******************************
Na Mwandishi Wetu
Tanzania imetajwa
kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki na ya nne Afrika kwa kuweka
mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara ndogondogo.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma, Msemaji mkuu wa Serikali na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Hassan
Abbasi amesema kuwa kidunia Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika
Nyanja mbalimbali ambapo katika suala hilo anasema kidunia imekuwa ya
21.
“Taasisi za
Kimataifa zinatambua juhudi za Serikali yetu katika kuwaletea wananchi
maendeleo, Baadhi ya masuala yaliyofanyika kwa wajasiriamali wadogo ni
kupewa vitambulisho maalum vya kuwatambulisha, tozo mbalimbali
zimefutwa ili kuwesesha ukuaji wa sekta ya biashara hapa
nchini”,Alisistiza Dkt. Abbasi
Akifafanua Dkt.
Abbasi amesema kuwa Kituo cha Kimataifa cha Televisheni cha CNBC Africa
kimerusha makala maalum inayoonesha mafanikio ya Serikali katika
kuwaletea wananchi maendeleo na kuoneshwa na zaidi ya nchi 100 Duniani.
Katika makala
hiyo iliyoakisi sekta za utalii, miundombinu, nishati, madini, kilimo na
uzalishaji, Dkt. Abbasi amesema kuwa hatua hiyo ni moja ya ishara kuwa
Taasisi za Kimataifa zinaendelea kutambua hatua zinazochukiliwa na
Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Katika hatua
nyingine Dkt. Abbasi amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika ya Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi aliwasilisha ripoti ya
Tanzania katika Baraza la Dunia la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu
na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu na kulinda haki za
binadamu kama ilivyokawaida yake.
“ Haki za
Binadamu sio siasa, kama nchi tumeendelea kusisitiza na tutaendelea
kuzienzi haki zote za Binadamu kwa maslahi ya watu wote” , alisisitiza
Dkt. Abbasi
Tanzania imetajwa
kwa nyakati tofauti na Taasisi mbalimbali za Kimataifa kuwa Taifa la
kupigiwa mfano kwa namna inavyochukua hatua za kuwaletea wananchi
maendeleo, kupiga vita rushwa, kujenga uchumi na ustawi wa wananchi
No comments:
Post a Comment