Pages

Friday, July 26, 2019

Fahamu chimbuko la hifadhi ya jamii, umuhimu wake-II


 
Majengopacha ya mfuko wa PSSSF ambayo ni mojawapo ya vitegauchumi vya hifadhi ya jamii vinavyotokana na michango ya wanachama. (Na mpigapicha Wetu)

Na Christian Gaya, gayagmc@yahoo.com:           Majira Ijumaa 26.Julai.2018.
WIKI iliyopita tuliona ya kuwa hifadhi ya jamii ina maana ni aina ya hatua madhubuti au mfuko uliobuniwa kama vile wa PSSSF ambao ni kwa ajili ya watumishi wa umma wa kuhakikisha ya kuwa wananchi wa jamii hiyo wanapata mahitaji yao ya lazima na ya msingi na wanapewa kinga ya hifadhi ya kutokana na majanga ili kuwawezesha kuwa na kiwango cha...
maisha ya kuishi kulingana na mila na desturi za jamii.
Majanga hayo ni kama; “uzee, ulemavu, kifo, ugonjwa, gharama za matibabu, kuumia kazini, uzazi, ukosefu wa ajira na ukubwa wa familia” 
Hivyo lengo kubwa la hifadhi ya jamii ni kuzuia umasikini, kupunguza au kuondoa kabisa umasikini, kuifidia jamii, kugawanya mapato sawasawa kwa wanajamii. Masuala mengi yanayogusa hifadhi ya jamii ni ya nyeti sana, yanagusa ni kiini muhimu sana cha wafanyakazi kwenye sekta rasmi na sekta zisizo rasmi. 
Tunachangia pamoja kwa kuweka kwenye chungu kimoja, kwa mshikamano mmoja, na kukabiliana na aina ya majanga ya aina mbalimbali yanayojitokeza miongoni mwetu. Mwenzetu yeyote akipatwa na janga lolote gharama za matibabu au kuumia na kupatwa na ulemavu zitachotwa kutoka katika kapu au chungu hicho hicho bila kujali amechangia uwingi wa kiasi gani wa michango. 
Lengo kubwa la hifadhi ya jamii ni kujaribu kugawanya mapato sawasawa kwa jamii kwa wale wa pato la juu na chini. Na wala siyo kumtajirisha mtu, hifadhi ya jamii siyo kuleta mgawanyo wa tabaka la juu na la chini, siyo michango ya mtu wa chini kutumika kumunufaisha mtu wa kipato juu kwa kupata pensheni kubwa zaidi kuliko kundi lingine katika jamii.

Kwa mujibu wa shirika la kazi duniani (ILO) hifadhi ya jamii ni mfumo ambao jamii husika imejiwekea kwa lengo ya kujikinga dhidi ya matukio yasiyotarajiwa.  

Hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu na ndiyo maana haki hii imeanzishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 11(1) na sera ya Taifa ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2003.

Haki hii pia imeiainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka 1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi duniani (ILO) ibara ya 102 ya mwaka 1952.
Kwa sababu sekta isiyo rasmi na mfumo wa hifadhi ya jamii wa asili unaotolewa kwenye ngazi ya familia unazidi kupungua na kuwa dhaifu siku hadi siku. Kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya kiuchumi na kijamii, familia nyingi zinajitosa tu kwa ajili ya baba, mke na watoto wao tu.
Hii inaashiria ya kuwa mfumo wa kukabidhiwa kulea familia zaidi ya moja imekuwa ngumu kwa karibu familia nyingi hapa duniani. Tofauti na huko nyuma ambapo mtu aliweza kukabidhiwa familia zaidi ya moja ili kuwapa kinga ya dhidi ya majanga.  Na ushahidi unaonesha kabisa ya kuwa mpaka sasa tunavyozungumzia mambo haya, utafiti unaonesha ya kuwa familia moja ya baba na mama zimeanza kushindwa hata kukabili majanga hatarishi ya familia.
Na kadiri tunavyo kuwa wazee na kufanya kazi, na kuzalisha na kipato chetu pia kinazidi kuwa kidogo zaidi na hivyo basi tunahitaji kupata kipato kutoka sehemu nyingine ili kuhakikisha ya kuwa tunaendeleza maisha yetu baada ya kustaafu au kupatwa na aina yeyote ya janga hatarishi.
Jamii na serikali mbalimbali za hapa Afrika ikiwemo nchi yetu ya Tanzania na za huko ulaya wameweza kuwa na vyombo mbalimbali kwa ajili kuwapa kinga ya hifadhi ya jamii. Ikiwemo hifadhi ya jamii inayotolewa na serikali kwa kutumia kodi za wananchi, kwa ajili ya kupunguza umaskini hasa kwenye kaya maskini.
Na kukinga majanga ya asili kama vile mafuriko na ukame. Haya maafa yote yanayotokea nchini hugharimiwa na kushughulikiwa na serikali yenyewe yakiwemo pamoja na mambo ya ustawi wa jamii kwa ujumla.
Na aina ya pili ya mfumo wa hifadhi ya jamii ni ule ambao huchangiwa na waajiri na wafanyakazi wao sehemu za kazi. Mfumo huu ni wa kisheria ili upate kutekelezwa. Mara nyingi watu wamekuwa wagumu sana kuchangia kwa ajili ya matukio hatarishi ya yanayoweza kutokea siku za mbeleni, watu wanaangalia kwa ajili ya mahitaji ya haraka ya leo tu.
Kwa hapa Tanzania kulingana na sheria ya mfuko wa PSSSF namba 2 ya mwaka 2018 mfanyakazi ambaye ni mwanachama wa mfuko hukatwa asilimia 5 ya jumla ya mapato yake yote kwa mwezi na mwajiri analazimika huchangia asilimia 15 ya mshahara wa mfanyakazi hivyo na kufanya kuwa jumla ya asilimia 20 na yote hupelekwa kwenye akaunti ya mwanachama wa mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii. PSSSF ni mfuko wa hifadhi ya jamii kwa ajili ya wafanyakazi wa umma.
Ambapo kuanzia Agosti Mosi, 2018, waliokuwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa yaani PPF, PSPF, LAPF, na GEPF waliohamishiwa katika mfuko wa PSSSF wataendelea kuwa wanachama na kuchangia katika mfuko wa PSSSF.
Wakati kulingana na sheria ya NSSF mfanyakazi ambaye ni mwanachama wa mfuko wa pensheni, hukatwa asilimia 10 ya jumla ya mapato yake yote kwa mwezi na mwajiri analazimika huchangia asilimia 10 ya mapato yote ya mshahara wa mfanyakazi hivyo na kufanya kuwa jumla ya asilimia 20 na yote hupelekwa kwenye akaunti ya mwanachama wa mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii.
Au mwajiri huweza kuchangia asilimia 15 na mwajiriwa asilimia 5 au asilimia yote 20 inaweza kutolewa na mwajiri kwa mfanyakazi wake kulingana na makubaliano kama sehemu ya motisha kwa mfanyakazi wake. Ambapo mfuko huu wa NSSF ni kwa ajili ya wafanyakazi kutoka katika sekta binafsi na sekta zisizorasmi.
Na mfumo wa mwisho wa hifadhi ya jamii ni mtindo wa kuchangia kwa hiyari. Mpango huu wa hiari ni mahususi kwa ajili ya kuwapatia huduma ya hifadhi ya jamii wale wote ambao awali kutokana na matakwa ya kisheria hawakuweza kujiunga na mifuko ya hifadhi ya Jamii.
Watanzania wote wanatakiwa wachukue fursa hii kujiwekea akiba ya ziada hata kwa wale ambao tayari wamo katika mifuko mingine wa hifadhi ya jamii hii itawasaidia kujiongezea na kutunisha na hivyo kunufaika na mafao ya muda mrefu na ya muda mfupi wakati wanapoendelea kufanya kazi na baada ya kustaafu.

No comments:

Post a Comment