Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalinzi, Wilaya ya
Kigoma Vijijini wakati Waziri huyo alipofanya ziara wilayani humo kwa
ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wilayani humo. Waziri
Lugola alitangaza operesheni kuanza kwa operesheni ya kuwaondoa
wahamiaji haramu mkoani Kigoma. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma,
Samson Anga. Kulia ni Mwanasheria wa Sekretaireti ya Mkoa wa huo, Said Kamugisha. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola akiyaangalia majina ya watuhumiwa waliopo mahabusu katika
Kituo cha Polisi Manyovu, wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma, alipokua
anaonyeshwa na Askari Polisi wa zamu kituoni hapo, Peter Charles. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola (katikati) akiwahoji watuhumiwa (hawapo pichani) ndani ya
mahabusu ya kituo cha Polisi Manyovu wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma,
alipofanya ziara katika kituo hicho kujua utendaji kazi wa Polisi wa
kituo hicho kilichopo mpakani na nchi ya Burundi. Kulia ni Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya
Buhigwe, Luteni Kanali, Michael Ngayalina, na nyuma yake ni
Mkuu wa
Kituo hicho, Nickobay Mwakajinga. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Felix Mwagara, MOHA-Buhigwe
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola, ameitaka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma ishirikiane na
Jeshi la Polisi kufanya operesheni maalum ya kuwaondoa wahamiaji haramu
mkoani humo.
Akizungumza na mamia ya wananchi
katika uwanja wa Mnanila mjini Manyovu wilayani Buhigwe, leo, Lugola
alisema anataarifa za kutosha kuhusu wahamiaji haramu kutoka nchi za
jirani wapo mkoani humo, hivyo lazima waondolewe kwa mujibu wa sheria.
Lugola ambaye alikua akishangiliwa
na wananchi baada ya kutoa agizo hilo, pia alikemea tabia ya baadhi ya
watu wanaohifadhi raia hao wa kigeni ambao wameingia nchini kinyume cha
sheria.
“Sasa natoa agizo hili na
litekelezwe, Uhamiaji mkoa washirikiane na polisi kuwaondoa raia hawa wa
kigeni ambao wameingia nchini kwa njia zisizo halali, nataka operesheni
hii ianze mara moja,” alisema Lugola.
Lugola pia aliirudia kauli hiyo ya
kuondolewa kwa wahamiaji hao haramu alipokua anazungumza na wananchi wa
Kijiji cha Kalinzi, Wilaya ya Kigoma Vijijini, na kuongeza kuwa
anashangaa wahamiaji hao wanaendelea kuwepo mitaani huku maafisa
uhamiaji wakiwepo mkoani humo.
“Hivi inakuaje, wananchi
wanalalamika hapa kuhusu uwepo wa wahamiaji haramu, lakini Uhamiaji mpo,
mnakaa kimya tu, mnataka mpaka mimi nije ndio nitoe maelekezo haya? Hii
sitaki kusikia tena, nataka operesheni hii ianza mara moja na iwe
endelevu,” alisema Lugola.
Hata hivyo, Lugola alisema katika
operesheni hiyo lazima maafisa wa uhamiaji wawe makini wakati
wanawaondoa wahamiaji haramu pekee na sio kuwasumbua wananchi wa Kigoma
ambao ni raia halali wa nchi hiyo.
Lugola alifafanua kuwa operesheni
hiyo itasaidia kupunguza matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali
mkoani humo ambapo kwa kiasi kikubwa hutekelezwa na wahamiaji hao
haramu.
Aidha, Waziri Lugola akiwa
wilayani Buhigwe, pia ametembelea kituo cha Polisi cha Manyovu kilichopo
mpakani na nchi ya Burundi na kukagua utendaji kazi wa askari Polisi wa
kituo hicho pamoja na kuiwahoji watuhumiwa waliopo mahabusu kujua
makosa yaliyowafanya wawepo ndani ya kituo hicho.
No comments:
Post a Comment