Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula akifunga
mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili Wataalamu wa Mipango Miji jijini Dodoma
Jana.
NA MUNIR SHEMWETA, DODOMA
NAIBU
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mbaula amewataka
wataalamu wa mipango miji kuwa na mipango endelevu na kabambe katika miji na halmashauri zote nchini
ili kuwa na miji iliyopangika na kuepuka ubomoaji nyumba za wananchi
unaosababishwa na uelewa mdogo wa sheria na taratibu za mipango miji..
Aliwataka
wataalamu wa mipango miji kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao kuepesha wananchi kuvunja sheria unaosababishwa
na wataalamu kutowaeleza ambapo alisema si kila mwananchi anayevunja sheria za
ujenzi mjini anafanya makusudi bali wengine hawajui sheria na taratibu na
kuhitaji kuelezwa.
Akizungumza
wakati wa kufunga mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango
Miji jijini Dodoma jana, Dk Mabula
alesema maeneo mengi ya miji wataalamu wanahangaika na kazi ya kurasimisha
jambo ambalo siyo suluhisho la upangaji miji bali ni kujaribu kuweka viraka
katika vazi lililochakavu.
Akigeukia
suala la kuwepo maeneo mengi yasiyopangwa, kupimwa na kumilikishwa Dk. Mabula
alisema eneo hilo linaibua changamoto mbalimbali kwa jamii ikiwemo ongezeko la makazi holela maeneo ya mijini, kukua kwa miji
isiyo na mpangilio mzuri pamoja na kukithiri kwa migogoro ya ardhi nchini na
kuwashauri wataalamu hao wa Mipango mijini nchini kuwafuata wananchi waliko kwa
ajili ya kutatua kero zao.
Alizitaka
halmashauri ambazo muda wa mipango yake kabambe imeisha kuhakikisha zinahuisha mipango hiyo ili kuwa endelevu kwa
minajili ya kuweka miji salama na ikiwa imeandaliwa miundo mbinu muhimu kwa
mustakabali wa maendeleo ya miji na taifa kwa ujumla.
Aidha,
Dk. Mabula ametaka maeneo ambayo reli ya SGR inapita ni vyema halmashauri za
maeneo husika kuanza kufanya upangaji mapema ili reli itakapoanza maeneo yote
yawe yamepangwa, yamepimwa na yamemilikishwa na uendelezaji umefanyika ili
kuinua uchumi kwa maeneo husika na kutosubiri wajanja wakaanza kuvamia.
Katika
maazimio yake yaliyosomwa na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu Mipango
Miji Hellen Mtutwa, Washiriki walikubaliana Chuo Kikuu cha Ardhi kwa
kushirikiana na Bodi ya Usajili Wataalamu Mipango Miji kuandaa muongozo
utakaowawezesha Watendaji wa Kata na Vijiji kuwa wasimamizi wa mipango miji kwenye maeneo yao ili kuepuka ujenzi
holela na miji isiyopangwa.
Aidha,
Washiriki walikubaliana urasimishaji wa makazi ufanayike katika maeneo yote ya
nchi na siyo baadhi ya maeneo na wataalamu mipango miji kuhakikisha wanaandaa
andiko la mradi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya upangaji miji
badala ya kusubiri serikali pekee.
Mkutano
huo wa Bodi ya Usajili Wataalamu Mipango Miji uliokuwa ukijadili matatizo na
changamoto zinazowakabili Wataalamu wa taaluma za Mipango Miji katika shughuli zao na kuweka
mikakati ya kukabiliana nazo na kushirikisha wataalamu 260 kutoka
Serikali na Sekta Binafsi pamoja na Makampuni yanayojishughulisha na mipango
miji.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula akisalimiana
na Msajili wa Bodi ya Usajili Wataalamu Mipango Miji Hellen Mtutwa alipokwenda
kufunga Mkutano wa tano wa Bodi jana jijini Dodoma, kushoto ni Mwenyekiti wa
Bodi Welbert Kombe.
Sehemu
wa washiriki wa Mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango
Miji uliofanyika jijini Dodoma. (Picha na Hassan Mabuye wa Wizara ya Ardhi)
No comments:
Post a Comment