Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa UTT AMIS, Simon Migangala.
Rais Dkt. John Magufuli Aakimkagua
samaki na kumnunua kwa mfanyabiashara wa soko la Samaki Feri, jijini
Dar es Salaam alipofany ziara ya kutembelea wafanyabiashara wadogo
wanaotumia vitambulisho vya wajasiriamali ambao wanaweza kukuza mtaji
wao kupitia uwekezaji kwenye Mfuko wa Hati Fungani.
……………………
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wengi wanatafuta
mafanikio maishani mwao lakini bila kuwa na bidii,
ustahimilivu, nidhamu
na shauku kubwa, huwezi kupata mafanikio ya kweli.
Kuna mbinu mbalimbali ambazo kila mwananchi anayetafuta mafanikio anaweza kuzitumia ili kufikisha lengo alilonalo.
Jambo la kwanza ni kujua unataka nini, ukijua unachotaka utakuwa na msimamo wa kutaka kufikia malengo yako.
Kama hujui unachotaka, jambo la msingi, chukua kalamu na karatasi kisha jiulize unataka kufanikiwa kitu gani?
Ni muhimu wakati unajiuliza, usifikirie mawazo hasi au mabaya ya kujiona kama utashindwa kufanikiwa bali kiajimi.
Ondoa wasiwasi wowote ambao
utakuwa nao, orodhesha mambo yote unayotaka kufanikiwa, anza kupanga
mipango kwa kujiwekea malengo, kutekeleza moja baada ya jingine.
Utajiri siyo fedha ambazo mtu anakusanya bali ni fedha ambazo huwekwa na kufanya kazi.
Tamaduni zetu zimeifanya jamii
kubwa kuhifadhi fedha ndani kwenye vyungu, magodoro hata vibubu. Njia
hizo zimekuwa zikibadilika taratibu sawa na ukuaji wa elimu na
teknolojia.
Uwekaji akiba na uwekezaji ni dhana mbili tofauti. Uwekaji akiba ni tabia nzuri lakini bila kuziwekeza ni bure.
Ili uwe muwekaji akiba mzuri,
unapaswa kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwani uwekezaji una uwiano
mkubwa na muda. Muda unapozidi kuwa mrefu na uwekezaji wako unazidi
kukuwa mkubwa. Mara zote pesa ndani ya uwekezaji UTT AMIS zinawekezwa
katika mpango wa faida jumusihi ambapo muda huwa ni jambo la msingi
kabisa.
UTT AMIS ni taasisi ya Serikali ambayo imepewa dhamana ya usimamizi wa mali kupitia Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.
Nchini Tanzania unaweza kuwekeza
fedha zako katika masoko ya fedha, mitaji. Hatua hiyo inahusisha akaunti
za muda maalum na zisizo za muda maalum katika benki za biashara.
Pia hati fungani za Serikali za
muda mfupi, mrefu, kampuni na hisa zilizo orodheswa katika Soko la Hisa
Dar es Salaam (DSE) ambazo zina nafasi kubwa ya kurejesha gawio zuri.
Uwekezaji unaofanywa na taasisi
hiyo kupitia mifuko ambayo wanaisimamia ni fursa mbadala inayowezasha
mtu, watu, vikundi, taasisi, kampuni kuwekeza pesa zao kwa Meneja wa
UTT.
Meneja wa mfuko huzichukua fedha
hizo, kuziwekeza kwenye masoko ya fedha na mitaji kulingana na waraka wa
makubaliano. Waraka wa makubaliano ni maandiko ya kisheria yanayo
zungumzia haki za pande zote mbili meneja na mwekezaji pia huanisha
sehemu za kuwekeza na uwiano wa kuwekeza.
Faida inayopatikana hugawanywa
kwa wawekezaji kulingana na uwiano wa uwekezaji uliofanyika kwenye
mfuko husika. Awali UTT ilipewa dhamana ya usimamizi wa mifuko mitano.
Mifuko hiyo ni Mfuko wa Umoja,
Wekeza Maisha, Watoto, Mfuko wa Kujikimu na Mfuko wa Ukwasi. Hivi sasa
taasisi hiyo imeongeza mfuko mwingine wa Hati Fungani.
Mfuko wa Umoja, ulioanzishwa Mei
16, 2005 ukilenga kutimiza mahitaji tofauti ya wawekezaji. Awali bei ya
kipande ilikuwa sh. 70, kwa sasa sh. 582.
Sifa zilizopo katika mfuko huo ni
vipande kuuzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga). kiwango
cha chini cha kujiunga ni vipande 10 tu, malipo ya mauzo hutozwa
asilimia moja ya thamani halisi, pia ni rahisi kujiunga na kutoka,
manunuzi na mauzo hufanyika kila siku ya kazi.
Mfuko wa Watoto una lengo la
kuwasaidia watoto katika maendeleo yao nchini. Awali bei ya kipande
ilikuwa sh. 100, mfuko ulianzishwa Oktoba 1, 2008.
Na kwa sasa thamani ya kipande
katika mfuko wa watoto ni shilingi 348 Sifa za mfuko huo ni uwekezaji
kwa ajili ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 18. Kiwango cha chini cha
uwekezaji sh. 10,000, unaruhusiwa kuwekeza kidogo kidogo kwa sh. 5,000.
Sifa nyingine ni vipande kuuzwa
kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga), mfuko hutoa mipango ya
aina mbili, kwanza malipo ya ada, pili mpango wa kukuza mtaji.
Malipo ya ada na mauzo ya vipande
yanaruhusiwa pale mtoto anapofikisha miaka 12. Mfuko huo ni miongoni mwa
mifuko inayotatua changamoto za kielimu hasa katika ulipaji ada kwa
wanafunzi, kutoa mtaji baada ya ukomo wa shule kufikia.
Pia mfuko una mipango miwili
mikubwa, mpango wa ada za shule na mtaji kwa mwanao. Ili mzazi aweze
kuchangia kupitia mfuko huo, anapaswa kuweka sh. 10,000 kima cha chini
na hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu. Mwekezaji anaweza kuwekeza mara
kwa mara kadri anaweza.
Mfuko wa Jikimu una lengo la
kukidhi mahitaji ya wawekezaji wanaohitaji uhakika wa mapato ya mara kwa
mara, ulianzishwa Novemba 3, 2008 ukiwa na sifa za mipango ya
uwekezaji, kiwango cha uwekezaji, mpango wa gawio robo mwaka.
Kiwango cha chini kuwekeza ili
kupata gawio mara nne kwa mwaka yaani kila robo mwaka ni shilingi
milioni 2. Mpango wa gawio wa mwaka (kiwango cha chini cha uwekezaji sh.
milioni moja), tatu mpango wa mwaka wa kukua (sh. 5,000).Vipande
vinauzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga).
Mfuko wa Ukwasi unaotoa nafasi ya
uwekezaji mbadala kwa wawekezaji wakubwa au taasisi ambao wangependa
kuwekeza fedha zao za ziada kwa kipindi kifupi ama cha kati huku
wakikuza mtaji wao.
Ulianzishwa Aprili 30, 2013, bei
ya kipande ikiwa sh. 100.00, hivi sasa imepanda hadi zaidi ya sh. 219
hii ikiwa ina maana ya kuwa mfuko umekua mara 2.19 ndani ya miaka mitano
au umekuwa kwa asilimia 119 huu ni ukuwaji mzuri sana kibiashara. Sifa
za mfuko huo ni rahisi mwekezaji kupata fedha zake za mauzo ya vipande
ndani ya siku tatu za kazi baada ya maombi ya kuuza vipande kupokelewa
Makao Makuu ya UTT AMIS.
Mfuko huo hauna ada ya kujitoa
wala kujiunga, una unafuu wa gharama za uwekezaji, unafaa kwa
wawekezaji mmoja mmoja au taasisi, kiwago cha chini cha kuwekeza sh.
5,000,000.00.
Kuongeza uwekezaji wako sh.
1,000,000.00, pia unaruhusu uhamishaji vipande kutoka kwa mwekezaji
mmoja kwenda mwingine, kuruhuusu uhamishaji vipande kwenda kwenye mifuko
mingine, kuviuza kwa thamani halisi.
Mfuko wa Wekeza Maisha unamwezesha mwekezaji kupata faida pacha (mapato mazuri pamoja na mafao ya bima).
Mfuko huo ulianzishwa Mei 16,2007,
wawekezaji kati ya miaka 18 na 55 ndio wanaoruhusiwa kujiunga. Unatoa
mipango ya aina mbili, kuchangia uwekezaji awamu ya kwanza, mkupuo
mmoja.
Vipande vinauzwa kwa thamani
halisi, hakuna gharama za kujiunga. Kujiunga ni sh. 8,340.00 tu kwa
mwezi. Mafao ya bima yanayopatikana ni bima ya maisha, ulemavu wa kudumu
na bima ya ajali.
Mfuko unamwezesha mwekezaji
kuwekeza kwa mpangilio, kuchangia kwa mwezi, mara mbili kwa mwaka, mara
moja kwa mwaka ambapo faida za uwekezaji katika Mifukoya Uwekezaji wa
Pamoja ni kukuza mtaji kwa kutoa faida nzuri ukilinganisha na mifuko
mingine kwenye masoko ya fedha.
Faida nyingine ni kutawanya hatari
za uwekezaji, mwekezaji hupunguza athari za uwekezaji kwa kuwekeza
katika uwekezaji anuai, wawekezaji kufaidika na unafuu wa gharama za
uwekezaji.
Pia wawekezaji wanaweza kufuatilia maendeleo ya masoko ya fedha kwa kufuatilia maendeleo ya mifuko.
Mfuko mpya Hati Fungani
unaojulikana kama ‘Bond Fund’ ni kati ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja
inayoendeshwa na UTT AMIS ulioanzishwa kwa malengo maalum.
Malengo hayo ni kubuni,
kuendeleza, kuanzisha na kusimamia Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja,
kuwekeza, kununua, kumiliki na kuuza dhamana, kutimiza malengo, wajibu,
haki na sheria.
Mengine ni kutoa huduma za
usimamizi wa fedha kwa kampuni na wawekezaji binafsi, kutoa ushauri wa
uwekezaji kwa taasisi na watu binafsi, kutunza taarifa za wawekezaji wa
mifuko na kuhamasisha wananchi kujiwekea akiba.
Kuanzishwa kwa Mfuko wa Hati
Fungani kumetokana na mahitaji ya wawekezaji na uchambuzi wa bidhaa za
kifedha zilizoko kwenye soko la mitaji kwa sasa.
Mfuko utawawezesha wawekezaji
wadogo na wa kati kuzifikia fursa za uwekezaji ambazo kwa hali ya
kawaida ni wawekezaji wachache na wakubwa ndio wanaozifikia.
Pia utawekeza kwenye hati fungani
zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa kwa asilimia 90 na asilimia 10
itakuwa kwenye uwekezaji wenye ukwasi mkubwa.
Lengo ni kuwawezesha wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha kutokana na uwekezaji wao katika mfuko wafanye hivyo.
Mfuko umeundwa ili kumwezesha kila
mwekezaji kuchagua kama anapenda kukuza mtaji au kupokea gawio kwa
mwezi, kila miezi sita kutokana na mahitaji yake ya kifedha.
Sheria
ya Masoko ya Mitaji inataka Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja kuwa na
Meneja, Mdhamini, Wakaguzi wa Mahesabu, Wanasheria na Msajili.
Mfuko huo utasimamiwa na UTT AMIS
kama Meneja na Benki ya CRDB kama Mdhamini. Utakaguliwa na KPMG ambayo
ni taasisi ya kimataifa ya ukaguzi wa mahesabu ya fedha.
Wanasheria watakuwa Kampuni ya
Abenry and Company ambao wana uzoefu mkubwa katika mifuko ya uwekezaji
wa pamoja na Msajili atakuwa UTT AMIS.
Akiuzungumzia
mfuko huo, Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi Mbaga,
alisemaumelenga kuondoa changamoto ambazo wawekezaji wanakutana nazo.
Anasema soko la fedha lina bidhaa nyingi zilizobuniwa ili kukidhi mahitaji tofauti ya watumiaji.
Baadhi ya bidhaa hizo zinaeleweka
kirahisi hata namna ya kuzifikia na kuwekeza lakijni wakati mwingine
hazitoi faida shindani kwa wawekezaji.
Anasema baadhi ya wawekezaji hasa
wadogo ni vigumu kuwekeza kwenye baadhi ya bidhaa katika soko la fedha.
Mfuko wa Hati Fungani umeratibiwa ili kuondoa changamoto hizo.
Mwekezaji anapata faida sawa na
wawekezaji wakubwa, akihitaji fedha anauza baadhi ya umiliki wake kwenye
mfuko kwa utaratibu rahisi bila kupoteza faida aliyoipata.
Pia mfuko huo unawafaa wawekezaji
wakubwa kwa sababu ya faida shindani, gharama ndogo za kuwekeza, ukwasi
wa kutosha, usalama wa mtaji, hatari ndogo za uwekezaji.
Mfuko unatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza, kushiriki katika masoko ya mitaji, kufaidika na uwekezaji huo.
Kwa mantiki hiyo, mfuko
umeandaliwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa kipato cha chini, kati na
kipato cha juu ambapo watu binafsi, kampuni, taasisi na vikundi rasmi
wanaweza kushiriki katika uwekezaji kwenye mfuko huo.
Lengo kuu la mfuko ni kuwawezesha
wawekezaji katika ushiriki mpana kupitia uwekezaji wa vipande na
kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba kupitia hati fungani, masoko ya
fedha.
Mfuko huo hutoa fursa ya uwekezaji
rahisi wa muda mrefu kwa wawekezaji ambao wangependa kuwekeza ili
kukuza mtaji wao, kupata gawio kila mwezi au kila baada ya miezi sita
kama mwekezaji anavyohitaji.
Mbaga anasema, mfuko una mipango
miwili ya uwekezaji ili kukidhi matakwa tofauti ya wawekezaji. Kuna
mpango wa kukuza mtaji, gawio kila mwezi na gawio kila miezi sita,
mpango wa kukuza mtaji.
Gawio la mara kwa mara
halitatolewa kwa wawekezaji badala yake faida iliyopatikana itarudishwa
kwenye uwekezaji wa awali kwa kununua vipande vitakavyonunuliwa kwa bei
ya wakati huo.
Mpango huo utawafaa wawekezaji
wanaohitaji kuweka akiba kwa malengo maalum mfano kujenga nyumba au
wafanyakazi wenye kipato kama wangependa kuwa na fedha ya akiba.
Wawekezaji katika mpango huo
wanaweza kuuza kiasi chochote cha uwekezaji wakiwa wamekidhi vigezo
vinavyohusu uuzwaji wa vipande.
Wawekezaji wanaohitaji kuchukua
faida kila mwezi kama wastaafu wanaopata fedha zao za mkupuo, kuwekeza
kwenye mfuko, wanashauriwa kuchagua kupokea gawio kila mwezi ili wapate
kipato cha kuishi bila kupoteza fedha walizopata.
Mbaga anasema wawekezaji wengine
wanaopata fedha nyingi mara moja mfano wachimba madini, wanaweza
kuchagua gawio kila mwezi ili wafanye shughuli zao bila kuathiri mtaji
wao.
Pia wawekezaji watakao jiunga na
mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vyote ili mradi wawe
wamekidhi vigezo vya mfuko vinavyohusu uuzwaji vipande.
Mpango wa gawio kila miezi sita,
Mbaga alisema hutegemea na mahitaji ya fedha ya mwekezaji na
anavyochagua kwenye fomu ya maombi ya kuwekeza kwenye mfuko.
Kwa wawekezaji ambao wanahitaji
kuchukua faida kila miezi sita mfano wafanyakazi wanaohitaji kuweka
kiasi cha fedha ili faida inayopatikana itumike kulipa ada kusomesha
watoto, wanaweza kuchagua kupokea gawio kila miezi sita.
Pia kuna wawekezaji wanaopata
fedha nyingi mara moja kama wakulima wa mazao mbalimbali ya msimu,
wanaweza kuchagua kupata gawio kila miezi sita.
Lengo ni kupata fedha wakati wa
kutayarisha, kulima mashamba na wakati wa kuvuna ili waweze kuendesha
shughuli zao kwa kufuata msimu bila kupoteza mtaji walio nao. Pia hawa
wanahitaji pesa wakati wote huku kilimo kikiwa ni cha msimu mpka msimu.
Wakati wanasubiri msimu mpya wana chukuwa pesa za kwa mwezi ili kukidhi
mahitaji ya kila siku.
Wawekezaji watakao kujitoa
kutoka mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vipande vyote ili
mradi wawe wamekidhi vigezo vya mfuko.
Akizungumzia
sera ya uwekezaji, Mbaga anasema muundo wa mgawanyo katika mfuko wa
Hati Fungani unatoa mapato ya muda mrefu ikijumuisha hati fungani
zinazotolewa na Serikali.
Uwekezaji kwenye hati fungani ili
mfuko uwe na mapato ya kudumu utakuwa si chini ya asilimia 90 ya thamani
ya mfuko, asilimia 10 itawekezwa kwenye rasilimali zenye ukwasi ili
wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha wafanye hivyo.
Meneja atawekeza kwenye rasilimali
zenye ukwasi ili kuhakikisha uwezo wa kulipa wawekezaji pale fedha zao
zitakapohitajika unakuwa imara.
Mbaga anasema wawekezaji wote wa
ndani, nje ya Tanzania kama Sheria ya Soko la Mitaji na Dhamana
inavyoruhusu wanaweza kuwekeza kwenye mfuko huo.
Kuhusu ununuzi wa vipande, alisema
vinanunuliwa siku yoyote ya kazi isipokuwa kipindi cha kufunga vitabu
ambacho hakitazidi siku saba za kazi.
Kuanzia Septemba 16 hadi Oktoba
16, mwaka huu itakuwa kipindi cha mauzo ya awali hivyo Watanzania
wachangamkea fursa hiyo kwani kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000 na
thamani halisi ya kipande itakuwa sh. 100.
Maombi ya kununua vipande yanaweza
kuwakilishwa katika tawi lolote la Benki ya CRDB, ofisi za madalali
waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam; Ofisi za Shirika la
Posta; Wakala yoyote atakayeteuliwa na UTT AMIS.
Wawekezaji walio nje ya Tanzania
anayetaka kuwekeza katika mfuko huo awasiliane na ofisi za madalali
waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam au kuwasiliana moja kwa
moja na Ofisi za UTT AMIS ili kupata taarifa na muongozo zaidi.
Anaongeza kuwa, thamani ya mwanzo
ya kipande itakuwa sh. 100. Thamani ya kuuza na kununua kipande itakuwa
sawa na thamani halisi ya kipande bila gharama yoyote.
Kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000, hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu ambapo hiyo ni fursa kwa kila Mtanzania.
Baada ya muda wa mauzo ya awali, mwekezaji anaweza kuwekeza kuanzia sh. 5,000, mara nyingi kadri awezavyo.
Malipo ya mauzo ya vipande
yanaweza kufanywa kwa fedha taslimu au hundi ya benki itakayolipwa
kwenye akaunti ya ‘Mfuko wa Hati Fungani’ iliyopo Benki ya CRDB.
Wawekezaji wanaweza kwenda kwenye
tawi lolote la Benki ya CRDB na kufanya malipo. Pia malipo yanaweza
kufanyika kwa kupitia M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money.
Kiwango
cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa Kukuza
Mtaji ni vipande 500. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100,
thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh. 50,000.
Unaposema Mfuko wa Kukuza Mtaji
maana yake mwekezaji atakuwa anawekeza mara kwa mara kwa malengo Fulani
ili kutimiza azima fulani huko mbele. Na kila anacho wekeza kitakuwa
kinakuwa kutokana na mwenendo wa soko
Kuhusu mpango wa gawio kila mwezi,
kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa mpango wa
gawio kila mwezi ni vipande 100,000. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya
kipande ni sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh.
10,000,000.
Mpango
wa gawio kila miezi sita, kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa
mauzo ya mwanzo kwa mpango wa gawio kila miezi sita ni vipande 50,000.
Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100, thamani ya chini ya
vipande katika mauzo itakuwa sh. 5,000,000. Kuhusu
ununuzi na mauzo ya baadaye yatakayoanza Oktoba Mosi, mwaka huu, idadi
ya chini ya vipande inayoweza kuuzwa ni vipande vyenye thamani ya sh.
5,000, vitaonekana katika mgawanyo wa desimali nne.
Maombi ya mauzo, manunuzi ya vipande yatapokelewa na kukubalika siku za kazi tu.
Mauzo ya vipande yatafanyiwa kazi
baada ya kupokelewa kwa fomu ya kuuza vipande ambayo itakuwa
imeambatanishwa na taarifa ya akaunti, nakala ya kitambulisho, kielelezo
kingine kitakachohitajika na Meneja wa Mfuko.
Malipo ya mauzo ya vipande kwenda
kwa mwekezaji yatafanyika kwa njia ya benki au kupitia Shirika la Posta
ndani ya siku 10 za kazi tangu kupokelewa maombi yaliyo kamili.
Lazima mwekezaji ajaze fomu ya
maombi ya kujiunga ili aweze kununua vipande na kuwekeza, fomu hiyo
ipelekwe kwa wakala yeyote aliyeteuliwa na Meneja wa Mfuko.
No comments:
Post a Comment