Pages

Monday, September 30, 2019

KATIBU MKUU MWAKALINGA AMKALIA KOONI MKANDARASI


Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mbeya Eng. Mwita Magesa, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, kuhusu hatua za ujenzi zilizofikiwa katika barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39 kwa kiwango cha lami, mkoani Mbeya.

Muonekano wa sehemu ya lami ya prime katika  ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39 kwa kiwango cha lami, mkoani Mbeya. Mradi huu unagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 59 ambazo ni fedha za Serikali na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2020.

Timu ya wahandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) ikiongozwa na Mhandisi Joyce Mbunju, wakikagua tabaka la juu la barabara kwa mawe yaliyosagwa KM 9.18, kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39, mkoani Mbeya.


Kazi zikiendelea za usukaji wa nondo katika Daraja la Lupa litakalokuwa na urefu wa mita 63 katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39, mkoani Mbeya.KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Chunya -Makongolosi kwa kiwango cha lami kuhakikisha anamaliza mradi huo ndani ya muda wa mkataba na si vinginevyo.
 Aidha, ameongeza kuwa hatamuongezea mkandarasi huyo muda wa kumaliza kwani muda aliopewa ulikuwa unamtosha kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
 Hayo ameyasema mkoani Mbeya alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amemuelekeza mkandarasi huyo kuongeza vitendea kazi na wataalamu ili kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliobakia.
 "Natarajia utaongeza vifaa na wataalamu ili kuhakikisha kazi hii inakamilika kwa wakati, pia ukumbuke kuwa sitakupa muda wa nyongeza hivyo fanya juhudi ili umalize mradi huu ndani ya muda", amesisitiza Arch. Mwakalinga.
 Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39 unajengwa na mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 59 ambazo zote ni fedha za Serikali na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2020.
 Arch. Mwakalinga amemuelekeza pia mkandarasi kutumia muda wake wote kuwa katika eneo la mradi hata ikiwezekana kuongeza masaa ya kufanya kazi usiku na mchana.
 "Fanyeni kazi usiku na mchana ili kuepukana na changamoto za vipindi vya mvua na hakikisheni barabara hii inajengwa kwa viwango vya ubora zaidi", amesema Arch. Mwakalinga.
 Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mbeya Eng. Mwita Magesa, amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 53 ukilinganisha na muda wa mkataba uliotumika ambao ni miezi 23 sawa na asilimia 85.19 ya muda wa mkataba.
 Eng. Mwita ameeleza kuwa mkandarasi mpaka sasa ameshakamilisha kujenga tabaka la juu la barabara kwa mawe yaliyosagwa KM 9.18, lami ya prime KM 6.78 na kazi zingine za ujenzi wa makalvati madogo na madaraja makubwa matatu zikiendelea.
 Mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39 ni sehemu ya barabara ya Mbeya-Rungwa yenye urefu wa KM 293 inayounganisha mkoa wa Mbeya na mikoa jirani ya Singida na Tabora ambapo barabara hii ikikamilika itaongeza zaidi fursa za kimaendeleo kwa wananchi kiuchumi na usafirishaji.

No comments:

Post a Comment