Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim
Wangabo amewashauri Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani Rukwa kukutana
na madiwani pamoja na wenyeviti wa halmashauri zinazopitiwa na barabara
ya Tunduma – Sumbawanga ili kuyabaini matuta yaliyowekwa maeneo ambayo
hayana ulazima hivyo kutostahili kuendelea kuwepo kwenye barabara hiyo
na
hatimae kujiandaa kuyapunguza wakati wakiendelea kusubiri maamuzi ya
Wizara.
Amesema kuwa endapo zoezi hilo
litakuwa shirikishi halitazua mzozo baina ya TANROADS na wananchi pindi
ajali zitakapoongezeka na kuwataka wabunge wa maeneo husika nao
kukubaliana na maamuzi yatakayotolewa na wizara husika baada ya utambuzi
huo wa matuta kufanyika.
“Kuna ukweli kwamba kuna baadhi ya
Matuta hayastahili kuendelea kuwepo, matuta zaidi ya 200 lakini kuna
baadhi yao yapo maeneo ambayo hayastahili kuwepo, mi nadhani
kungefanyika utambuzi wa matuta ambayo sio ya lazima, halafu ndio hoja
inakuwa kwamba kuna matuta Fulani ambayo sio ya lazima yapo katika
maeneo Fulani ambayo hata waheshimiwa madiwani wa maeneo yale
wameyaafiki kwasababu hii isiwe kazi ya TANROADS peke yao,”Alishauri.
Ameshauri hayo katika kikao cha
Bodi ya Barabara ya Mkoa kilichowashirikisha Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Wakuu wa
Wilaya, Wabunge, Wakurugenzi wa halmashauri pamoja na Wenyeviti wa
halmashsuri za Mkoa huo.
Ushauri huo umekuja baada ya
mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Mh. Aeshi Hilary kuilalamikia
TANROADS kuhusu wingi wa matuta hayo na matokeo yake kuwakera wasafiri
wanaotumia barabara hiyo jambo ambalo limekuwa likiwachosha wasafiri
wanaotoka mikoa ya mbali na Mkoa wa Rukwa.
“Utakuta kuna matuta ambayo
yanawekwa sehemu ambapo wala hayastahili, barabra hii ya Tunduma –
Sumbawanga ina matuta zaidi ya 240 inazidi hata kilometa za barabara
yenyewe, kuna tuta lipo katikati ya daraja, kwa mfano kuna Kijiji cha
Tamasenga peke yake kina matuta kumi, kuna umuhimu gani wa kuyaweka yote
hayo katika Kijiji kimoja, mlisema mtayaondoa lakini hapa kwenye bajeti
yenu sioni kama mmelizungumzia,” Aliuliza.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS
Mkoani Rukwa Mhandisi Masuka Mkina alibainisha kuwa uwepo wa matuta
hayo umepunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani na kuongeza kuwa
wafadhili waliowezesha ujenzi wa barabara hiyo kauli mbiu yao ilikuwa ni
“Usalama Kwanza”.
“Alipokuja hapa Katibu Mkuu
Nyamhanga nilizungumza lakini baadae akasema tuyaache kwanza, kwahiyo
suala la matuta kwa sasa mimi sina la kuzungumza kwasababu serikali bado
wanaendelea kulitafakari kwamba wayatoe au yabaki, kwasababu yamesaidia
sana ukiangalia takwimu kwa barabara ya Tunduma – Sumbawanga ajali
nikama sifuri,” Alisema.
Barabara ya Tunduma – Sumbawanga
yenye kilometa 227 inakadiriwa kuwa na matuta 212 huku madatuta kadhaa
yakiwa katikati ya madaraja na Kijiji cha Tamasenga kuwa na matuta 10
imefadhiliwa kwa msaada wa watu wa Marekani imesaidia kurahisisha safari
ya Tunduma kwenda Sumbawanga ambapo hapo kabla wasafiri walitumia siku
nzima.
No comments:
Post a Comment