Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewa himiza watanzania kushirikiana
na Serikali yake katika masuala makubwa ya msingi ili kuliletea Taifa
maendeleo ya haraka
Akizungumza leo katika ukumbi wa
Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, wakati wa
Kongamano kuhusu
hali ya uchumi na Siasa nchini, lenye mada isemayo “Miaka Mitatu ya
Serikali ya Awamu ya Tano Tunatoka Wapi, Tuko Wapi na Tunakwenda Wapi?”,
Rais Magufuli alisema kuwa anawaomba watanzania kuendelea kushirikiana
Serikali yake ili kujiletea maendeleoa.
“Nawaomba watanzania katika mambo
makubwa ya msingi ni lazima tusimame kwa pamoja, na si kujali itikadi za
vyama vyetu vya siasa”alisema Rais Magufuli
Aidha, alisisitiza kuwa “ mambo ya chama yatatuchelewesha, watanzania hawataki vyama, wanataka maendeleo”
Katika kongamano hilo ambalo Rais
Magufuli alikuwa mgeni maalum, amesisitiza namna ambavyo Serikali ya
Awamu ya Tano imedhamiria kuwaletea maendeleo watanzania kwa
kushirikiana na sekta binafsi ili kujenga uchumi.
Rais Magufuli amekaribisha sekta
binafsi katika kilimo ili kuimarisha sekta hiyo kwa kuwekeza katika
kilimo cha kisasa na ikiwa ni pamoja na kupata soko la uhakika la mazao
ya wakulima.
“Benki ya kilimo ina shilingi
bilioni 300, sekta binafsi wanaweza kuja kushirikiana na Serikali kwa
kuanzisha viwanda vitakavyosaidia sekta hiyo ya kilimo” alisema Rais
Magufuli
Kuhusu matumizi ya lugha ya
kiswahili, Rais Magufuli alisema aliamua kuzungumza kiswahili kwa sababu
kiswahili ni utamaduni wa mtanzania, lakini ni lugha ya kumi kwa kuwa
na wazungumzaji wengi duniani, na ni lugha ya pili Afrika.
Hivyo, amewataka watanzania kukithamini zaidi kiswahili, licha ya kuwa wanaweza kujifunza lugha nyingine zozote.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli
ambaye amezungumza baada ya kusikiliza mada tano zilizotolewa na
wanataaluma wakongwe wa uchumi, lugha, siasa na utawala amnbapo Rais
aliahidi kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa katika
kongamano hilo, ambayo anaamini yataleta tija na maendeleo kwa Taifa.
Mada zilizowasilishwa na
kujadiliwa ziligusia masuala mbalimbali kama vile viwanda, nishati
ambapo ifikapo mwaka 2020 vyanzo vya nishati jadilifu na visivyojadilifu
vitazalisha megawati 5,000 na mwaka 2025 megawati 10,000 za umeme.
Aidha, mafanikio mengine
yaliyojadiliwa ni pamoja na ukuaji wa uchumi kwa asilimia saba na
jitihada sahihi zinazofanywa kuelekea asilimia nane, na kufanya Tanzania
kuongoza katika nchi za Afrika Mashariki, na kuwa miongoni mwa nchi 5
za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.
Vile vile, katika kipindi hiki cha
miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na mafanikio mengine
makubwa ya kufufua miradi ya msingi wezeshi, kama ununuzi wa ndege saba,
uboreshaji wa bandari, viwanja vya ndege na barabara ni fursa ya
kuwezesha miaradi mingine ya kiuchumi,mfano,viwanda vipya zaidi ya
3,066, vilivyojengwa vitahitaji huduma za maji umeme, barabara, bandari
kama mahitaji wezeshi ya msingi.
Huduma kama usafiri wa anga
zimeboreshwa, ikiwemo sekta ya utalii ambapo mikakati ya sekta hiyo,
matarajio yake mwaka ujao watalii wanaotarajiwa kutembelea Tanzania
wataongezeka hadi kufikia milioni 2, kiwango kitakachokuwa karibu mara
mbili ya watalii waliokuwa wanatembelea Tanzania miaka ya nyuma
Katika kongamano hilo,
wahudhuriaji walipata fursa ya kujadili mada zilizotolewa, ambazo kwa
ujumla tafiti za mada zimebaini juhudi kubwa alizofikia Rais na Serikali
yake kwa muda mfupi na wasomi tafiti zao zimebaini kuwa miradi mikubwa
inayoendelea vema, itawezesha miradi mingine kuanzishwa au kufufuliwa
na kuleta maendeleo, mfano ujenzi wa Umeme ni mradi utakaowezesha ujenzi
wa viwanda, pia wameeleza changamoto na kutoa maoni.
Kongamano hilo limehudhuriwa na
viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na watendaji
mbambali wa Serikali, wakiwemo viongozi wastaafu, wabunge pamoja na
wanafunzi wa vyuo na sekondari.
No comments:
Post a Comment