Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Profesa Adelardus Kilangi akisisitiza kwa Baraza la Uongozi la TLS
likiogozwa na Rais wake Dk. Rugemeleza Nshala kwamba Serikali
itashirikiana na TLS,Wakati Baraza hilo lilipomtembelea na kufanya
mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ofisini kwake Mitumba-
Ihumwa Jijini Dodoma. Mazungumzo hayo yalifanyika jana alhamisi.
Ujumbe wa Baraza la Uongozi la
TLS wakiwa katika mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baadhi ya
mambo yaliyojadiliwa ni kuhusu namna bora ya kuhakikisha sheria ambazo
zimefanyiwa urekebu na baada ya kupitishwa na Bunge zinawafikia wadau
kwa wakati. Pia walijadiliana kuhusu haja na umuhimu wa kuzifanyia
urekebu wa baadhi ya sheria zenye changamoto.
…………………………
Na Mwandishi Maalum- Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Profesa Adelardus Kilangi, amesema, Serikali inatambua mchango wa Chama
cha Mawakili wa Tanganyika ( TLS) katika kuimarisha na kudumisha
Utawala wa Sheria nchini.
Akasema wakati wote Serikali ipo
tayari kupokea maoni na ushauri kutoka TLS ilimradi kwamba, maoni au
ushauri huo unajikita katika kujenga, kuimarisha, hauegemei upande
wowote, wenye staha na usio na mashinikizo.
“ Kwanza niwashukuru sana kwa kuja
kukutana na kufanya mazungumzo nami, niwapongeze wewe Rais kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa TLS pamoja na wote mliochaguliwa katika baraza
la uongozi. Ni matumaini yangu kwamba, hamtawaangusha wanachama wenu
waliowachagua, msiwaagushe tafadhali” Akasema Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na kuongeza
“Wakati wote Serikali imekuwa
ikithamini sana mchango wenu na maoni yenu. Na kwa kweli mmekuwa mkitoa
mchango na maoni mazuri sana, niwahakikishe kwamba Serikali wakati wote
ipo tayari kushirikiana nanyi. Jambo la muhimu ni kuwa na majadiliano (
dialogue) pale ambapo mnaona kunajambo la kujadiliana kabla ya kulitolea matamko.
“Niwahakikishe kwamba, Serikali
kwa ujumla na hasa Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika uongozi wake
anapenda sana Sheria na anataka mambo yafanyike kisheria na kwa
kuzingatia sheria ” akasisitiza Profesa Kilangi
Profesa Kilangi ameyasema hayo
wakati alipokutana na kufanya mazungumza na ujumbe wa Balaza la Uongozi
la TLS likiongozwa na Rais wake Dk. Rugemeleza Nshala.
Mazungumzo kati ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali na Ujumbe wa Balaza la Uongozi yaliyochukua zaidi ya
masaa matatu, yalifanyika siku ya Alhamisi katika ukumbi wa Mikutano wa
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mitumba- Ihumwa Jijini Dodoma.
“Niwaombe sana katika uongozi wenu
msimamie sana weledi wa tasnia ya Sheria, hili nawaomba sana, sisi
sote ni maofisa wa Mahakama, ni katika mkutadha huu tunatakiwa
kutekeleza majukumu yetu ya uofisa Mahakama kwa welidi wa hali ya juu
sana na kwa kuzingiatia misingi na maadili ya kazi zetu. Lisimamieni
sana hili, simamie professionalism” akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Rais wa TLS Dk, Rugemeleza Nshala
pamoja na kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwakubalia
ombi lao na kukutana nao. Alisema kuna mambo kadhaa ambayo walitamani
au waliona ni vema wakabilishana naye mawazo.
Dk Nshala aliyataja baadhi ya
mambo hayo kuwa ni pamoja na kuangalia namna bora itakayowawezesha TLS
na wadau wengine wa Sheria nchini, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya kushirikiana katika kuhakikisha kwamba Mawakili wa
kujitegemea na Mawakili wa Serikali wanatekeleza majukumu yao kwa weledi
na kwa kuzingatia maadili na miiko ya kazi zao.
Jambo jingine ambalo Dk. Nshala
kwa niaba ya jumbe wake aliliwasilisha kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ni la namna ya kuangalia jinsi ya kuifanyia marekebisho baadhi
ya vifungu vya Sheria ya TLS hasa katika kifungu cha uchaguzi wa
Viongozi unaotakiwa kufanyika kila mwaka.
“Katika mkutano wetu wa Arusha
wanachama tulilijadili hili la uchaguzi wa kila mwaka, ni hitajio la
kisheria lakini gharama za kukutana kila mwaka ni kubwa sana na
zinabebwa na wanachama, hivyo tulijadiliana kuona namna gani tunaweza
kuliboresha hili kwa kujadiliana na wadau wengine na kwa kuangalia
mifano ya nchi nyingne akasema “ Rais wa TLS.
Dk. Nshala pia alizungumzia
kuhusu mitaala ya mafunzo Sheria katika Vyuo Vikuu na kushauri kwamba
wadau wa Sheria wanapashwa kukaa na kujadiliana namna bora ya
kuuboresha ili iendane na wakati.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa TLS
amesema kwa uzoefu wake na katika utekelezaji wa majukumu yake kuna
mifano hai ya mapungufu ya kiutendaji kwa kwa baadhi ya mawakili
ambayo mengi kati ya hayo ni ukosefu wa mafunzo Stahiki
Katika hilo la uboreshaji wa
mfumo wa ufundishaji, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema anakubaliana
nalo kwa asilimia kubwa, na kwamba , tatizo ambalo yeye analiona ndiyo
changamoto kubwa katika tasnia ya Sheria ni mafunzo kwa vitendo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Profesa Kilangi na Uongozi wa TLS walijadili pia kuhusu namna bora ya
kuhakikisha kwamba Sheria zinazofanyiwa urekebu na mara zikisha
pitishwa na Bunge Ofisi ya Mwanasheria Mkuu isisambaze ili zinawafikia
wadau kwa wakati.
Vile vile walibadilishana mawazo
kuhusu haja na umuhimu wa kuzifanyia urekebu baadhi ya Sheria ambazo
zinamatatizo au changamoto katika utekelezaji wake. Baadhi ya Sheria
hizo ni pamoja na baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jinai na Sheria ya
Usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama.
Walibadilishana mawazo pia kuhusu
mazingira ya utendaji kazi wa Mawakili hasa mawakili wa kujitegemea
ambao Dk. Nshala alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
zinazopashwa kutafutiwa ufumbuzi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Evaristo Longopa na Mkurugenzi
wa Idara ya Uratibu na Utoaji wa Huduma Dk. Gift Kweka.
No comments:
Post a Comment