Ofisa madini mkazi wa Mirerani,
Daudi Ntalima akizungumza na waandishi wa habari juu ya maagizo
mbalimbali ya Serikali ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya
Tanzanite.
…………………………………………………………………………………………………
WAKURUGENZI wa kampuni ya
TanzaniteOne na viongozi waandamizi wa kampuni hiyo
wamepigwa marufuku
kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji
mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kufanya shughuli
yoyote wala kusogelea eneo hilo kwa mita 200.
Kampuni ya TanzaniteOne ilikuwa
inamiliki kitalu C kwa ubia na serikali kupitia shirika la madini
(Stamico) wa kila mmoja asilimia 50 ila leseni yao ilifutwa hivi
karibuni na Tume ya madini na kutangazwa bungeni na Waziri wa Madini,
Dotto Biteko.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani,
Daudi Ntalima akizungumza jana ofisini kwake alisema hatua kali za
kisheria dhidi ya viongozi hao wa TanzaniteOne zitachukuliwa pindi
wakikiuka agizo hilo.
Ntalima aliwataja wakurugenzi wa
kampuni ya TanzaniteOne ambao hawatakiwi kuingia ndani ya ukuta
unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ni Faisal Shabahi na Hussein
Gonga.
Aliwataja wafanyakazi wengine wa
kampuni hiyo ni mkuu idara ya ulinzi Abubakari Lombe, msimamizi Thomas
Mollel, msaidizi idara ya ulinzi Elisamehe Msuya na msimamizi Baraka
Mkongo.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa
madini ya Tanzanite wa kitalu B (Opec) na D ambao wanapakana na kampuni
ya TanzaniteOne wamefurahia hatua hiyo kwani migodi yao iliyositisha
eneo la mitobozano itaendelea na kazi.
Mmoja kati ya wamiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite, Samuel Rugemalira alisema manyanyaso yote yana mwisho ambao huwa mbaya.
“Hongereni sana Rais John
Magufuli, Waziri wa Madini Dotto Biteko na Ofisa madini mkazi Mirerani
Daudi Ntalima na Tume ya madini kwa ujumla kutokana na uamuzi huo na
wakifika hata soko la mbuzi wanakamatwa,” alisema.
Meneja wa kampuni ya Building
Utilities, Charles Chilala alisema wakati wa Mungu umefika kwani
amewaletea wachimbaji madini ya Tanzanite, Rais John Magufuli ili
awatetee na ndivyo alivyofanya.
Hata hivyo, mkurugenzi wa
Tanzanite One, Faisal Shabhai alisema hawana taarifa rasmi za kufukuzwa
kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani.
“Tunafuatilia lakini kama ni maagizo ya serikali tutatekeleza bila tatizo lolote lile,” alisema Shabhai.
No comments:
Post a Comment