KUWEPO KWA SERA INAYOMLINDA MWANAHABARI MWANAMKE KATIKA KILA CHOMBO CHA HABARI ITALETA USAWA NA KUPUNGUZA UKATILI WA KIJINSIA.
Na Zena Mohamed,Dodoma
WANAHABARI wanawake wamekuwa na mchango mkubwa
katika ujenzi wa Taifa kutokana na kujitoa kwa kufanya kazi kwa juhudi
kubwa na maarifa ili kuleta tija katika taasisi, taifa na wao wenyewe
pia. Mwanahabari mwanamke anamchango mkubwa katika kuleta
maendeleo licha ya kwamba huwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
katika maeneo yao ya kazi jambo ambalo husababisha kutekeleza majukumu
yao katika mazingira magumu. Miongoni mwa changamoto ambazo huwarudisha nyuma wanahabari
wanawake wakati wa harakati za utekelezaji wa majukumu yao ni pamoja na
unyanyasaji wanaofanyiwa ndani ya vyumba vya habari na sehemu
mbalimbali za kazi huku wengine wakishindwa na kuchukua umamuzi wa
kuomba kuhama ama kuacha kazi. Unyanyasaji wa wanahabari wanawake hasa katika nchi za
ulimwengu wa tatu umekuwa ukiongezeka mara kwa mara licha ya asasi
mbalimbali za kiraia kama Chama cha waandishi wanawake Tanzania
(TAMWA),kuchukua jukumu la kutoa elimu kwa wadau ili kukomesha vitendo
hivyo ambavyo huwanyima haki ya msingi ya kufanya kazi kwa uhuru mkubwa
kunakosababishwa na unyanyasaji wa wanawake kazini. Kumekuwa na matukio mengi ambayo huripotiwa katika vyombo
mbalimbali vya habari hapa nchini kuhusu unyanyasaji unaofanywa sehemu
za kazi ambapo wanawake husumbuliwa na mabosi zao lakini kwa waandishi
wa habari wanawake imekuwa ngumu taarifa zao kupaa kutokana na wao ndio
watoa taarifa za wengine. Waajiri wengi wanaume muda mwingine huwanyanyasa wanahabari
wanawake kwa kuwaomba rushwa ya ngono kabla ya kuwaajiri na wakati
mwingine licha ya kuwa na sifa, vigezo na uzoefu wa kazi, mwanamke
anaweza kukosa kazi kwa kutokubali kutoa rushwa ya ngono kwa mwajiri
huku wengine wakiamua kutoa ili tu kupata kazi kutokana na changamoto
walizonazo na kutaka kujikwamua. Unyanyasaji wa wanahabari wanawake sehemu za kazi umekuwa
ukiwaletea madhara mbalimbali wanawake ikiwa ni pamoja na kuathirika
kisaikolojia, kutotekeleza majukumu yao kikamilifu na kwa ufanisi,
kuambukizwa magonjwa ya zinaa, kuzaa na watu wasiowapenda na kusababisha
migogoro isiyoisha kutokana na kukubali bila kuridhika. Vitendo hivi vya unyanyasaji wa wanawake na wanawake
wanahabari kazini vikikomeshwa, itasaidia kujenga Taifa lenye uchumi
imara kutokana na mwanamke kuwa na nguvu kubwa katika kufanya kazi kwa
bidii na ufanisi lakini pia kujenga jamii huru na yenye usawa katika
utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Pamoja na Asasi za Kirai kutoa elimu kwa wadau na waandishi
wa habari kuhusu unyanyasaji wa wanawake maeneo ya kazi, sheria ya Ajira
na Mahusiano kazini ya mwaka 2004 haijatamka wazi kupinga unyanyasaji
huu. Sheria hiyo sehemu ya pili katika haki za msingi na ulinzi
7(4) inaeleza kuwa Mwajiri yeyote asifanye ubaguzi wa dhahiri au
usiokuwa wa dhahiri kwa mwajiriwa, katika sera au mazoea huku ikitaja
kwa Mwanamke na Mwanaume, Jinsia na ujauzito pekee. Sheria haijaeleza wazi kuhusu unyanyasaji unaofanywa kwa
wanawake pindi wanapoomba kazi ama unyanyasaji wanaofanyiwa wanawake
waliomo katika ajira jambo ambalo ni kikwazo kikubwa kwao kuweza
kupigania haki zao. Tafiti za kina zinaonesha kuwa hali ya unyanyasaji wa kingono
makazini kwa wanawawake wenye umri kati ya miaka 25 hadi 35 ni mbaya
zaidi ikilinganishwa na wanawake wengine ambapo theluthi mbili ya
wanawake hao wamesema kuwa wamewahi kunyanyaswa kingono katika maeneo
yao ya kazi. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa Makala hii kwa kuwahoji
baadhi ya wanahabari wanawake ambao wameajiriwa katika vyombo tofauti
vya habari tofauti unaonesha kuwa takribani mwanamke mwanahabari mmoja
kati ya 10 amenyanyaswa kingono na mkubwa wake wa kazi ama chanzo cha
habari kikiwa ni mwanaume. Uchunguzi huo unaonesha kuwa baadhi ya wanawake makazini
wamekuwa wakitumiwa vibaya kingono katika maeneo yao ya kazi na
kufanyiwa utani usiofaa ambapo asilimia 80 ya wanawake hao wanaofanyiwa
unyanyasaji huo wa kingono hushindwa kuripoti kwa waajiri wao kwa
kuhofia kuharibika uhusiano wao katika mazingira ya kazini. Katika kuhakikisha unyanyasaji wa wanawake kazini unakoma,
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kimekuwa kikitoa mafunzo
mbalimbali kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuripoti
unyanyasaji wanaofanyiwa wanawake kwenye maeneo yao kazi ili kukomesha
tabia hizo na kuleta usawa wa kijinsia. TAMWA imekuwa mstari wa mbele katika kupigania aina zote za
unyanysaji unaofanywa kwa wanawake kwa kuamini kwamba, Mwanamke akiachwa
huru bila kunyanyaswa ataweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi
kuliko Mwanaume na hivyo kutoa mchango mkubwa wa maendeleo kuanzia ngazi
ya familia hadi Taifa .
Hivi karibu TAMWA imetoa mafunzo kwa wanahabari
nakuelekeza kufanyika baadhi ya mambo ili kukomesha vitendo vya
unyanyasaji wa wahabari wanawake wawapo makazini ambapo imeshauri kila
chombo cha habari kuwa na sera inayomlinda mwanahabari mwanamke awapo
chumba cha habari ilikuweza kutimiza majukumu yake pasipo kunyanyasika.
No comments:
Post a Comment