Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Magufuli amesema kituo kipya cha ukaguzi Namanga kinatarajia kuingizia
Tanzania Shilingi Bil. 58 mwaka huu wa fedha, 2018/2019.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo
Namanga, Jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kituo hicho uliofanyika
mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Rais Magufuli amesema, kukamilika
kwa kituo hicho kumeongeza mapato kutoka wastani wa
shilingi Bil. 3 kwa
mwezi hadi shilingi Bil. 4.5 kwa mwezi ambapo kwa mwaka huu wa fedha
Serikali ya Tanzania inatarajia kukusanya jumla ya shilingi Bil. 58
kutoka katika kituo hicho.
“Ujenzi wa vituo vya huduma za
pamoja mipakani vimerahisha huduma za usafiri na kupunguza gharama za
muda.Zamani watu walikuwa wakitumia siku nzima kuvuka mpaka, lakini sasa
hivi mtu anatumia dakika 15 tu kuvuka mpaka huo,” amesema Rais
Magufuli.
Amesema, kituo hicho
kitawawezesha wafanyabiashara kuvusha bidhaa zao zaidi ya mara Kumi kwa
mwezi tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo ilikuwa nadra kwa
mfanyabiashara kuvuka mpaka huo hata mara Nne kwa mwezi.
Aidha amesema, kituo hicho
kitaimarisha shughuli za biashara na utalii kwa nchi zote mbili kutokana
na kurahisishwa kwa huduma ya usafiri pamoja na miundombinu mingine
katika kituo hicho.
Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri
ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta amesema ni jukumu lao viongozi kuhakikisha
wananchi wanafanyabiashara bila kupingwa na waweze kuimarisha biashara
kati ya nchi hizo mbili.
Amesema dhumuni la ujenzi wa
kituo hicho ni kuwarahisishia wafanyabiashara wadogo na wakubwa kufanya
biashara zao kwa urahisi, ili kila mwana jumuiya wa Afrika Mashariki
aweze kunufaika na umoja huo.
Aidha amewataka wale wote
waliopewa jukumu la kusimamia kituo hicho basi wajue kazi yao sio
kumnyanyasa mwananchi bali kumsaidia mwananchi afanye biashara yake. Pia
wananchi wajue kuwa wakisaidiwa kufanya biashara hawajaambiwa kufanya
biashara ya madawa ya kulevya, kuua wanyama au biashara ya magendo bali
wanatakiwa kufanya biashara ya haki ili mtu apate fedha yake ya haki.
Nae, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe Balozi Dkt. Augustine Mahige
amesema, kuwa na kituo kimoja cha forodha na uhamiaji kinaboresha soko
la pamoja la Afrika Mashariki.
Vile vile amesema, baada ya soko la pamoja, Jumuiya ya Afrika Mashariki inajiandaa kuwa na sarafu moja ifikapo 2020.
Kituo cha pamoja Namanga
kimejengwa kwa ufadhili wa nchi ya Japani kupitia Shirika la Maendeleo
la JICA ambapo kwa upande wa Tazania jumla ya shilingi Bil. 18.6
zimegharamiwa . Aidha Benki ya Maendeleo ya Afrika imefadhili kiasi cha
Dola za Marekani 117,000 kwa ajili ya kuweka vifaa vya ofisi kwa upande
wa Tanzania na Kenya.
No comments:
Post a Comment