Watoto
ambao ni wagonjwa wa moyo kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania wakiwa na wazazi
wao wakisubiri kulazwa wodini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo na
madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana wenzao wa mradi wa afya wa Little Hearts wa
nchini Saudi Arabia ambao ni moja ya mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya
Msaada ya Muntada yenye makao Makuu yake
mjini London nchini Uingereza. Jumla ya watoto 80 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji
katika kambi hiyo ya matibabu ya siku nane.
NA
GENOFEVA MATEMU – JKCI
JUMLA
ya watoto 80 wenye matatizo ya moyo wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo
katika kambi maalum ya matibabu itakayofanywa na madaktari bingwa wa magonjwa
ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
mradi wa Little Heart wa nchini Saud Arabia ambao ni moja ya mradi wa Afya
ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao Makuu yake mjini
Londoni nchini Uingereza. Matibabu
hayo yatahusisha upasuaji wa moyo wa kufungua kifua kwa watoto wenye matatizo
makubwa na upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo kwenye paja kwa
watoto wenye matatizo yasiyohitaji upasuaji wa kufungua kifua. Watoto
wanaotarajiwa kufanyiwa matibabu hayo katika kambi hiyo wameshafika katika Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kufanyiwa uchunguzi wa awali tayari kwa
kulazwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji huo. Kambi
hiyo ya siku nane inatarajia kuanza kesho tarehe 1 Desemba 2018 hadi tarehe 8
Desemba 2018 kwa kutoa matibabu ya kina kwa watoto wote walioandaliwa kwa ajili
ya kupatiwa matibabu ya magonjwa ya moyo. Tangu
mwaka 2015 jumla ya watoto 296
wameshafanyiwa upasuaji na madaktari kutoka mradi wa Little Heart kwa
kushirikiana na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI ambapo
watoto 111 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na watoto 185 walifanyiwa
upasuaji wa bila kufungua kifua. Hii
ni mara ya nne kwa madaktari wa Little Heart wa nchini Saud Arabia ambao ni
moja ya mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao
Makuu yake mjini London nchini Uingereza kuja hapa nchini kwa ajili ya kutoa matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto kwa
kushirikiana na madaktari wa JKCI.
No comments:
Post a Comment