*******************************
Shirika la Reli Tanzania nchini –
TRC latoa nafasi 20 za mafunzo kwa vitendo kwa muda wa
miezi miwili
katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kwa wahandisi wanawake
katika hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya makao makuu
TRC Dar es Salaam hivi karibuni Oktoba 01, 2019.
Lengo la kutoa nafasi hizo kwa
wahandisi wanawake ni kuwaongezea ujuzi lakini pia kuongeza idadi ya
wahandisi wanawake katika Miradi ya Shirika hususani mradi wa SGR ili
waweze kujenga na kubuni miundombinu ya reli nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu
Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa Shirika limetoa nafasi hizo ili
kuhamasisha wanawake na kuondoa dhana ya kwamba shughuli za uhandisi
zinafanywa na wanaume na si wanawake, pia amewaasa kuwa na moyo wa
kulitumikia taifa lao na kuwa na uthubutu wa kufanya vitu kwa maendeleo
ya taifa.
“Watu wanapopata nafasi ya mafunzo kama haya, ni dhahiri wanapaswa kuyafanyia kazi” alisema Ndugu Kadogosa.
Aidha Ndugu Kadogosa alisema kuwa
TRC ni sehemu nzuri ya kupata mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wa
nyanja tofauti na pia kuwasihi wahandisi hao kujenga tabia ya kufuatilia
miradi ya reli katika nchi za nje kupitia mtandao ili kupata ujuzi
zaidi.
Naye Msajili wa Bodi ya Wahandisi
kutoka Bodi ya Usajili Wahandisi Tanzania – ERB, Mhandisi Patric Balozi
amesema mafunzo haya ya vitendo kwa kundi hili maalumu la wahandisi
wanawake yatasaidia kuongeza wingi wa wataalamu hapa nchini na kuacha
kutegemea wataalamu wa nje.
“Watanzinia wawe wazalendo kwaajili ya kutumikia nchi yao wenyewe”, alisema Mhandisi Balozi
Mhandisi Balozi ametoa shukurani
kwa Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa kutoa nafasi hii na kusema kuwa
wanawake wanapopata nafasi kama hizi wanatakiwa kujituma hali hii
itawafanya kuwa wakakamavu na kushirikiana kwa pamoja katika maendeleo
ya kujenga taifa.
“Tunawahamasisha wahandisi wa kike ili tusiwapoteze, watumie
nafasi hii kujifunza waweze kuwa katika historia ya mradi mkubwa wa SGR”
alisema Mhandisi Balozi.
Meneja Mradi ujenzi wa Reli ya SGR
kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro Mhandisi Machibya Masanja
amesema kuwa kikubwa ni juhudi katika kazi na kujifunza, pia
amewakaribisha wahandisi hao kujifunza ili kuweza kuendesha miradi ya
reli itakayoendelea .
No comments:
Post a Comment