Pages

Tuesday, March 31, 2020

Dkt. Mabula Awaka, Wakurugenzi Hawafuatilii Wadaiwa Sugu Kodi ya Pango la Ardhi.



Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Dkt. Angeline Mabula akizungumza na Wakurugenzi pamoja na Wataalam wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri sita za Mkoa wa Simiyu kuhusu ukusanyaji kodi ya Pango la Ardhi pamoja utunzaji wa nyaraka za
sekta ya Ardhi.
Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula, Akikabidhi vitendea kazi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bariadi Mjini, Melikzedek Humbe kwa niaba ya Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu mara baada ya kuzungumza na Wakurugenzi pamoja na Wataalam wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri hizo kuhusu ukusanyaji kodi ya Pango la Ardhi pamoja utunzaji wa nyaraka za sekta ya Ardhi.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami, akifafanua hali ya makusanyo ya kodi ya pango la Ardhi kwa nchi nzima, hadi sasa Serikali kupitia Wizara Ardhi inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ulipaji wa kodi hiyo.
******************************
Mwandishi Wetu- SIMIYU
Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amesema anasikitishwa sana na Wakurugenzi katika Halmashauri za Mkoa wa Simuyu kutojishughulisha hata kidogo na
ufuatiliaji wa kodi ya pango la Ardhi.

Naibu Waziri aliyasema hayo katika ziara yake Mkoani Simiyu, alipokutana na wakurugenzi pamoja na maafisa
mbalimbali wa Sekta ya Ardhi mkoani humo kwa lengo la kugawa vifaa vya kusaidia ukusanyaji kodi ya pango la Ardhi, pamoja na kukagua utunzaji wa nyaraka katika masjala za Ardhi.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Dkt Mabula alipata nafasi ya kupokea taarifa ya hali ya makusanyo ya kodi ya pango la Ardhi kutoka katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu na baadae taarifa ya jumla ya makusanyo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi ndugu Denis Masami kabla hajagawa vifaa vya kusaidia kazi ya ukusanyaji.

Taarifa ya jumla iliyowasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Kodi, ilionesha Mkoa wa Simiyu kuwa nyuma sana katika makusanyo. Ukilinganisha kiasi kilichokusanywa na Mkoa na lengo lililokusudiwa kukusanywa kwa mwaka,
bado hata nusu ya lengo haijafikiwa na muda uliobaki kumaliza mwaka wa fedha ni miezi miwili tuu.

Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi alisema, kwa kuliona hilo la kuwa nyuma kimakusanyo kama changamoto, Wizara iliamua kuzipatia Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu vifaa kama vile Karatasi na Wino ili kuongeza kasi katika ufuatiliaji wa kodi ya Pango la
Ardhi.

Aliongeza kwamba, Wizara imesaidia kupatikana hivyo vifaa ikiamini sasa hati za madai zitaandaliwa na wadaiwa watapelekewa ili kodi stahiki ya Serikali ikusanywe.

Nae Naibu Waziri Dkt Mabula wakati anakabidhi vifaa hivyo alisema, hakuna sababu tena ya Wakurugezi kutokukusanya kodi ya pango la Ardhi kwa kuwa vitendea kazi vya msingi wamepewa na Serikali kupitia Wizara.

Aliongeza kwamba, Wakurengi waone kazi ya makusanyo ya kodi ya Pango la Ardhi katika umuhimu wake kwani Sekta ya Ardhi ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment