Hata hivyo wananchi 8 kati ya 10 wanasema wanapaswa kuwa huru kumkosoa Rais na serikali
29 Machi 2018, Dar es Salaam:
Idadi kubwa ya wananchi hawajisikii huru kumkosoa Rais (60%), Makamu wa
Rais (54%) na Waziri Mkuu (51%). Karibu nusu ya wananchi pia hawajisikii
huru kuwakosoa mawaziri (47%), Wakuu wa Mikoa (46%) na Wakuu wa Wilaya
(43%). Hata hivyo, idadi kubwa ya wananchi (87%) wanasema wanapaswa kuwa
huru kuikosoa serikali na Rais kwa kufanya maamuzi mabaya na
kutosikiliza ushauri (80%). Wanaamini kupitia ukosoaji wanaweza
kuisaidia serikali kutofanya makosa (81%) na si
kuwashushia hadhi
watendaji wa umma au kuhatarisha umoja (19%). Vilevile wananchi hawaungi
mkono matumizi ya lugha ya matusi ambapo asilimia 71 ya watanzania
hawataki wananchi waruhusiwe kuwaita wafuasi wa chama chochote cha siasa
“wapumbavu au malofa”.
Matokeo haya yametolewa na
Twaweza katika muhtasari wake uitwao Siyo kwa kiasi hicho? Maoni ya
wananchi kuhusu taarifa na mijadala. Takwimu za muhtasari huu zinatokana
na utafiti wa Sauti za Wananchi ambao huratibiwa na taasisi ya Twaweza.
Sauti za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu
za mikononi. Una uwakilishi wa Tanzania Bara pekee, Zanzibar haihusiki
kwenye utafiti huu. Kwa maelezo zaidi kuhusu mbinu za utafiti huu
tembelea www.twaweza.org/sauti.
Takwimu za muhtasari huu zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,519 kutoka
awamu ya 25 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, na zilikusanywa kati
ya Novemba 7 na Novemba 27 mwaka 2017.
Wananchi wengi wana imani
kubwa na taarifa zinazotolewa na Rais (70%) na Waziri Mkuu (64%). Idadi
ndogo zaidi wanamwamini mwenyekiti wao wa kijiji (30%), wabunge (wa
chama tawala 26%, wa upinzani 12%), na viongozi wa serikali kwa ujumla
(22%).
Wananchi pia wanaendelea
kuunga mkono kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa taarifa: wananchi 7 kati
ya 10 wanasema taarifa zinazomilikiwa na mamlaka za umma ni mali ya
umma (70%, juu zaidi kutoka 60% mwaka 2015); na wananchi 9 kati ya 10
wanasema wananchi wa kawaida wapate taarifa zinazomilikiwa na mamlaka za
umma (86%, juu zaidi kutoka 77% mwaka 2015) na kwamba kwa kuwapa
wananchi uwezo wa kupata taarifa kunaweza kupunguza rushwa (86%, juu
zaidi kutoka 80% mwaka 2015).
Pamoja na kuunga mkono kwa
kiwango kikubwa upatikanaji wa taarifa, wananchi 9 kati ya 10 hawajawahi
kuomba taarifa kutoka katika ofisi za serikali (95%), mamlaka za maji
(93%), au vituo vya afya (93%). Wananchi wameendelea kutumia vyanzo vile
vile vya habari bila kuwa na mabadiliko makubwa isipokuwa kwa upande wa
runinga: mwaka 2013 runinga ilikuwa ni chanzo kikuu cha taarifa kwa 7%
ya wananchi, mwaka 2017 ni asilimia 23 ya wananchi. Hata hivyo, imani
kwa aina mbalimbali za vyanzo vya habari inashuka – radio kutoka 80%
mwaka 2016 hadi 64% mwaka 2017, runinga kutoka 73% mwaka 2016 hadi 69%
mwaka 2017 na maneno ya kuambiwa kutoka 27% mwaka 2016 hadi 13% mwaka
2017.
Pamoja na kushuka kwa imani na
vyombo vya habari, wananchi bado wanaunga mkono uhuru wa vyombo vya
habari: wananchi wanasema gazeti lililochapisha taarifa za uongo ama
zisizo sahihi liombe radhi na kuchapisha marekebisho (62%) badala ya
gazeti hilo kufungiwa ama kutozwa faini (38%). Idadi kubwa ya wananchi
pia wanasema kuwa serikali ipate ridhaa ya mahakama katika kufanya
maamuzi yoyote ya kuliadhibu gazeti kwa kutoa taarifa zenye maudhui
yasiofaa (54%).
Japokuwa wananchi wana mtazamo
thabiti kuhusu upatikanaji wa taarifa na uhuru wa kuzungumza, ni
wananchi wachache sana wanaofahamu sheria zinazohusiana na masuala ya
habari. Sheria inayofahamika zaidi katika suala hili ni Sheria ya Makosa
ya Mtandao (2015), ambayo inafahamika na asilimia 10 ya wananchi huku
asilimia 4 pekee ya wananchi wakifahamu Sheria ya Huduma za Habari
(2016). Wananchi wengi pia hawajaunganishwa kwenye mifumo ya uraia
ambapo ni mwananchi 1 kati ya 4 au pungufu mwenye cheti cha kuzaliwa
(25%), kitambulisho cha uraia (21%), leseni ya udereva (9%) na hati ya
kusafiria (5%). Hata hivyo, karibu wananchi wote (98%) wana vitambulisho
vya mpiga kura
Mkurugenzi Mtendaji wa
Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema: “wananchi wanaunga mkono kwa kiasi
kikubwa upatikanaji wa taarifa na uhuru wa kujieleza. Lakini ukweli wa
mambo ni kwamba, wananchi hawaombi taarifa hizo, wana imani duni na
vyanzo vyote vya taarifa ukiweka kando kauli zinazotolewa na Rais na
Waziri Mkuu, na hawajioni kama wanaweza kuwakosoa viongozi wakuu wa
serikali.”
“Kutokana na kwamba hivi karibuni serikali imepitisha kanuni za Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa
tuna imani kuwa itakidhi kiu ya
wananchi ya kupata taarifa kutoka serikalini. Tunaishauri serikali
kuweka wazi taarifa ili kuyafikia matarajio ya wananchi. Cha
kusikitisha, wananchi wanakamatwa na serikari kwa kujieleza kupitia
mitandao ya kijamii. Ni vyema serikali ikatambua thamani ya mijadala
huru ya umma na ukosoaji wenye lengo la kujenga katika mapambano dhidi
ya rushwa na katika harakati za kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.”
No comments:
Post a Comment