Kuna kipande cha video kinasambaa
mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa raia wa Tanzania wanaoishi nchini Oman
wamekusanyika ofisi ya Ubalozi kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana
na mateso na adhabu kali wanazopata kutoka kwa mabosi wao.
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama kipande hicho cha
video iliwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa madhumuni ya
kujua usahihi wa jambo hilo.
Ubalozi ulitoa ufafanuzi kuwa
uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi Oman na ulipangwa
kufanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat tarehe 23 Machi
2018. Matangazo ya mkutano huo yalitaka Watanzania watakaopenda
kushiriki wajisajili kabla ya siku ya mkutano. Watanzania takriban 200
walijisajili na ubalozi ulifanya maandalizi ya ukumbi, vyakula na
vinywaji kwa ajili ya watu 300 kwenye hoteli ya Golden Tulip.
Siku ya mkutano ilipowadia,
Watanzania zaidi ya elfu moja walijitokeza na kusababisha ugumu wa
kuendelea na mkutano kutokana na maandalizi yaliyofanywa yalilenga watu
300.
Kamati ya maandalizi ilipoona
ukumbi umejaa na watu walio nje ni weng mara mbili zaidi ya watu
waliokuwemo ndani ya ukumbi iliamua kufunga milango na kuwaomba
waliochelewa warejee nyumbani.
Uamuzi huo haukuwafurahisha
watu waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe kwenye ukumbi wa
mkutano, kitendo ambacho kiliashiria uwezekano wa kutokea vurugu kubwa.
Kutokana na uhalisia huo,
Kamati ya maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi wa Watanzania
wanaoishi nchini humo ilishauriana na kuamua kuwa mkutano huo uahirishwe
na maandalizi yaanze upya kwa madhumuni ya kupata ukumbi na huduma
nyingine zitakazokidhi idadi kubwa ya watu.
Kutokana na ufafanuzi huo,
Wizara inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa kipande hicho cha
video kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza kuingia kwenye
ukumbi wa mkutano na sio kwamba wamekusanyika kwenye ofisi ya ubalozi wa
Tanzania kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso
wanayoyapata.
No comments:
Post a Comment