
********************************
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
6.1.2019
SERIKALI katika kipindi cha mwaka
wa fedha 2019/2020 imepanga kutumia Tsh. Bilioni 301 kwa ajili ya
kukamilisha miradi ya maji vijijini inayoendelea kutekelezwa katika
maeneo
mbalimbali nchini, ambapo fedha za ndani ni Tsh. Bilioni 224.03
na fedha za nje ni Tsh. Bilioni 77.22.
Pamoja na juhudi hizo za Serikali
sekta ya maji imekuwa inakabiliwa na changamoto ya upotevu wa maji
kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyojengwa miaka mingi iliyopita.
Katika kukabiliana na changamoto
hizo, Serikali imeendelea na jitihada za uwekezaji katika ukarabati wa
miundombinu chakavu maeneo mbalimbali ya mijini ikiwemo Mikoa ya Dar es
Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Morogoro, Singida pamoja na ukarabati wa
miradi ya kitaifa ya Makonde, Wanging’ombe, Maswa, Mugango Kiabakari na
Chalinze.
Tanzania kupitia miradi ya maji
vijijini imejenga zaidi ya vituo 80,000 vya maji ambavyo vimeunganishwa
na mfumo wa maji ya bomba, ambapo baadhi ya vituo vimechakaa na kuhitaji
matengenezo lakini ukosefu wa takwimu sahihi juu ya vituo hivyo
kunaikwamisha Serikali kupanga bajeti ya kuwapatia wananchi wa vijijini
huduma bora ya maji.
Takwimu zilizopo katika Ripoti ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji ya mwaka 2016, zinaonyesha kuwa kati ya mwaka
2010/11 na mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kujenga jumla ya vituo vya
maji 99,515 lakini ilishia kujenga vituo 42,718 pekee.
Ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba
mwaka 2016 inaeleza kuwa theluthi moja ya miradi hiyo ya maji
haikutekelezwa ndani ya awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta
ya Maji (WSDPI) jambo lililofanya baadhi ya vituo vya maji vichelewe
kujengwa.
Ili kuboresha upatikanaji wa maji
maeneo ya vijijini, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo
imeendelea kuimarisha Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi
wa Mazingira Vijijini kwa kutumia Mfumo wa Malipo kwa Matokeo (Payment
by Results – PbR) unaolenga kuongeza kasi ya uendeshaji, matengenezo na
ukarabati wa miundombinu ya miradi ya maji vijijini.
Kupitia Programu hiyo, Serikali
imeanza kuziwezesha Halmashauri za Miji nchini kuviendeleza vituo vya
maji vilivyopo na kutumia takwimu kujenga vingine vipya katika maeneo
yenye uhitaji mkubwa wa maji.
Ili kufikia malengo ya Programu
hiyo, mwaka 2017 wataalamu hao walitembelea vituo 9,0000 katika
Halmashauri 56 nchini vijiji ili kujionea hali halisi ya utendaji wa
vituo vya maji, ambapo ilibainika kutofautiana kwa taarifa za baadhi ya
vituo zilizopo Wizara ya Maji na Umwagiliaji na eneo kilipo ikizingatiwa
kuwa maeneo mengi ya vijijini hayana anuani na mitaa yenye mpangilio
mzuri.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio
ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Maji,
Prof. Makame Mbarawa anasema katika jitihada za kuhakikisha miradi ya
maji vijijini inakuwa endelevu, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la
Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID) inatekeleza Mpango wa Mfumo
wa Malipo kwa Matokeo (Payment by Results – PbR) ambao una lengo la
kuimarisha uendelevu wa miradi ya maji vijijini.
Anasema kuwa hadi April 2019,
awamu ya pili ya programu hiyo imekamilika ambapo Halmashauri 95
zilifuzu na kupewa Shilingi bilioni 8.55 kati ya Shilingi bilioni 53.6
zilizotengwa katika mwaka 2017/2018, ambapo awamu ya tatu inaendelea na
inahusisha Halmashauri 181 ambazo zitapewa fedha kwa vigezo vya idadi ya
vituo vilivyojengwa na kutoa maji.
‘Kupitia PbR, Paundi 300 hutolewa
kwa kila kituo kilichohakikiwa na kinachofanya kazi na Paundi 1,500
hutolewa kwa kituo kipya kitakachojengwa, Katika mwaka 2018/2019, jumla
ya Paundi milioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza programu hiyo
kwenye Halmashauri zote nchini’’ alisema Waziri Mbarawa.
Aliongeza kuwa Hadi mwezi Aprili
2019, fedha zilizolipwa katika awamu ya tatu ni Paundi milioni 8.7 sawa
na Shilingi bilioni 25.43. Katika mwaka 2019/2020, Shilingi bilioni
46.47 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo.
Maji ni
rasilimali muhimu kwa maisha ya binadamu na maendeleo ya jamii na sekta
mbalimbali za kiuchumi zikiwemo viwanda, kilimo, uvuvi na utalii, ili
kufikia azma ya Serikali ya kuwapatia wananchi majisafi na salama pamoja
na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kufikia mwaka 2025,
Wizara inatekeleza mipango mbalimbali.
Ni wajibu wa wananchi na wadau wote kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji
wa takwimu na taarifa za mwenendo wa rasilimali za maji ili kuimarisha
usanifu wa miundombinu ya kusambaza maji nchini.
No comments:
Post a Comment