Waziri wa Madini Nchini Uganda,
Peter Lokeris na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus
Nyongo (katikati) wakiangalia namna kifusi cha mchanga kinavyotolewa
kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Blue Creef uliopo Wilayani Geita Mkoani
Geita unaomilikiwa na Christopher Kadeo tarehe 02 Aprili, 2019
Waziri wa Madini Nchini Uganda,
Peter Lokeris (wa pili kulia) akifafanua jambo kwenye Mgodi wa Dhahabu
wa Blue Reef uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita unaomilikiwa na
Christopher Kadeo mara baada ya yeye pamoja na ujumbe wake kufanya ziara
kwenye mgodi huo. Katikati ni Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania,
Stanslaus Nyongo.
Mkurugenzi wa kampuni ya
Tan-Discover Mineral Consultancy Co. Ltd, Peter Kaheshi (kushoto) akitoa
ufafanuzi kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (kulia)
mara baada ya yeye pamoja na ujumbe wake kufanya ziara katika kituo cha
mfano cha Rwamgaza kwa ajili ya kutoa mafunzo ya namna bora ya uchimbaji
na uchenjuaji wa madini kilichopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani
Geita Mkoani Geita.
Mtaalam kutoka Mgodi wa Dhahabu wa
Busolwa uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita, Felix Adolf Ishebabi
(katikati) akielezea shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu
zinavyofanywa na mgodi huo kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter
Lokeris, Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo pamoja
na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania kwenye ziara hiyo.
Afisa Migodi Mkazi wa Mkoa wa
Geita, Ernest Maganga (kulia) akielezea namna biashara ya madini
inavyofanyika kwenye Soko la Madini la Geita kwa Waziri wa Madini Nchini
Uganda, Peter Lokeris (kushoto) na Waziri wa Madini Nchini Tanzania,
Stanslaus Nyongo (katikati) pamoja na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania
kwenye ziara hiyo
……………..
Na Greyson Mwase, Geita
Waziri wa Madini Nchini Uganda,
Peter Lokeris ames ema kuwa amefurahishwa na usimamizi wa sekta ya
madini nchini Tanzania na kusisitiza kuwa Uganda bado itaendelea kutuma
wataalam wake pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania kwa
ajili ya
kujifunza namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Lokeris aliyasema hayo jana
tarehe 02 Aprili, 2019 mara baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji
wadogo na wa kati ya madini iliyopo Wilayani Geita Mkoani Geita, ikiwa
ni sehemu ya ziara yake ya siku nne nchini Tanzania yenye lengo la
kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika Sekta ya Madini kupitia
Wizara ya Madini hususan katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.
Akiwa ameongozana na ujumbe
wa maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa
wachimbaji wadogo aliwasili mkoani Geita na kupokelewa na Kaimu Mkuu wa
Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita pamoja na Naibu
Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.
Ziara hiyo pia ilihusisha
wataalam kutoka Wizara ya Madini. Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi na
usalama vya mkoa pamoja na waandishi wa habari.
Akielezea hali iliyopelekea
nchi ya Uganda kuichagua nchi ya Tanzania kama sehemu ya kujifunza
kuhusu Sekta ya Madini, Lokeris alisema kuwa, baada ya kutanya utafiti
katika nchi za Aftika Mashariki, walibaini kuwa nchi ya Tanzania ni nchi
iliyopiga hatua kubwa kwenye usimamizi wa sheria na kanuni za madini
hali iliyopelekea wananchi wengi kunufaika nayo hususan wachimbaji
wadogo wa madini.
Aliendelea kusema kuwa, Sekta
ya Madini Nchini Uganda ndio inaanza kukua, hivyo wameona ni vyema kuja
Tanzania kwa ajili ya kujifunza na kwenda kuimarisha Sekta ya Madini
ili baada ya miaka kadhaa angalau iwe inakaribiana na nchi ya Tanzania.
Akielezea mikakati ya matumizi
ya uzoefu mkubwa ujumbe huo ilioupata kutoka kwa nchi ya Tanzania,
Waziri Lokeris alisema hatua ya kwanza itakayofanywa na Serikali ya
Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhamasisha wachimbaji wadogo
wa madini kuunda vikundi na kuwapatia leseni.
Aliongeza kuwa, mara baada ya
kuwapatia leseni hatua itakayofuata itakuwa ni kuwaleta Tanzania kwa
ajili ya mafunzo ambapo watajifunza kupitia wachimbaji wadogo wa madini
wa Tanzania waliofanikiwa kwenye shugfhuli za uchimbaji na uchenjuaji wa
madini.
Aliendelea kueleza kuwa, nia
ya Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhakikisha sekta
hiyo inakua kwa kasi na kuanza kuzalisha dhahabu na kuuza nyingine nje
ya nchi na kujipatia mapato makubwa.
“Tumefurahishwa na usimamizi
mzuri kwenye sekta ya madini hususan kwenye eneo la uwezeshaji wa
wachimbaji wadogo, tumeona namna wanavyochenjua madini huku wakizingatia
sheria na kanuni za mazingira,”alisisitiza Waziri Lokeris.
Naye Naibu Waziri wa Madini
Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo akielezea mafanikio ya sekta ya madini
nchini alieleza kuwa, mafaniko yaliyopatikana ni pamoja na uboreshaji
wa sheria mpya ya madini pamoja na kanuni zake inayotambua madini kama
mali ya watanzania na kusisitiza kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa
wanufaika kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kuwa, Serikali
kupitia Wizara ya Madini imeondoa tozo mbalimbali zisizo za lazima hali
iliyopelekea wachimbaji wadogo kuzalisha madini kwa gharama nafuu na
kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.
Alieleza mafanikio mengine
kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko nchini kama njia mojawapo ya
kudhibiti utoroshwaji wa madini kwa kuhakikisha wachimbaji wa madini
wanakuwa na soko la uhakika la kuuzia madini yao kwa bei yenye faida.
Naye mmiliki wa mgodi wa
dhahabu wa Blue Reef uliopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani Geita
mkoani Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji wa Madini
Mkoa wa Geita (GEREMA), Christopher Kadeo akizungumza na ujumbe huo
uliofanya ziara kwenye mgodi wake akielezea mchango wa mgodi wake katika
jamii iliyopo jirani alisema mgodi wake tangu ulipoanzishwa mwaka 1991
mpaka sasa umefanikiwa kuajiri watumishi 160 na vibarua takribani 200.
Alieleza mafanikio mengine
kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu,
ulinzi kupitia ujenzi wa vituo vya polisi na kusisitiza kuwa mgodi
umekuwa ukishirikiana kwa karibu zaidi na Tasisi nyingine za Serikali
kama vile Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma
(MRI), Chuo Cha Ufundi Dar es Salaam (DIT), Wizara ya Madini, Tume ya
Madini na mashirika mengine ya kimataifa.
Aidha, aliongeza kuwa mgodi
wake umewahi kupewa tuzo ya utunzaji bora wa mazingira na Rais wa Awamu
ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Akielezea mikakati ya mgodi
wake kwenye shughuli za uchimbaji wa madini alisema mgodi wake
unatarajia kufanya utafiti zaidi ili kugundua madini zaidi na
kuunganisha leseni zake tano unazomiliki na kutoka kwenye uchimbaji wa
kati hadi mkubwa.
No comments:
Post a Comment