Pages

Friday, July 20, 2018

Watumishi wasioripoti vituoni kufukuzwa

Picha
Fadhili Abdallah, Kigoma
SERIKALI imetangaza kuwafuta kwenye ajira ya utumishi wa serikali watumishi wote wa sekta ya afya walioajiriwa mwaka huu ambao watashindwa kuripoti kwenye vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14 kuanzia sasa.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitoa kauli hiyo ya serikali alipoanza ziara ya kiserikali ya siku tatu mkoani Kigoma na kusema kuwa watumishi wataoshindwa kuripoti vituoni wataondolewa kwenye mpango wa kuajiriwa serikalini.
Akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma ya Maweni, Waziri Ummy alisema serikali haitakubali kuona mpango wa kuondoa upungufu mkubwa wa watumishi sekta ya afya unavurugwa na watu wenye mazoea ya kuishi Dar es Salaam.
Alisema serikali imeajiri watumishi 1,468 kati ya watu 4,302 walioomba ajira kwenye sekta ya afya na kwamba kati ya hao hakuna mtumishi hata mmoja ambaye amepangwa Dar es Salaam ukiwa ni mpango maalumu wa serikali kuhakikisha maeneo yenye ugumu wa kufikika yenye uhaba mkubwa wa watumishi yanakuwa na huduma muhimu na za kibingwa za afya.
Pamoja na hilo, alisema serikali inaweka mazingira mazuri kwa madaktari bingwa mikoani kutumia vifaa vya serikali siku ambazo si za kazi kuhudumia wagonjwa kwa malipo nafuu yatakayotozwa kwa madaktari hao ili kuwezesha wagonjwa kupata huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari hao wakati wote.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy aliitaka Hospitali ya Mkoa Kigoma ya Maweni kuweka orodha ya huduma za matibabu katika mbao za matangazo eneo la mapokezi ya Huduma za Nje ili kuwezesha wagonjwa kujua gharama bila kuzunguka kuulizia gharama hizo.
Awali Mganga Mkuu wa Mkoa Kigoma, Paul Chaote alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma ya afya mkoani humo, ambapo kwa mwaka wa fedha ulioisha, serikali imetoa Sh bilioni 6.4 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati mkubwa kwenye vituo vya afya 10 kwenye halmashauri saba za mkoa huo.
Sambamba na hilo, Dk Chaote alisema kwa mwaka uliopita mkoa umepokea watumishi 396 ambapo kati yao 31 wamepangwa Hospitali ya Rufaa ya Maweni, ikiwa ni kukabiliana na pengo la asilimia 65 ya watumishi linaloukabili mkoa huo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Maweni, Dk Osmund Vyegura alisema kuwa hospitali inakabiliwa na mrundikano mkubwa wa wagonjwa kwani inapokea wagonjwa kutoka hospitali zote za wilaya za mkoa huo huku, ikiwa na idadi ya madaktari bingwa watatu ambapo ameishukuru serikali kwa kuipatia madaktari saba kati yao watatu wakiwa madaktari bingwa.

No comments:

Post a Comment