Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando akiandika taarifa za kazi ofisini kwake.
Ofisa madini mkazi
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando akikagua madini ya yaliyokamatwa
Kata ya Hedaru Wilayani Same yakisafirishwa kwenda jijini Dar es salaam
bila kibali.
……………………………………..
TANI tatu za madini
mchanganyiko yenye thamani ya sh15 milioni yamekamatwa Mkoani
Kilimanjaro, mengine yakisafirishwa kwenda kuuzwa jijini Dar es salaam
bila kuwa na kibali.
Ofisa madini mkazi
wa mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando alisema watu saba walikamatwa
kwenye maeneo tofauti wakiwa na madini hayo.
Kyando alisema watu
watatu walikamatwa na madini aina ya Feldspar Carrot kwenye eneo la
Hedaru wilayani Same wakitoa wilayani Simanjiro mkoani Manyara
wakiyasafirisha jijini Dar es salaam.
Alisema watu wawili
walikamatwa wilayani Same wakiwa na madini ya vito aina ya Red garnet na
Almandite bila kuwa na kibali cha aina yoyote kinachowapa haki ya kuwa
na madini hayo.
Alisema mjini Moshi
waliyakamata madini tofauti ikiwemo vito mchanganyiko na madini ya
viwanda na watu wawili ambao hawakuwa na kibali cha kuwa na madini
hayo.
“Tulishirikiana na
askari polisi kwenye matukio hayo hapa Moshi na kule wilayani Same
akiwemo OCCID na askari polisi wa kituo kidogo cha Hedaru katika
kuwakamata watuhumiwa hao,” alisema Kyando.
Mmoja kati ya
wachimbaji madini wa mkoa huo, Godfrey Kiangi alipongeza ofisi ya madini
ya mkoa wa Kilimanjaro kwa kazi kubwa wanayofanya na ushirikiano
wanaotoa kwa wadau.
Kiangi alisema
utendaji kazi wa ofisi ya madini Kilimanjaro ni mzuri kwani wanatoa
huduma bora ikiwemo maelezo yaliyojitosheleza na utunzaji wa mazingira
mzuri.
“Hakuna urasimu
kwenye ofisi zao na pia unaweza kupiga simu saa 24 ukapatiwa huduma
kwani wanafanya kazi kwa vitendo bila ubaguzi wa kufahamiana hivyo
wanastahili hongera kwa kazi nzuri wanayofanya,” alisema.
Hata hivyo, aliwaasa
wafanyakazi wa serikali wa ofisi nyingine kufanya kazi zao kwa kuiga
mambo mazuri yanayofanywa na ofisi ya madini mkoani Kilimanjaro ambapo
ukimaliziwa tatizo una hamu ya kurudi kwa namna huduma inavyotolewa.
No comments:
Post a Comment