Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika
Kitaifa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mjini Mtwara, Oktoba 1, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika
Kitaifa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mjini Mtwara, Oktoba 1, 2019.
Kulia ni Mkalimani wa lugha ya alama, Ally Nalinga Uwesu.(Picha na
ofisi ya Waziri Mkuu)
………………..
WAZIRI MKUU amesema Serikali
itaendelea kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya ukatili,
kuwawekea
miundombinu na mazingira bora katika kutumia vyombo vya usafiri na
kuweka utaratibu na vigezo vitakavyowawezesha kulipwa pensheni.
Waziri Mkuu
ameyataka mashirika ya wazee yaelekeze rasilimali wanazozipata katika
kutoa huduma za msingi kwa wazee na waepuke kutumia fedha nyingi kwenye
mikutano, warsha na makongamano ambayo hayawafaidishi moja kwa moja
wazee wenye uhitaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumanne, Oktoba 1, 2019) wakati akihutubia wananchi katika kilele cha
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa
katika Uwanja Nangwanda Sijaona Manispaa ya Mtwara.
Amesema utoaji wa huduma kwa
wazee ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli na kwamba itaendelea kuchukua hatua za
makusudi kwa lengo la kuboresha hali na maisha ya wazee nchini.
Amesema miongoni mwa hatua
zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha ustawi na maendeleo ya
wazee ni pamoja na kuanzishwa kwa mpango wa TASAF wa kunusuru kaya
masikini uliolenga kuyasaidia makundi mbalimbali ya jamii yanayoishi
katika umasikini uliokithiri likiwemo kundi la wazee.
“Hadi kufikia Septemba 2019
jumla ya wazee 680,056 kutoka kaya 1,118,747 wananufaika na mpango wa
TASAF kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Mpango huu, umesaidia wazee
kujikimu na kumudu majukumu ya kulea wajukuu ambao wazazi wao wamepoteza
maisha kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa ukimwi.”
Amesema Serikali pia inaendelea
kutekeleza Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inatambua kuwa
wazee ni kundi maalumu linalohitaji kupewa kipaumbele katika kupata
huduma bora za afya, inaweka mkazo kuwa wazee wote wenye umri wa miaka
60 na kuendelea na wasiokuwa na uwezo watibiwe bila malipo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
ameendelea kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zoezi la
kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wazee wasiokuwa na uwezo linakuwa
endelevu ili waweze kunufaika na huduma ya matibabu bila
malipo wanapougua.
Kadhalika, Waziri Mkuu
amevitaka vituo vyote vya kutoa huduma za afya vya umma kutoa huduma
bora na za haraka kwa wazee wenye vitambulisho hivyo na watenge dirisha
maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wazee ili wasikae kwenye foleni muda
mrefu.
Akizungumzia kuhusu matunzo ya
wazee, Waziri Mkuu amesema Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003
inatamka kuwa familia na jamii zina wajibu wa msingi wa kuwatunza na
kuwahudumia wazee.
“Hii ni kutokana na ukweli
kuwa mazingira ya familia yanamuwezesha mzee kujiona sehemu ya jamii na
hivyo, kumfanya aondokane na msongo wa mawazo unaotokana na upweke na
kutengwa. Familia kwa mtazamo wa hapa nchini kwetu inajumuisha baba,
mama, watoto pamoja na ndugu wengine.”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa
familia, jamii na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutimiza wajibu wao wa
kutoa matunzo na malezi kwa wazee wasiojiweza, hatua ambayo itaonesha
kuwa jamii inathamini mchango mkubwa walioutoa wazee kwa ustawi na
maendeleo ya Taifa. “Vilevile, nisisitize kuwa jukumu la kuwatunza wazee
ni la kila mmoja wetu, hivyo kila mmoja anawajibika kuwatunza wazee.”
“Nyote mtakubaliana nami kuwa
matunzo ya wazee katika makazi hutolewa kwa wazee wasiojiweza na wasio
na ndugu wa kuwatunza. Suala la kumpeleka mzee katika makazi ya wazee
litakuwa ni kimbilio la mwisho baada ya njia nyingine zote za matunzo
katika familia na jamii kushindikana.”
Waziri Mkuu amewataka
vijana na jamii kwa ujumla wasikwepe jukumu la kuwatunza wazee kwa
sababu bila wao wasingekuwa hivyo walivyo leo. Ikumbukwe kuwa wazee hao
nguvu zao za uzalishaji mali zimepungua kutokana na kazi waliyoifanya
wakiwa vijana kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa familia zetu na Taifa
kwa ujumla.
Pia, Waziri Mkuu ameziagiza
Mamlaka za Serikali za Mitaa ziombe vibali vya ajira ili
waajiri Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii Wasaidizi
ambao wanahitajika kufanya kazi kuanzia ngazi za Kata hadi Halmashauri
ikiwemo kushughulikia changamoto za wazee katika jamii.
Pia, Waziri Mkuu ameielekeza
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iendelee
kuimarisha na kusimamia Mabaraza ya Wazee ili yashiriki kikamilifu
kuelimisha familia na jamii kutimiza wajibu wao wa kutunza wazee.
Pia, Waziri Mkuu ametaja
changamoto zinazowakabili wazee ni pamoja na vitendo vya mauaji ya wazee
kutokana na imani za kishirikina. “Napenda kurudia Wito kwa jamii
kuhusu kuongeza mapambano ya kutokomeza vitendo vya mauaji kwa wazee
wasiokuwa na hatia. Wakuu wa mikoa na wilaya waweke utaratibu maalumu wa
kuwalinda wazee.”
Awali,Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema lengo
la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala
mbalimbali ya wazee ikiwa ni pamoja na kutafakari fursa za changamoto
zinazowakabili wazee na namna ya kuzitatua.
Waziri Ummy alisema kupitia
maadhimisho hayo jamii inakumbushwa kuzingatia kwa kutekeleza kwa
umuhimu haki za wazee na wazee nao wanakumbushwa wajibu wao kwa wajibu
wao kwa jamii. Sens aya watu na makazi ya 2012 Tanzania inakadiriwa kuwa
na wazee 2,507,568 sawa na asilimia 5.6 ya wananchi wote.
Alisema taarifa kutoka Ofisi
ya Rais-TAMISEMI, hadi Desemba 2018 jumla ya wazee 1,837,162
wametambuliwa na kati yao wazee 684,383 sawa na asilimia 37 ya wasiokuwa
na uwezo wamepatiwa vitambulisho vinavyowawezesha kupata huduma za
matibabu bila ya malipo. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 319
mara tatu zaidi ya idadi ya wazee 214,370 waliopewa vitambulisho vya
matibabu kwa 2016/2017.
No comments:
Post a Comment