NA MWANDISHI MAALUM
“Kesho ya Mtu hujengwa leo na Tofali la kujengea kesho hufyatuliwa
leo” hii ni kauli ya Bibi.
Sarah Kibonde Msika, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji kutoka
Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii – SSRA akizungumza na vijana
waliotembelea banda la Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 13 ya Elimu ya Juu na
Taasisi za Kitafiti na wadau wa elimu ya juu yanayoendelea katika viwanja vya
Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Akifanunua kauli hiyo, Mkuu huyo wa Kitengo kutoka SSRA
anasema, Taifa linakabiliwa na kiwango kikubwa cha umaskini wa kipato hasa kwa
baadhi ya makundi kama ya wazee, jambo linalotokana na watu wengi kutokuwa na
utaratibu wa kujiwekea akiba na maandalizi ya kufikia uzee, hivyo kuwahimiza
vijana wenye nafasi ya kurekebisha hali hiyo kuanza maandalizi mapema kwa
kujiwekea akiba kwa njia mbalimbali ikiwemo Mifumo ya Hifadhi ya Jamii .
Kwa kutambua changamoto hiyo ya umaskini wa kipato hasa wakati
wa uzee, SSRA inajukumu la kuhakikisha watanzania wanapata kinga kwa ajili ya
kuwalinda dhidi ya majanga ya kiuchumi na kijamii. Mpaka sasa imefanya juhudi
ya kuanzisha mipango ya kupambana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha
mfumo utakaoruhusu kila kundi katika jamii kufaidika na huduma za Hifadhi ya Jamii.
Miongoni mwa mipango hiyo ni pamoja na mfumo wa hiari/ziada (Supplementary
Schemes), wenye lengo la
kukabiliana na mahitaji mahususi
ya nguvukazi katika sekta isiyo rasmi ambayo kwa hakika inajumuisha sehemu
kubwa zaidi ya nguvukazi nchini, anasema Bibi. Sarah Kibonde.
Akifafanua kuhusu Mpango huo, Bibi. Sarah anasema chini
ya usimamizi wa SSRA, nguvukazi kutoka katika wa sekta isiyo rasmi na hata
wanafunzi wa vyuo vikuu sasa ina fursa ya kuchagua na kuchangia kiasi chochote
wanachomudu kila mwezi au kila mara kadiri watakavyoweza. Katika mfumo huo
inahimizwa zaidi kuwa fao litakalopatikana litategemea kiasi cha michango kitakachotolewa.
Kiasi cha michango kinavyokuwa kikubwa zaidi ndivyo fao linavyokuwa kubwa
zaidi. Kuhusu utaratibu na namna ya kujiunga na mfumo huu wa hiari Bibi. Sarah
anawashauri vijana kutembelea katika ofisi za Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii.
Hivyo basi, SSRA inatumia maonesho haya ya Elimu ya Juu kuelimisha
Umma juu ya masuala ya Hifadhi ya Jamii hususani kukutana na vijana waliopo
vyuoni na wanaotarajiwa kuingia vyuoni, lengo likiwa ni kuwaelimisha na
kuwaimiza kuweka akiba jambo litakalowajengea tabia ya kuwekeza kwa ajili ya
maisha ya baadae na kuwaepusha na changamoto ya umaskini wa kipato wakati wa
uzee. “Majuto ya kesho huandaliwa leo” anasisitiza Bibi. Sarah
Kibonde
Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye banda la SSRA wakati wa
Maonyesho ya Taasisi za Elimu ya Juu yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi
Mmoja jijni Dar es Salaam.
Afisa Matekelezo wa SSRA Bw. David Lyanga akitoa maelezo
kwa wananchi waliotembelea banda la SSRA lililoko kwenye Maonyesho ya Taasisi
za Elimu ya Juu yanaendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment