Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Madaktari na Wauguzi wa Kituo cha Afya cha Maramba
wilayani Mkinga baada ya kutembelea kituo hicho, Machi 2, 2020. Kushoto
ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Veronica Msaki ambae amejifungu mtoto wa kike Doreene
(pichani) katika Kituo cha Afya cha Maramba wilayani Mkinga. Mheshimiwa
Majaliwa alitembela wodi ya wazazi katika kituo hicho, Machi 2, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisikiliza kwaya ya Jeshi la Kujenga Taifa, Kambi ya Maramba wilyani
Mkinga wakati alipowasili kwenye uwanja wa CCM Maramba kuhutubia mkutano
wa hadhara , Machi 2, 2020. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,
Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa
wa Kambi ya Maramba wakiimba katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika uwanja wa CCM Maramba, Machi 2,
2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano iko imara na...
inamipango madhubuti ya kuwahudumia na kuwatumikia Watanzania katika
maeneo yote nchini.
Ili kutimiza
adhima hiyo, Waziri Mkuu amepiga marufuku kitendo cha watumishi wa umma
kumaliza wiki wakiwa maofisini na badala yake amewataka watumie siku nne
kwenda kwa wananchi katika maeneo yao.
Waziri Mkuu
aliyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akizungumza
na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM
Maramba wilayani ya Mkinga, Tanga.
“Ni lazima
wananchi wahudumiwe wakati wote. Watumishi wa umma ni marufuku kumaliza
wiki nzima mkiwa ofisi mnatakiwa kutumia siku mbili ofisini na siku nne
zilizobaki nendeni mkasikilize kero za wananchi katika maeneo yao na
kuzipatia ufumbuzi,”
Pia, Waziri Mkuu
amewataka watumishi wa umma wahakikishe fedha zote zinazotolewa na
Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatumika kama
ilivyokusudiwa. “Fedha hizi tunazoleta ni za moto zisidokolewe
zitawaunguza.”
Kufuatia
changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya
ya Mkinga, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo
watenge fedha za mapato ya ndani na kuanzisha miradi ya uchimbaji wa
visima wakati Serikali ikiendelea kulishughulikia suala hilo.
Kadhalika, Waziri
Mkuu alimuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Mkinga ahakikishe wananchi
wanaokwenda kufuata huduma za matibabu katika vituo vya afya na zahanati
wanapatiwa dawa badala ya kuelekezwa kwenda kununua kwenye maduka.
Alisema Serikali
imeongeza bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 37 hadi sh bilioni 269,
hivyo hakuna sababu ya mwananchi kwenda kwenda eneo la kutolea huduma ya
afya na kukosa dawa. “Lazima mhakikishe dawa zote zinazotakiwa
zinakuwepo kwenye zahanati na hivyo hivyo kwenye vituo vya afya na
hospitali.”
Kuhusu ombi la
mbunge wa Mkinga Danstan Kitandula la kutaka wananchi wapewe mashamba
yasiyoendelezwa ili waweze kuyatumia katika shughuli za kilimo, Waziri
Mkuu alisema atalifanyia kazi suala hilo.
Pia, Waziri Mkuu
aliwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao na kwamba changamoto
mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za upatikanaji wa huduma za maji,
umeme na miundombinu ya barabara zitafanyiwa kazi.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza
tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali
nchini ikiwemo na wilaya ya Mkinga ili kuwawezesha wananchi hasa
wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda
wao mwingi kutafuta maji.
Waziri Mkuu
alisemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua
mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini
wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Kuhusu suala la
upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu alisemamaeneo hayo yatasambaziwa umeme
kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi hawatowajibika
kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme
kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.
“Rais wetu Dkt.
John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena
kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza
umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vya wilaya hii ya Mkinga.
Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”
Kabla ya
kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alizindua miundombinu ya kituo cha
afya cha Maramba ambayo ilifanyiwa ukarabati na kusema kwamba Serikali
itaendelea kukiimarisha kituo hicho ili kukiboresha huduma za afya kwa
wananchi.
No comments:
Post a Comment