Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akimkabidhi Ngao Omar Mwinyikondo Mkurugenzi Utumishi na Uendeshaji Wizara ya Afya ikiwa mojawapo ya Waajiri wachangiaji Bora wa ZSSF wakati wa mojawapo wa Mkutano Mkuu wa Wanachama na Wadau wa Mfuko huo.[ katikati]ni Mwenyekti wa Bodi ya ZSSF Dkt.Suleiman Rashid.
Na Christian Gaya
Majira Ijumaa 30. Agosti. 2019 www.majira.co.tz
Mojawapo ya wajibu wa mifuko
ni kuhakikisha ya kuwa inawashirikisha wanachama na wadau wake wote wakuu hasa wanachama,
waajiri, na serikali ambaye ndiye mdhamini mkuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii,
ambapo makundi hayo matatu yanaunda kitu kinachoitwa utatu.
Ni haki na wajibu wa wanachama
na wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii kufuatilia na kujua utendaji wa mifuko
hii inayosimamiwa na bodi za wadhamini kwa njia ya mikutano mikuu inayofanyika
kila mwaka, kwa vile wana haki ya kujua maamuzi muhimu yaliyoamuliwa.
Mipango ya hifadhi ya jamii ni ya lazima kisheria
ambayo mfanyakazi pamoja na mwajiri wanachangia pamoja na mwajiri kutakiwa
kuwakilisha michango hiyo kwenye chombo cha mfuko wa hifadhi ya jamii, ingawa
pamoja na hayo pia inatoa mipango mengine ya hifadhi ya jamii kwa mfumo wa
hiari kama mafao ya ziada kwa wanachama.
Kwa mujibu wa sheria za
hifadhi ya jamii, uwakilishi wao lazima unatakiwa kuwemo ndani ya utawala wa
mifuko hii ya hifadhi ya jamii mara kwa mara kwa vitendo na kwa kuwakumbusha
wajibu na haki za wanachama.
Njia nyingine ya
kuwashirikisha wanachama na wadau wa mifuko ni kwa kutumia mkutano wa
mwaka ambapo wawakilishi kutoka kwa
waajiri, wanachama, serikalini na wadau wengine hukutana pamoja kujadili juu ya
uendeshaji na afya mfuko kwa ujumla.
Kisheria
mfanyakazi ana wajibu wa kuelewa haki, wajibu, na taratibu za kupata huduma
bora kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii. Pia ana haki ya kupata elimu ya hifadhi
ya jamii bila ya kujali ni mfanyakazi ni mtumishi wa umma, anatoka sekta rasmi au
sekta isiyokuwa rasmi ikiwezekana hata kabla ya zoezi la uandikishaji kufanyika.
Ambapo
mwajiriwa akisha andikishwa anapaswa kupata kadi ya uanachama yenye namba ya
uanachama ambapo mwanachama hupaswa kupokea kadi hiyo ndani ya siku 90 tangu
uanachama kuanza. Kadi ni mali ya mwajiriwa siyo ya Mwajiri na mwajiri
haruhusiwi kutunza kadi ya mwanachama. Anayeyeruhusiwa kutunza kadi ya
uanachama ni mwajiriwa yaani mfanyakazi mwenyewe na siyo vinginevyo.
Wakati inapotokea
mabadiliko yoyote kuhusu taarifa za mwajiriwa au mwajiri, inakuwa ni wajibu wa
mwajiri kutoa taarifa kwa mfuko husika ndani ya siku 30 ya mabadiliko
hayo. Mwajiri pia ana wajibu inapotokea
mwajiriwa anaacha kazi au ajira kwisha kwa sababu zozote kuwasiliana na mfuko
husika na kutoa taarifa hiyo kwa barua.
Wajibu mwingine wa
mwajiri mpya ni kuhakikisha anatoa taarifa kwa mfuko husika kuhusu mwanachama
ambaye ni mwajiriwa mpya, ili kuhakikisha ya panakuwepo usahihi wa taarifa za
wanachama.
Mfuko una wajibu wa
kuandikisha wanachama, kukusanya michango kutoka kwa wanachama, kuwekeza
michango ya wanachama, na kulipa mafao kwa wanachama. Mfuko wa hifadhi ya jamii
una wajibu wa kuwaelimisha wanachama na waajiri juu ya mahitaji yote ya mfuko,
na kuwaelekeza jinsi ya kujaza fomu mbalimbali.
Waajiri wanaohusika kisheria kuandikishwa katika mfumo huu
wa hifadhi jamii ni waajiri wote walio katika sekta binafsi, na sekta
sizizorasmi, taasisi zisizokuwa za kiserikali, ofisi za kibalozi zinazoajiri
watanzania, taasisi za kimataifa zinazofanya shughuli ndani ya Jamuhuri ya
muungano wa Tanzania,
Zingine ni pamoja na taasisi za wizara za serikali
zinazoajiri wafanyakazi kwa masharti ya muda, mashirika ya umma yanayoajiri
wafanyakazi kwa masharti ya muda na kwa watumishi wa umma kwa ujumla.
Watu binafsi waliojiajiri wenyewe, sehemu yoyote ya shughuli
kama mwajiri mlipa michango pia wanatakiwa kujiandikisha kisheria na kuwa
waajiri wachangiaji mara tu anapoanza shughuli zao.
Mfuko una wajibu wa
kuelimisha wanachama juu ya mafao wanayotakiwa kupata kutoka kwenye mifuko hiyo
na ni lini kuipata hayo mafao, na jinsi yakufungua hayo mafao au madai na
kuhakikisha kuwa malalamiko ya wanachama kutoka kwa waajiri na wanachama
yanasikilizwa na kuchukuliwa hatua mara moja kwa kuyafanyia kazi.
Kwa upande mwingine
mfuko una wajibu wa kuweka uhusiano mkubwa sana kati ya mfuko na wanachama na
pale wanachama wanapogundua kuwa waajiri wao hawajapeleka michango kwenye
mifuko, wanatakiwa kutoa taarifa kwenye mifuko hasa pale kwenye ofisi
walizokuwa karibu nazo.
Pia wafanyakazi
wanashauriwa kutokuwa na mashaka yoyote kutoa taarifa kwenye mifuko kwa waajiri
wanaokwenda kinyume au wasio watendea haki wafanyakazi wao juu ya mambo yanayo
husiana na michango.
Mfanyakazi akitoa
taarifa ya kwenye mifuko inatakiwa itunzwe kama siri kwa ajili ya kumlinda
mfanyakazi na taarifa inapotolewa mapema inafanyiwa kazi mapema inasaidia
kurekebisha matatizo ya mchangiaji kutatuliwa mapema na kwa haraka.
Ni wajibu wa waajiri na
wafanyakazi kutoa hizo taarifa mapema wakati wako kazini, wasingojee mpaka
waache kazi, au waachishwe kazi, kwa kufanya hivyo, wakati mwingine inakuwa ni
vigumu kutatua matatizo yanayo mkabili, wakati yuko nje ya ajira.
Mwanachama ana haki ya kupewa
kitambulisho cha uanachama ambacho kinatumika kwa ajili ya kupata mafao na
huduma yoyote nyingine kutoka katika mfuko wowote aliojiandikisha nao.
Vilevile ni haki ya mfanyakazi
yaani mwanachama kupata taarifa ya michango yake anayokatwa kila mwezi. Waajiri
pia wana wajibu wa kutunza kumbukumbu zote za malipo ili kuwezesha mifuko,
inapofanya ukaguzi iwe rahisi kupata kumbukumbu hizo.
Mwajiri yeyote anawajibika
kujiandikisha katika mfuko kama mlipa michango na kupewa namba ya uandikishaji
mara tu anapoanza shughuli zake. Mwajiri yeyote awajibika kuwaandikisha
wafanyakazi wote alionao na kupewa namba za uanachama ambazo ni lazima kwa mwanachama
kutunza namba hiyo.
Wafanyakazi pia wanajibu wa
kuhakikisha kuwa michango yao iliyokatwa na waajiri iko sahihi na pale
wanapoona ya kuwa wana wasiwasi na waajiri juu ya michango yao iliyokatwa,
ambayo sio sahihi wanatakiwa kutoa taarifa kwenye mifuko iliyo karibu kwa
ushauri zaidi.
Pia ni wajibu wa mifuko
kuchukua hatua za kisheria mapema kwa waajiri ambao hawataki kupeleka michango
kwa wakati muafaka, na wale waajiri wanaokataa kuwaandikisha wafanyakazi wao
kwenye hii ya mifuko ya hifadhi ya jamii.
No comments:
Post a Comment