Pages

Friday, March 29, 2019

SERIKALI KUSOMESHA WATAALAM 100 ISRAEL

????????????????????????????????????
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe. Omari T. Mgumba (Mb.)  (kulia) akiongea na Naibu Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ambae pia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya MASHAV, Bw.  Gil Haskel walipofanya kikao katika Ofisi ya Naibu Waziri wa Kilimo, iliyopo Kilimo IV, Mjini Dodoma hivi karimuni
………………………
Na Bashiri Salum,Wizara ya Kilimo – Dodoma

Serikali kupeleka wataalam 100 wa kilimo nchini Israel ili kujifunza  mbinu bora na
teknolojia za kisasa za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji nchini.
Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano baina  ya Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe. Omari T. Mgumba (Mb.) na Naibu Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ambae pia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya MASHAV, Bw.  Gil Haskel walipofanya kikao katika Ofisi ya Naibu Waziri wa Kilimo, iliyopo Kilimo IV, Mjini Dodoma
Mhe. Mgumba amebainisha kuwa,  nafasi hizo za masomo ya kilimo nchini Israel zitatoa fursa kwa wataalam hao kuongeza ufanisi katika Sekta ya kilimo nchini na kukifanya kilimo kuwa na tija zaidi.
Aidha, Naibu Waziri wa Kilimo amesema kuwa, tatizo kubwa la Sekta ya Kilimo nchini ni uzalishaji mdogo usiokuwa na tija  ambapo wakulima hutumia nguvu kubwa lakini matokeo yanakuwa madogo. Hivyo, Naibu Waziri huyo alisisitiza kuwa, wakulima nchini wanatakiwa kuzingatia mbinu bora za kilimo, matumizi sahihi ya pembejeo, mbolea na pia kutumia mbegu bora ili kuweza  kumnufaisha mkulima.
Akiongea na mgeni huyo kutoka Israel,  Mhe. Mgumba amebainisha kuwa, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kwa kiasi kikubwa Sekta ya  Kilimo hivyo ni muhimu kilimo cha umwagiliaji kikaanza kutumika maeneo mbalimbali ya nchi kwa sababu ya uwepo wa vyanzo vya maji vya kutosha na sio kuendelea kutegemea kilimo cha mvua ili  kupambana na hali hiyo.
Pia, Mhe. Mgumba amesisitiza kuwa, serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuwa ikihamasisha wakulima nchini kuanza kufanya kilimo cha kibiashara ili kuweza kuongeza kipato chao.
Aidha, ametoa ufafanuzi kwa mgeni  huyo kuwa, Serikali ya Israel bado inaweza kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa bado eneo linalotumika kwa kilimo hicho ni dogo ikilinganishwa mahitaji.
“Hadi sasa eneo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 475,000 na Mkakati wa Serikali ni kufikia hekta milioni moja ifikapo mwaka 2035”alisema Naibu Waziri, Mhe. Mgumba.
Aidha, Mhe. Mgumba ameiomba Serikali ya Israel kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza bonde la mto rufiji kwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili wakulima wengi waachane na kilimo cha kutegemea mvua kama ilivyo sasa.
Awali, Mhe. Mgumba alimfahamisha Mtendaji Mkuu huyo wa Taasisi ya MASHAV kwamba, bado kuna fursa ya uwekezaji katika eneo la uhifadhi wa mazao kwa kuwa hali ya  upotevu wa mazao baada ya mavuno ni asilimia 40 ikilinganishwa na nchi ya Israel ambayo upotevu ni asilimia 20. Akifunga Kikao hicho, Mhe. Mgumba alisema kuwa, ili kilimo kiwe na tija na kuweza kumkomboa mkulima nchini, lazima kuacha kutegemea mvua za msimu pekee na hivyo kuanza kutumia kilimo cha umwagiliaji nchini.

No comments:

Post a Comment