Pages

Sunday, September 30, 2018

NAIBU WAZIRI DKT MABULA ASHANGAZWA NA UCHELEWESHAJI UTOAJI HATIMILIKI ZA ARDHI MVOMERO


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akikagua majalada ya hati za Ardhi katika ofisi za wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kukagua mashamba makubwa katika wilaya hiyo.
NA MUNIR SHEMWETA, WANMM MVOMERO
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ameshangazwa na ucheleweshaji utoaji hati miliki za ardhi kwa wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro. Dkt. Mabula alibaini hali hiyo baada ya kuelezwa na Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Keneth Mwenda kuwa hati 53 bado hazijapelekwa ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati kwa ajili ya kukamilishwa ili kugawiwa kwa wananchi.
Hali hiyo ilimshtua Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo hakuridhishwa na sababu za ucheleweshaji utoaji hati hizo kwa wananchi kwa sababu tu wameshindwa kuzipeleka ofisi ya Kanda huku baadhi ya hati hizo zikiwa ni za tangu mwaka 2017 na kuagiza majalada ya hati hizo 53 kuwasilishwa kwake mara moja kabla ya hajaondoka ili kujiridhisha na maelezo hayo. Dkt. Mabula alikuwa wilayani Mvomero katika ziara yake ya siku moja mwishoni mwa wiki kukagua Mashamba makubwa kwa lengo la kubaini mashamba yasiyoendelezwa ili hatua za kisheria zichukuliwe ikiwemo kuyafuta mashamba yote ambayo hayajaendelezwa. Baada ya kuletewa na kukagua majalada, Dkt. Mabula aliagiza hati hizo kuwasilishwa haraka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Kanda ya Kati kabla ya tarehe 10 Oktoba, 2018 kwa ajili ya kusainiwa na kurejeshwa ili zitolewe kwa wamiliki. “Hati inaweza kuandaliwa kwa siku tatu na kwa mfumo wa sasa hati inaweza kupatikana kwa siku moja lakini ninyi mnakaa nazo bila kuzifanyia kazi kwa haraka kitu ambacho kinawachelewesha wananchi kupata hati zao jambo linalowafanya walalamike.’’ alisema Dkt. Mabula.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amezitaka halmashauri zote nchini kuipa kipaumbele sekta ya ardhi kwa kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuingizia serikali mapato na kubainisha kuwa fedha nyingi zinazotumiwa na idara mbalimbali katika halmashauri nyingi zinatoka katika sekta ya ardhi. Alisema katika halmashauri nyingi alizotembelea amebaini idara ya ardhi kuwa idara pekee iliyotelekezwa kwa kutopatiwa mgao wa fedha wa kutosha pamoja na mahitaji muhimu kama magari kwa ajili ya kuiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi. Katika halmashauri ya wilaya ya Mvomero imeelezwa kuwa idara nyingine kama Afya na Elimu zimekuwa zikipatiwa fedha nyingi za matumizi hadi kufikia milioni mia mbili huku idara ya ardhi ikiambulia milioni moja jambo linaloifanya idara hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha, Aliwataka watumishi wa idara ya ardhi katika wilaya ya Mvomero kuacha kufanya kazi maofisini pekee na badala yake watenge muda wa siku tatu ndani ya wiki moja kuenda kwa wananchi kwa ajili ya kutatua kero za ardhi. Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl. Mohamed Utaly amekiri idara ya ardhi kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kupata fedha kidogo kwa ajili ya kuendesha shughuli zake za kushughulikia migogoro ya ardhi pamoja na kupima maeneo. Awali akisoma taarifa kuhusiana na sekta ya ardhi katika halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri hiyo Rugembe Maiga alieleza kuwa jumla ya mashamba 26 hayajaendelezwa katika wilaya hiyo na tayari wahusika washapelekewa wito wa kujieleza kuhusiana na kutoendeleza mashamba na kati ya hao waliopelekewa wito huo wamiliki 12 walitekeleza huku 14 wakiwa kimya jambo linaloifanya halmashauri kuanza mchakato wa kuyafuta.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akitoa maelekezo kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro wakati wa ziara yake ya kukagua mashamba makubwa katika wilaya hiyo, kulia kwake ni mkuu wa wilaya ya Mvomero Mohamed Utaly.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akitoa maelekezo kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro wakati wa ziara yake ya kukagua mashamba makubwa katika wilaya hiyo, kulia kwake ni mkuu wa wilaya ya Mvomero Mohamed Utaly.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro Mwl Mohamed Utaly akizungumza katika kikao baina ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kukagua mashamba makubwa katika wilaya hiyo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akiwasili katika ofisi za wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kukagua mashamba makubwa katika wilaya hiyo, kulia kwake ni mkuu wa wilaya ya Mvomero Mohamed Utaly.

No comments:

Post a Comment