Katibu Tawala wa Mkoa
wa Manyara, Missaile Mussa akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa huo
kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa
Manyara Alexander Pastory Mnyeti akizungumza kwenye kikao cha kamati ya
ushauri cha mkoa huo (RCC) Mjini Babati.
Meneja wa Tanroads
Mkoani Manyara mhandisi Bashiri Rwesingisa akielezea taarifa ya
utekelezaji wa matengenezo na ukarabati wa barabara za mkoa huo Mjini
Babati.
…………………………
MKUU wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amesema mkoa huo unazidi kung’ara na
kupiga hatua kwenye sekta mbalimbali ya maendeleo, hivyo viongozi
waendelee kuwatumikia zaidi wananchi.
Alisema kwenye makusanyo ya ndani mkoa huo umeshika nafasi ya pili kitaifa katika kipindi hiki cha robo mwaka.
Alisema kwenye miradi
ya maendeleo iliyokaguliwa na mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka huu
wamefanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa kwani miradi yao ilikubaliwa
na ilipitishwa yote, hakukuwepo uliokataliwa.
Alisema kwenye
makusanyo ya mamlaka ya mapato nchini (TRA) mkoani humo lengo lilikuwa
kukusanya shilingi bilioni 6.453 kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka
huu, wamekusanya shilingi bilioni 6.695 sawa na asilimia 103.8 ya
lengo.
“Katika mwaka huu wa
fedha tumepiga hatua ya maendeleo katika ukusanyaji wa mapato ambapo
Halmashauri zimekusanya shilingi 5,464,290,534.38 sawa na asilimia 38 ya
lengo la mwaka,” alisema Mnyeti.
Alisema kwenye agizo
la kila mkoa kuwa na viwanda vipya 100 wamefanikiwa kwenye hilo kwani
hata Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo alisema mkoa wa Manyara upo kwenye
tatu bora kwa kuwa na viwanda vipya.
“Kwenye viwanda vipya
tumefanikiwa mno na katika hili najua tunapambana na mkoa wa Pwani,
kwani huku kuna viwanda vinalipa kodi kubwa serikalini na vimetoa ajira
nyingi kwa wananchi,” alisema Mnyeti.
Alisema hali ya elimu
ipo vizuri kwani kuna ongezeko la watoto wakuandikishwa kuanzia darasa
la kwanza na kidato cha kwanza baada ya sera ya elimu bila malipo kuanza
kutekelezwa.
“Lengo la mkoa la
kuandikisha wanafunzi wa darasa la awali lilikuwa 46,709 ila
wameandikishwa 42,989 sawa na asilimia 92 na darasa la kwanza lengo
lilikuwa 52,923 na wameandikishwa 54,496 sawa na asilimia 107.4,”
alisema Mnyeti.
Alisema ongezeko hilo
limekwenda sambamba na ongezeko la ufaulu wa wanafunzi wa darasa la
saba kutoka asilimia 59. 18 mwaka 2015 hadi asilimia 70.79 mwaka huu.
Alisema kwa upande wa kidato cha nne ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 72 mwaka 2015 hadi asilimia 82.53 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment