Pages

Wednesday, July 25, 2018

TANZIA: ALIYEKUWA MPIGA PICHA WA UHURU NA MZALENDO MWALIMU OMARY AFARIKI AKIPATIWA MATIBABU HOSPITALI; ALIAGIZA APELEKEWE FULANA YAKE ILIYOANDIKWA "UHURU NA MZALENDO"



NA K-VIS BLOG, Khalfan Said

ALIYEKUWA Mpiga picha mashuhuri wa mgazeti ya Chama Cha Mpainduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, Mwalimu Omary amefariki dunia mapema leo alfajiri Julai 25, 2018, akiwa na umri wa miaka 86.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 25, 2018 na mtoto mkubwa wa marehemu, Bw. Omary Mwalimu Omary imesema Mwalimu Omary amefariki leo alfajiri Julai 25, 2018 wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali na Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam

“Mzee alianza kulalamika kuumwa tumbo wiki mbili zilizopita na kufuatiwa na kupooza mkono na mguu, ambapo kabla ya kufikishwa hapa Mloganzila, Mzee tulimpeleka hospitali za Magomeni Mapipa na kuhamishiwa Mwananyamala kabla ya kuletwa huku Mloganzila  kufanyiwa vipimo vya kichwa.” Alisema.

Bw. Omary alisema, Mwalimu Omary ambaye alifanya kazi kwa miaka mingi kwenye magazeti ya Uhuru na Mzalendo, alipata nafuu kidogo na aliweza hata kuzungumza nae.

“Nakumbuka mara ya mwisho (jana Julai 24, 2018) Mzee aliniambia nimletee fulana yake iliyoandikwa Uhuru na Mzalendo, na kweli nilikuwa nimemchukulia leo hii, lakini nilipofika nikakuta kitanda chake kiko tupu, na baada ya kuuliza nikaambiwa na manesi pole, mzee ametutoka,” Alisema Bw. Omary katika mahojiano kwa njia ya simu.

Aidha Bw. Omary amesema, mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa marehemu Mburahati jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Omary ameacha mke, watoto wanne na wajukuu 11.

Mwenyezimungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi AMIN.

No comments:

Post a Comment