisema pia utabiri wa awali uliofanywa na Shirika lisilo la
kiserikali linaloshauri nchi na taasisi za kimataifa la DEFC unaonesha
kuwa mwenendo wa uchumi duniani umebadilika na utaendelea kubadilika
ambapo sekta za utalii na usafiri wa anga ziilizokuwa zimeshamiri, kwa
sasa zitakuwa za mwisho kwenye uchangiaji wa ukuaji wa uchumi duniani.
‘’Sekta ya Utalii
nchini Tanzania inachangia takribani asilimia 17-17.5 ya mapato ya
Serikali (GDP) ambapo kwa mwaka 2018 Tanzania ilitembelewa na watalii
wapatao 1,505,702 kutoka watalii 1,327,143 wa mwaka 2017, hivyo janga
la virusi vya CORONA limeleta athari kwenye soko la utalii duniani na
hapa nchini pia kwenye sekta zinazowezesha sekta ya utalii’’ alisema
Jaji Mihayo.
Aidha Jaji Mihayo
aliitaja mikakati endelevu iliyowekwa na TTB katika kuendeleza na
kukuza sekta ya utalii nchini ni pamoja na kushirikiana na wadau wa
utalii kuandaa mkakati wa pamoja wa kukabiliana na janga la COVID-19
kwenye sekta ya utalii, kuandaa mkakati mpya wa mauzo wa kimataifa
kupitia ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na
kushirikisha watu mashuhuri na mabalozi wa utalii Tanzania kwa ajili ya
kutangaza utalii.
Aliitaja mikakati
mingine ni pamoja na kuimarisha timu ya mauzo kubuni mbinu za kisasa na
kitaalamu zenye ubunifu wa kuandaa mikakati ya mauzo ya mtandao,
kutangaza utalii wa ndani kupitia programu maalum za mashule na vyuo vya
elimu pamoja na kushirikiana na Balozi za Tanzania nje ya nchi kuweka
mikakati bayana ya kuwapata mabalozi wa TTB.
Kwa mujibu wa
Jaji Mihajo alisema mara baada ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa
CORONA, TTB ilianza kuchukua tahadhari mbalimbali ikiwemo kuandaa na
kurusha makala fupi ya dakika 1.5 iliyosambaa duniani kuhamasisha
watalii kujikinga na COVID-19 na kuwakumbusha wasifute safari zao za
utalii nchini Tanzania.
‘’Makala hiyo
fupi imezunguka kwenye masoko yetu yote makubwa duniani na imevuka
matarajio ya awali ya kiwango cha watu waliyoiona na pia makala hiyo
imeoneshwa kwenye vituo vyetu vya Televisheni na kuwekewa lugha za
kiarabu, kifaransa, kijerumani na kidachi’’ alisema Jaji Mihayo.
Jaji Mihayo
alisema TTB, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya
Uhifadhi Ngorongoro (NCAA) wameingia ubia na kampuni ya Great Migration
Camp kwa pamoja wamebuni kipindi maalum kinachoitwa ‘’Serengeti Live
Show’’, kinachorushwa mubashara na vingine kurekodiwa na kurushwa kwa
awamu kwenye mitandao ya TTB na washirika wake nchini na nje ya nchi
kuonesha utalii wa Tanzania.
Aliongeza kuwa
madhumuni ya vipindi hivyo ni kukonga mioyo ya watalii ambao
wameahirisha safari zao za kuja Tanzania kwa kipindi hiki cha mlipuko wa
ugonjwa wa CORONA, ambapo kupitia vipindi hivyo Tanzania itahakikisha
kuwa Jina maalum la kutangaza utalii wa Tanzania la Tanzania Unforgettable linaendelea kutumia ili kuhamasisha sekta ya utalii nchini.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Devotha Mdhachi alisema mwezi Mei mwaka huu
Ofisi yake inatarajia kufanya kikao na wadau wa sekta ya utalii nchini
ili kujadili mikakati ya pamoja inayolenga kuimarisha soko la utalii
nchini katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiriwa na mlipuko wa
ugonjwa wa CORONA.
No comments:
Post a Comment