Na Lilian Lundo - MAELEZO
Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere umeongeza idadi ya abiria
watakaokuwa wakihudumiwa na Uwanja huo kutoka abiria milioni 2 mpaka
abiria milioni 8 kwa mwaka. Ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa
ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Uwanja huo lenye uwezo
wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akitoa hotuba wakati wa
uzinduzi wa jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa
wa Julius Nyerere.
"Mradi huu umekamilika na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 720.
Kukamilika kwa mradi huu kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya
fedha za Serikali na nidhamu ya kutumia fedha hizo," amesema Rais
Magufuli.
Rais Magufuli amesema asilimia 100 ya fedha za ujenzi wa jengo hilo ni
fedha za Watanzania ambapo asilimia 15 imelipwa fedha taslimu na
asilimia 85 imekopwa na itarejeshwa kupitia kodi.
"Watanzania tunaweza, tunachotakiwa ni kujiamini na kuamua kufanya. Bila
kuamua Tanzania tutaendelea kuwa wategemezi katika miradi ya maendeleo
ya nchi yetu," amesema Rais Magufuli.
Aidha, ameitaja miradi mingine inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kutumia fedha za ndani kuwa ni mradi wa kufua umeme wa mto
Rufiji wenye thamani ya shilingi trilioni 6.5, daraja la Selander lenye
thamani ya shilingi bilioni 270, ujenzi wa viwanja vya ndege 15 nchini
vyenye thamani ya shilingi ya trilioni 1.868, ujenzi wa vituo vya afya
352, zahanati 30, hospitali 67 na ukarabati wa hospitali za zamani 21
wenye gharama ya shilingi bilioni 321.6 pamoja na ujenzi wa barabara wa
nchi nzima wenye jumla ya kilomita 2105 yenye gharama ya shilingi
trilioni 5.37.
Miradi mingine ni ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi katika ziwa
Victoria, barabara ya njia ya nane kutoka Kimara Dar es Salaam hadi
Kibaha, ununuzi wa rada, utanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, ununuzi wa
vifaa vya hospitali pamoja ukarabati wa shule kongwe.
Rais Magufuli amesema kuwa, heshima ya miradi yote hiyo iwaendee
Watanzania na kuwataka Watanzania kulifuta kabisa neno la kujiita
masikini kwani Tanzania ni nchi tajiri.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi
Isack Kamwelwe amesema Jengo la pili la abiria nalo linahitaji
kukarabatiwa na kuongezwa uwezo wa kubeba abiria mara mbili ya sasa,
ambapo kwa sasa lina uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
Mhandisi Julius Ndyamukama amesema taasisi yake imeshahamishia shughuli
za uendeshaji wa ndege katika Jengo hilo kutoka Jengo la abiria la pili.
Vile vile amesema, jumla ya vijana 130 kati ya vijana 241 waliokuwa
wanahitajika wameajiriwa, ambapo kwa sasa wapo katika mafunzo ya nafasi
walizopangiwa kufanya kazi.
Vile vile Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patric Mfugale amesema
ujenzi wa jengo la abiria la kwanza ulijengwa mwaka 1956 ambapo unauwezo
wa kuhudumia abiria laki 5 kwa mwaka. Mwaka 1984 ilikamilisha ujenzi wa
jengo la tatu la abiria ambalo linauwezo wa kuhudumia abiria milioni
1.5 kwa mwaka.
Amesema baada ya kuonekana jengo la pili la abiria kutotosheleza abiria
wanaohudumiwa uwanjani hapo, ndipo Serikali ilipoamua kuanza ujenzi wa
jengo la tatu la abiria, ambalo ni jengo la kisasa zaidi ukilinganisha
na majengo yote ya abiria hapa nchini.
No comments:
Post a Comment