Pages

Friday, March 2, 2018

TEMESA NA TBA ZATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KASI NA VIWANGO



Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akifungua mkutano Uliowakutanisha Wataalam kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) na Menejimenti ya Sekta Mawasiliano (hawapo pichani), kujadili namna ya kuzingatia sheria za manunuzi Mkoani Dodoma.Kulia ni Afisa Utumishi Mwandamizi wa Sekta ya Mawasiliano, Trano Mubarok.
2
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na wafanyakazi wa Tasisi ya Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA) na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) alipokutana nao Mkoani Dodoma.
3
Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), Marwa Chacha, akimwoyesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, baadhi ya vifaa vilivyotengenezwa  kwenye moja ya magari ya Serikali yanayotengezwa na Wakala huo, wakati Naibu Waziri huyo alipokagua karakana ya magari ya wakala huo Mkoani Dodoma.
4
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akiangalia uchakavu wa moja ya nyumba zinazomilikiwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA), alipokagua nyumba hizo Mkoani Dodoma.TBA mpaka sasa inamiliki nyumba zaidi ya 800 mkoani humo.
5
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA) , Steven Simba (kulia), akimweleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (kushoto), hatua iliyofikiwa ya ukarabati wa moja ya nyumba za viongozi, wakati Naibu Waziri huyo alipokagua maendeleo ya ukarabati wa nyuma za viongozi Mkoani Dodoma.
6
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (wa kwanza), akitoa maelekezo kwa Uongoz wa Wakala wa MAjengo Nchini (TBA), alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mkoani Dodoma.
………………….
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amezitaka taasisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mkoani Dodoma kufanya kazi kwa kasi, viwango na ufanisi ili kuendana na kasi
ya Serikali ya Awamu ya tano yenye kauli mbiu ya Hapa Kazi tu.
Akizungumza wakati wa kikao kazi na wafanyakazi wa Taasisi ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Wakala wa Majengo (TBA) amesema ni wakati sasa wa taasisi hizo kuja na mwarobaini wa changamoto zilizopo na kubuni fursa za kuongeza kasi ya maendeleo kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya mji.
“Utendaji wenye weledi kwenye taasisi hususani katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, ufundi na ujenzi utakidhi mahitaji ya watumishi wa Serikali kwa kuwapa nyumba na ofisi zenye viwango ambazo zitakuwa za mfano kwa Makao Makuu ya Serikali”, amesema Kwandikwa.
Naibu Waziri Kwandikwa amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuzingatia thamani ya fedha kwa kuwekeza kwenye miradi yenye tija na faida ili kwenda na wakati na teknolojia iliyopo.
Baada ya kukagua nyumba zinazomilikiwa na TBA, Naibu Waziri Kwandikwa, amesema ni wakati muafaka wakala huo kuitazama upya mikataba iliyoingia na wapangaji wa nyumba hizo ili kurekebisha vipengele vyote vyenye changamoto kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa nyumba hizo ili zitunzwe na kudumu.
“Tazameni upya mikataba mliyoingia na wapangaji, haiwezekani nyumba zinachakaa na takataka zinatupwa ovyo ovyo bila kuzingatia utaratibu, ifike mahala sasa mikataba ieleze bayana, utaratibu wa utunzaji wa nyumba lakini pia uelekeze namna bora ya kutunza mazingira”, amesisitiza Kwandikwa.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa wakala huo kupitia nyumba hizo kila wakati ili kufahamu nyumba chakavu na kuweka mikakati ya kuzikarabati ili kuokoa fedha nyingi ambazo zinatumika katika ukarabati wa mara moja kwa nyumba nyingi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TBA, Steven Simba, amemuhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa TBA imejipanga kuhakikisha kuwa nyumba za Serikali zinajengwa kwa kuzingatia viwango kulingana na mahitaji.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Kwandikwa amemueleza kuwa mwanzoni walikua na nyumba mia nne, lakini sasa wameongezewa nyumba nyingine mia nne kutoka CDA na pia kuna miradi inaendelea ya ujenzi wa nyumba nyingine, hivyo uwepo wa nyumba hizo utapunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wanaohamia mkoani humo.
Naibu Waziri Kwandikwa amekagua karakana ya TEMESA, nyumba zaidi ya 800 za watumishi na viongozi na maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment