Waziri wa Katiba na Sheria Mh.
Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) akisalimiana na afisa wa magereza
wakati wa ziara ya kikazi katika gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe
Jijini Mbeya. Nyuma ya Waziri Mahiga ni Mkuu wa Gereza la Tukuyu ASP.
Samwel J. Kaluwa (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka (DPP) Biswalo
Mganga (katikati).
Waziri wa Katiba na Sheria Mh.
Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) akisalimiana na afisa wa magereza
wakati wa ziara ya kikazi katika gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe
Jijini Mbeya. Kushoto ni Mkuu wa Gereza la Tukuyu ASP. Samwel J. Kaluwa
akiwatambulisha Staff wa gereza hilo mbele ya Waziri.
Waziri wa Katiba na Sheria Mh.
Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) katikati akiwa katika picha ya pamoja
na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mh. Chalya J. Nyangidu (wa pili kushoto) na
Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Biswalo Mganga (wa pili kulia),
walipotembelea Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya leo tarehe 28 Nov. 2019
wakati wa ziara ya kikazi wilayani humo.
Waziri wa Katiba na Sheria Mh.
Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) kulia akiwa na mwenyeji wake Kamishna
Msaidizi wa Magereza Mkoa wa Mbeya Mathias Mkama (ACP) katikati,
alipotembelea Gereza Kuu la Ruanda Mbeya 27 Nov. 2019. Kushoto ni
Kamishna Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza la Ruanda Mbeya
Vendeline Tesha wakati wa ziara ya kikazi jijini humo.
……………….
Katika mwendelezo wa ziara ya
kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga
(Mb) kwenye mikoa ya kusini, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Tanzania (DPP)
Biswalo Mganga amefuta jumla ya kesi 59 katika mahakama za Mkoa wa
Mbeya.
Mkurugenzi Biswalo ameyafanya hayo
katika gereza la Ruanda mjini Mbeya na gereza la
Tukuyu Wilaya ya
Rungwe alipoambatana na Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Mahiga ili
kujionea hali halisi ya mazingira ya utoaji haki jinai katika magereza
hayo na taasisi mbalimbali za haki jinai ikiwemo Ofisi ya Taifa ya
Mashitaka, Polisi, Mahakama na Magereza yenyewe.
“Niliowafutia Kesi nendeni mkawe
raia wema, msirudie makosa, badala yake mkawe mabalozi wema mtakaofanya
kazi kwa bidii ili kumuunga mkono Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe
Joseph Maguli katika kauli yake ya hapa kazi tu.”
Kwa upande wake Waziri mwenye
dhamana ya Katiba na Sheria Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) aliwataka
wote waliofutiwa mashitaka kwenda kufurahi na familia zao huku
wakimshukuru Mungu na kujutia makosa yaliyosababisha kushitakiwa kwao.
Aidha, aliwaonya kutokurudia makosa hayo badala yake watumie nguvu na
akili walizonazo kuzalisha mali kwa maendeleo yao na familia zao pamoja
na kukuza uchumi wa Taifa.
“Mliosamehewa leo nendeni
mkafurahi na familia zenu sambamba na kuwa watu wema katika jamii
inayowazunguka kwani ni matumaini yangu kuwa mmejifunza mengi na
mmebadilika. Kuna watu hapa nikiwatizama misuli yao, walipaswa
wakaitumie kufanya kazi na kuzalisha mali kwa maendeleo yao na Taifa kwa
ujumla badala ya kuitumia kufanya uhalifu.”
Kwa mujibu wa kifungu cha 91(1)
cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa
marejeo 2002, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka anayo mamlaka ya kuwafutia
mashitaka watuhumiwa wa makosa ya jinai katika magereza mbalimbali
nchini. Mpaka sasa katika ziara hii ya kikazi ya Waziri wa Katiba na
Sheria katika mikoa mitatu DPP Biswalo ameshafuta jumla ya kesi 120 na
bado ziara inaendelea katika Wilaya ya Kyela na baadae mkoa wa Njombe.
No comments:
Post a Comment