Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imeandaa Mdahalo mkubwa utakaofayika Novemba 19,
kwa lengo la kuongeza uelewa wa Wananchi juu ya umuhimu wa Takwimu
katika maendeleo ya Taifa.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mayasa
Mahfudh Mwinyi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa
habari ofisini kwake Mazizini kuhusu shamrasharma za maadhimisho ya siku
ya Takwimu Afrika.
Amesema Takwimu zina umuhimu
mkubwa katika kupanga maendeleo ya Taifa hivyo
wananchi wanapaswa kujua
kwa undani wake ili kutoa mashirikiano kwa ofisi hiyo.
Amesema Ofisi ya Takwimu
itaendelea na jukumu lake la kufanya Tafiti katika nyanya mbalimbali
ikiwemo za kiuchumi, kimaendeleo na kijamii na kuishauri Serikali na
Taasisi binafsi kuhusu mwelekeo wa kiuchumi.
Aidha amezishauri Taasisi za
Serikali na binafsi kuzitumia Takwimu zinazotolewa na ofisi hiyo ili
zipige hatua mbele kimaendeleo na kukabiliana na changamoto zao.
Alisisitiza wadau wote wanaotaka
kufanya tafiti rasmi kwenda katika Ofisi yao kuomba ushauri wa kitaalamu
ili Takwimu watakazozipata katika tafiti zao ziwiane na Takwimu ya
Ofisi yake.
“Ili kuepuka mgongano wa Kitakwimu
nawaomba Wadau wote wanaofanya Tafiti basi waje ofisini tuwasiliane
kuboresha Takwimu badala ya takwimu hizo kugongana” alisisitiza Mtakwimu
Mkuu.
Mbali na kilele Mtakwimu Mayasa
alielezea mambo watakayoyafanya ikiwa ni pamoja na kutoa msaada katika
nyumba za kulelea watoto Mazizini ambapo Jumapili kutakuwa na Mchezo wa
Mpira wa Miguu kati ya Ofisi ya Mtakwimu na Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa
Serikali.
Awali Mtakwimu Mwandamizi kutoka
Ofisi ya Mtakwimu Abdulmajid Jecha alisema kulingana na Takwimu za
uwezekano wa umri wa kuishi kwa Mzanzibari ni miaka 67.
Alisema miaka hiyo imeongezeka
kutokana na uimarishwaji wa huduma za Afya Zanzibar na matumizi madogo
ya ulevi ikiwemo Pombe kwa Wanzanzibari.
Hali hiyo ni tafauti kidogo kwa Tanzania Bara ambapo Makadirio ya kuishi ni miaka 66.
“Sababu zinazofanya Makadirio ya
kuishi kwa Wazanzibari kuwa juu ukilinganisha na Bara ni uimarishwaji wa
huduma za Afya kwa mfano kupungua kwa Malaria ikilinganishwa na Bara
lakini hata Ulevi ambao ni chanzo cha magonjwa Zanzibar ni kidogo
ukilinganisha na Bara ” alibainisha Abdulmajid Jecha
Hivyo Jecha alishauri watu wazidi
kuzitumia Takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi hiyo ili kujipangia
mipangilio yao ya maendeleo.
Kila ifikapo November 18 ni siku
ya Takwimu Afrika ambapo kwa Zanzibar itaadhimishwa November 19 katika
viunga vya Ofisi hiyo Mazizini, ili kufikisha ujumbe kwa wananchi wengi.
No comments:
Post a Comment