Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na waandishi wa habari Jijini
Dodoma kuhusu Ukaguzi wa Maduka ya kubadilisha Fedha za Kigeni ambapo
alisema lengo lake sio kufuta biashara ya maduka hayo bali ni kudhibiti
ukiukwaji washeria uliokithiri na utakasishaji wa Fedha haramu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) Prof. Florens Luoga, akieleza kuwa jumla ya maduka 87 yamefanyiwa
ukaguzi Jijini Dar es Salaam na ni maduka matano pekee ndio yamebainika
kutokiuka sheria, wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), na waandishi wa habari katika ukumbi
wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango
Bw. Benny Mwaipaja (kushoto), wakiwa katika Mkutano na Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ambapo Waziri huyo
alisema hakuna mmliki wa Duka la Kubadilisha Fedha ambaye amewasilisha
malalamiko yoyote kwa mamlaka husika kuhusu zoezi la ukaguzi wa maduka
hayo.
Mwandishi wa Habari wa Gazeti la
Mwananchi, Sharon Sauwa, akiuliza swali kuhusu kufungwa kwa maduka ya
kubadilisha fedha za kigeni wakati wa Mkutano kati ya waandishi wa
habari na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
(Mb), (hayupo pichani) kuhusu ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za
kigeni, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akifafanua jambo wakati wa mkutano kati
yake na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango
Jijini Dodoma. Kulia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof.
Florens Luoga, na kushoto ni Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Kamishna wa Sera
wa Wizara hiyo Bw. Mgonya Benedicto
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
Prof. Florens Luoga, wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika
ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
(Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)
……………………….
Katika kutekeleza majukumu yake ya
kuhakikisha kuwa Sekta ya Fedha inachangia ipasavyo utulivu na ukuaji
wa uchumi nchini, Benki Kuu ya Tanzania ilibaini uwepo wa maduka ya
kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalikuwa yakiendeshwa pasipo
kuzingatia Sheria ya Foreign Exchange Act 1992, Kanuni za The Foreign Exchange (Bureau de Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017
na Taratibu za utoaji wa huduma za ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Kufuatia hali hiyo, zoezi maalum la ukaguzi wa kina kwa maduka hayo
lilifanyika Arusha Novemba 2018 na kwa Dar es Salaam siku ya tarehe 27
Februari 2019, 1 na 8 Machi 2019 kwa kuhusisha vyombo vya Dola na
kubaini ukwepaji mkubwa wa kodi na uvunjaji wa Sheria.
Zoezi hili limebaini pia
uondoshwaji wa fedha katika mfumo rasmi wa fedha na kuelekezwa kwenye
mifumo ya utakasishaji wa fedha haramu, kupokea Amana kutoka kwa
wafanyabiashara kinyume cha matakwa ya leseni za biashara husika,
kudhoofisha thamani ya shilingi, pamoja na mambo mengine ambayo yalianza
kuathiri usalama wa nchi kwa ujumla. Kwa mfano, baadhi ya maduka
yaligundulika kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za kigeni
lakini fedha kidogo za kigeni ziliuzwa na hakuna taarifa ya matumizi ya
fedha za kigeni zilizobaki.
Ni vizuri ieleweke kuwa, zoezi la
ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni lilitekelezwa kwa
kuzingatia Sheria za nchi tofauti na malalamiko na tuhuma mbalimbali
zilizotolewa za kudai uwepo wa ukiukwaji wa Sheria na haki kwa wamiliki
wa maduka hayo. Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mmiliki yeyote wa
duka aliyewasilisha malalamiko kuhusiana na zoezi hili kwenye mamlaka
husika. Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka nyingine za
Serikali zinafuatilia kwa umakini ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo
zinazotolewa.
Serikali ya Awamu ya Tano
inatekeleza majukumu yake kwa umakini. Hivyo, Serikali inauthibitishia
umma wa Watanzania kuwa katika zoezi la ukaguzi wa Maduka ya Kubadilisha
Fedha za Kigeni hakuna fedha au mali yeyote iliyotaifishwa. Taratibu za
kisheria zilifuatwa wakati wa kuchukua vielelezo mbalimbali zikiwemo
fedha, kompyuta, simu za viganjani, mashine maalum za kuhifadhi taarifa
na taarifa mbalimbali ili kusaidia uchunguzi. Aidha, lengo la zoezi hili
sio kufuta biashara ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni kwa watu
binafsi, bali ni kudhibiti ukiukwaji wa sheria uliokithiri, ukwepaji wa
kodi na utakatishaji wa fedha haramu. Maduka machache ya kubadilisha
fedha za kigeni ambayo yalizingatia Sheria na Kanuni za Foreign Exchange na masharti ya biashara hiyo yaliachwa kuendelea na utoaji wa huduma hiyo.
Hivi sasa Serikali imeandaa Kanuni
mpya kwa ajili ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni
ambazo zitaelekeza jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo
kwa mtu binafsi au taasisi yeyote na masharti ya kuzingatiwa wakati wa
shughuli hizo.
Kanuni hizo zinalenga kuweka
mazingira mazuri ya biashara ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha
na uchumi jumla, na inakuwa yenye manufaa kwa nchi. Kwa kuzingatia
maduka mengi yaliyokaguliwa yamefungwa, Benki Kuu ya Tanzania imechukua
tahadhari ya kuhakikisha huduma ya ubadilishaji fedha za kigeni
inaendelea nchini kwa kutolewa na benki zote pamoja na Shirika la Posta.
Benki Kuu ya Tanzania itakuwa inatoa taarifa kuhusu upatikanaji wa
huduma hiyo na kuzihimiza benki za biashara na Shirika la Posta kutoa
taarifa kwa umma kuhusiana na huduma katika maduka yaliyofunguliwa na
benki hizo na Ofisi ya Posta.
Kwa kipindi kifupi cha utekelezaji
wa zoezi la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni,
thamani ya shilingi imeimarika na upatikanaji wa fedha za kigeni katika
benki za biashara umekuwa mzuri. Kabla ya zoezi la udhibiti wa biashara
ya kubadilisha fedha ya kigeni dola ya Marekani ilikuwa inauzwa kwa
wastani wa shilingi 2,450 na baada ya utekelezaji wa zoezi hivi sasa
dola ya Marekani inauzwa kwa wastani wa shilingi 2,300. Aidha, Benki za
biashara kwa wastani hivi sasa zinakusanya jumla ya dola za Marekani
milioni 15 kwa siku. Ni matarajio ya Serikali kuwa udhibiti huu
utaziwezesha Benki za biashara na taasisi nyingine kuuza fedha za kigeni
kwa wingi kwenye soko la fedha za kigeni na hatimaye kuongeza akiba ya
fedha za kigeni.
Serikali inatoa tahadhari kwa
wananchi kutoshiriki kwenye biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa
njia zisizo halali. Hivi sasa kuna taarifa kwa baadhi ya maeneo ya
mipakani na majiji ya Dar es Salaam na Arusha wamejitokeza watu
wanaofanya biashara haramu ya kubadilisha fedha za kigeni ambao
wamewaathiri baadhi ya wananchi kwa wizi. Vyombo vya usalama ikiwemo
jeshi la polisi vimeongeza nguvu katika kuhakikisha biashara hii haramu
(Black Market) inatokomezwa na hivi sasa wahalifu saba wamekamatwa na
kufikishwa mahakamani.
Serikali inapenda kuwahakikishia
Watanzania wote kuwa inayo akiba ya fedha za kigeni ya kutosha zipatazo
dola za Marekani bilioni 4.67 hadi tarehe 30 Machi 2019 zenye uwezo wa
kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisicho pungua
miezi 4.8. Hivyo, wasiwasi kuwa Serikali imechukua hatua ya kufunga
baadhi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwa sababu haina akiba
ya fedha za kigeni si ya kweli hata kidogo. Aidha, hofu kwamba nchi
inarejea katika kipindi cha nyuma ambapo fedha za kigeni zilikuwa
zinatolewa kwa vibali (rationing) ili kukidhi mahitaji ya fedha hizo
kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, nazo hazina msingi.
Mapato ya Nchi yanayotokana na
vyanzo vya fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi
yalikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 8,554.5 kwa mwaka
unaishia Februari 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.4 ikilinganishwa
na fedha za kigeni zilizopatika mwaka unaishia Februari 2018. Ongezeko
hilo la mapato ya fedha za kigeni kwa Nchi yamechangiwa zaidi na uuzaji
wa bidhaa zisizo asilia nje ya nchi zikiwa na thamani ya dola za
Marekani milioni 3,878.5 sawa na asilimia 10.3 ikilinganishwa na mwaka
uliotangulia. Vile vile, huduma zilizotolewa nje ya nchi kama vile
usafiri na usafirishaji na utalii ziliingiza jumla ya dola za Marekani
milioni 4,074.1 sawa na ongezeko la asilimia 6.1 ikilinganishwa kiasi
kilichopatikana mwaka ulitangulia.
Aidha, Serikali inachukua fursa
hii kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu ina akiba ya chakula cha kutosha
ambacho kina utoshelevu wa asilimia 124 kwa mwaka huu wa fedha 2018/19.
Hivyo, Serikali haitarajii kutumia fedha za kigeni kuagiza chakula
kutoka nje ya nchi isipokuwa tu kama ikitokea hali ya ukame ikawa mbaya
katika siku zijazo.
Serikali, kupitia Benki Kuu ya
Tanzania, inawataka wafanyabiashara ya huduma ya kubadilisha fedha za
kigeni kuzingatia na kutii Sheria ya Foreign Exchange 1992, Kanuni ya Foreign Exchange (Bureau de Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017,
Masharti ya biashara ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni na
Maelekezo ya Msimamizi (BOT) wa Sekta ya Fedha Nchi. Mwisho Serikali
inawapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuwa waelewa na watulivu wakati
wote zoezi la ukaguzi likiendelea, licha ya kujitokeza kwa taarifa za
upotoshwaji wa zoezi hili.
No comments:
Post a Comment