Rais
wa Iran Hassan Rouhani amesema leo kuwa uamuzi wa Marekani kumuekea
vikwazo Mohammed Javad Zarif inaonyesha kuwa Marekani inamuogopa
mwanadiplomasia huyo mkuu.
Katika hotuba ya moja kwa moja ya televisheni, Rouhani amesema Marekani
wanaogopa mahojiano yanayofanywa na waziri wa Iran wa mambo ya nchi za
kigeni. Akimaanisha mahojiano ya karibuni aliyoyafanya Zarif na vyombo
vya habari vya kigeni mjini New York.
Rouhani amesema wakati akiwa ziarani katika mji wa kaskazini magharibi
wa Tabriz kuwa uamuzi huo wa Marekani ni wa "kitoto” na kizuizi kwa
diplomasia. Utawala wa Trump umemuwekea vikwazo Javad Zarif, na hivyo
kumfungia kabisa mlango mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.
Vikwazo hivyo vinazuia mali zozote za Zarif nchini Marekani au
zinazodhibitiwa na makampuni ya Marekani. Serikali ya Washington imesema
hatua hiyo itadhibiti safari zake za kimataifa.
Taarifa ya Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin imesema kuwa Zarif
anatekeleza ajenda hatari ya kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali
Khamenei, na yeye ndiye msemaji mkuu wa utawala wa Iran kote duniani.
Marekani inatuma ujumbe wa wazi kwa utawala wa Iran kuwa tabia yake ya
karibuni haikubaliki kamwe.
Zarif alijibu maramoja akiandika kwenye Twitter kuwa Marekani inajaribu
kumyanyamazisha kwenye jukwaa la kimataifa. Akasema vikwazo alivyowekewa
havitakuwa na athari yoyote kwake wala familia yake kwa sababu hana
mali wala maslahi yoyote nje ya Iran.
Lakini katika ujumbe mwingine wa kukanganya kwa Tehran, Marekani
imerefusha kwa siku 90, msamaha wake kwa miradi mitatu ya nyuklia kwa
matumizi ya kiraia ili kuepuka kuzikasirisha nchi nyingine zilizosaini
makubaliano ya nyuklia ya 2015, ambazo ni China, Urusi, Ujerumani,
Ufaransa na Uingereza.
Akizungumza jana, Zarif alisema Iran iko tayari kupunguza ahadi zake za
mkataba wa nyuklia, kama washirika wa Ulaya hawatoilinda dhidi ya
vikwazo vya Marekani kwa kuhakikisha kuwa inaweza kuuza mafuta na
kupokea mapato.
Mbali na kujaribu kutwaa mali zake, Marekani pia itauminya uwezo wa
Zarif kusafiri kimataifa kama mwanadiplomasia. Anatarajiwa kuendelea
kuzuru Umoja wa Mataifa mjini New York, ijapokuwa chini ya udhibiti
mkali.
No comments:
Post a Comment