Mkuu wa Idara ya Radiolojia katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Flora Lwakatare akizungumza na
waandishi wa habari juu ya wataalam kuzibua njia ya nyongo ya mgonjwa
kupitia huduma ya kibingwa ya tiba radiolojia kwa kushirikiana na Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Taasisi ya Tiba ya Mifupa
Muhimbili (MOI) na Chuo Kikuu cha Yale na Emory nchini Marekani. Kutoka
Kushoto ni daktari bingwa wa upasuaji wa Muhimbili, Dkt Godfrey Mchele
na mtaalam wa tiba ya radiolojia, Profesa Frank Minja kutoka Chuo Kikuu
cha Yale nchini Marekani.
Baadhi ya wataalam wa tiba hiyo pamoja na waandishi wa habari wakimsikiliza Dkt. Flora Lwakatare.
Wataalam wa radiolojia wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) pamoja na wataalam kutoka
Chuo Kikuu cha Yale na Emory nchini Marekani wakishirikiana kuzibua
njia ya nyongo ya mgonjwa kupitia huduma ya kibingwa ya tiba radiolojia.
Mtaalam
wa tiba radiolojia, Profesa Frank Minja kutoka Chuo Kikuu cha Yale
nchini Marekani akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jinsi wataalam
wa Muhimbili, MUHAS na MOI walivyofanya maandalizi ya kufanikisha
huduma ya tiba radiolojia. Kushoto ni Dkt. Lwakatare na kulia ni mtaalam
wa huduma za radiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Emory nchini Marekani.
Baadhi ya wataalam wa huduma za tiba radiolojia wakifuatilia mkutano huo leo.
Dkt Lwakatare akifafanua jambo
kwenye mkutano huo leo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba
Shirikishi Muhimbili, Dkt. Praxeda Ogweo, Dkt. Mchele wa Muhimbili,
Prof. Minja kutoka Chuo Kikuu cha Yale, Dkt. Prologo kutoka Chuo Kikuu
cha Emory na Dkt. Mechiris Mango wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili
(MOI).
……………………
Dar es salaam
Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi (MUHAS), Taasisi ya Tiba Mifupa (MOI), Chuo Kikuu
cha Yale na Emory nchini Marekani wameendesha kambi maalum ya kutoa
huduma za kibingwa kupitia tiba Radiolojia ambapo wagonjwa 23
wamenufaika na tiba hiyo.
Tiba hiyo inahusisha utaalam wa kutumia vifaa vya Radiolojia kama X-Ray, MRI, CT-Scan na
Ultra- Sound kutibu moja kwa moja ugonjwa au kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya
Radiolojia MNH, Dkt. Flora Lwakatare amesema huduma hiyo ya kibingwa
ilianza kwa mara ya kwanza nchini Novemba mwaka jana ambapo kabla ya
uanzishwaji wake wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma hizi walikuwa
wakienda nje ya nchi.
Akielezea
kuhusu huduma zilizitolewa katika kambi hiyo amesema ni utoaji wa
sampuli kutoka kwenye vivimbe katika sehemu mbalimbali za mwili ambazo
si rahisi kufikiwa bila upasuaji mkubwa, kuzibua mirija ya nyongo,
kuweka mirija kwenye figo ambazo mirija ya mkojo imeziba na unyonyaji wa
vivimbe vyenye maji au usaha.
‘‘Kambi
hii imehusisha wakufunzi ambao ni madaktari bingwa, mafundi sanifu
Radiolojia, wauguzi Radiolojia kutoka vyuo vikuu vya Yale na Emory. Pia,
watalaam kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa na CCBRT nao wananufaika
na mafunzo hayo.’’
Akielezea
faida ya tiba hiyo amesema inamuwezesha mgonjwa kuepuka upasuaji mkubwa
ambao ni hatarishi, kuepuka ukaaji wa muda mrefu hospitalini na
kupunguza gharama.
Tangu kunzishwa kwa tiba Radiolojia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wagonjwa takribani 100 wamenufaika na huduma hiyo.
Naye
Dkt. Mchele amesema kuwa ujio wa wataalam hao kutoka Chuo Kikuu cha
Yale na Emory umekua msaada mkubwa kwa wataalam wa Muhimbili, MUHAS na
MOI kwa kuwa wamejifunza mambo mengi ya kitaalam.
“Tumejifunza
mambo mengi ambayo yatatuwezesha kuendelea sisi wenyewe baada ya timu
hii kurejea Marekani. Hii imetusaidia sana kwani kuna baadhi ya
wagonjwa wana usaa kwenye ini, hivyo wametuwezesha kugundua tatizo
mapema na kuweza kufanya upasuaji kwa mgonjwa bila kuacha jeraha kubwa,”
amesema Dkt. Mchele.
Amesema
kuanza kwa huduma ya tiba radiolojia ni hatua nzuri na muhimu kwani
mwaka 2022, Muhimbili inatarajia kuanza kupandikiza ini na kwamba tiba
radiolojia ni moja ya maandalizi ya kuelekea kupandikiza ini.
No comments:
Post a Comment