Pages

Tuesday, March 31, 2020

EKARI 328.6 ZIMETENGWA KWA AJILI YA UJENZI WA UWANJA WA MICHEZO JIJINI DODOMA



………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna, Dodma
Serikali ya Tanzania imesema imetenga eneo lenye Jumla ya ekari 328.6 kwa ajili ya ujenzi wa
Uwanja wa mchezo wa mpira wa miguu unaotarajiwa kujengwa jijini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe  wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Felister Bura (CCM) aliyetaka kujua ni lini uwanja wa Michezo utaanza kujengwa kutokana na serikali kupata ufadhili kutoka Serikali ya Morocco.
Dk Mwakyembe amesema baada ya kutenga eneo hilo serikali imefanya tathimini ya mazingira, kijamii na kuandaa mchoro wa awali wa uwanja huo.
Dk Mwakyembe amesema Serikali mbili za Tanzania na Morocco zinaendelea na mawasiliano kuhusu kukamilisha mradi wa ujenzi wa uwanja wa huo.
“ Maandalizi yote ya msingi kuhusu ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu tayali yamekamilika na tunaendelea kufanya mawasiliano na serikali ya Morocco ili kuweza kukamilisha mradi huo”, ameongeza Dk Mwakyembe.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa mradi huo unatokana na ahadi za Mfalme Mohamed VI alipofanya ziara yake Tanzania Oktoba, mwaka 2016 alitoa ahadi ya kufadhili miradi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mchezo wa mpira wa miguu.
Dk Mwakyembe amesema kuwa Serikali iliamua Uwanja huo ujengwe katika Jiji la Dodoma eneo la Nane Nane ambapo ndo makao makuu ya nchi.

No comments:

Post a Comment